Mwanza/Dar. Utata umeibuka kuhusu taarifa ya chanzo cha kifo cha Rashid Nyandonga (31), kufuatia ukinzania baina ya kinachoelezwa na Polisi Mkoa wa Mwanza dhidi ya maelezo ya familia na mashuhuda.
Wakati polisi wakisema amefariki dunia baada ya kuishiwa nguvu akiwa mikononi mwa askari mgambo, familia na mashuhuda wamedai kuwa, umauti wake umesababishwa na kipigo cha mgambo waliomkamata.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema leo kuwa, marehemu alikuwa akituhumiwa kwa kuuza mirungi.
Amesema kwa kuwa mgambo walikwenda kumkamata, “siwezi kusema imetumika nguvu au haikutumika nguvu, lakini alikimbia na akafukuzwa, baada ya kufukuzwa, akakurupushana na mgambo, siwezi kusema nguvu gani imetumika kumkamata.”
Mtanda amesema kwa sababu kulikuwa na kashkash, ilionekana apelekwe hospitalini moja kwa moja.
“Sitaki kusema amepigwa au hakupigwa tuache uchunguzi wa polisi na wa kitaalamu ufanyike, wao wataalamu watatumbia sasa asilimia ngapi ya ngapi imesababisha ndugu kufa au alikuwa na tatizo la muda mrefu mimi siwezi kujua.”
Pia, mwenyekiti huyo wa kamati ya usalama ya mkoa amesema Serikali haimtumi mtu kuua au kujeruhi lakini kuna ukamataji salama na kuna kudhibiti kama anataka kukimbia, “lakini ndugu wasubiri uchunguzi na ripoti za daktari au mahakamani.”
Hata hivyo, ukinzani huo wa taarifa za kifo cha Nyandonga, haupishani na ule uliotokea katika kifo cha Dafroza Jacob, Novemba 5, mwaka jana. Polisi ilidai amefariki dunia kwa kuishiwa nguvu akiwa anachukuliwa maelezo kituoni, lakini ndugu na jamaa, walidai ameiaga dunia kwa kipigo cha polisi.
Tukio lingine linalofanana na hayo, lilimhusu Mohamed Kisingwe aliyefariki dunia mikononi mwa maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Februari, mwaka huu mkoani Tanga.
Polisi mkoani Tanga, ilisema uhai wa Kisingwe ulikoma, baada ya kuugua presha akiwa mikononi mwa maofisa hao, lakini ndugu zake walidai enzi za uhai wa ndugu yao, hakuwahi kuwa na historia ya ugonjwa huo.
Utata unaogubika taarifa hizo, mwaka 2021, ulisababisha polisi mkoani Mtwara, iunde kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma za kuuawa kwa mfanyabiashara wa madini mkoani humo, ambaye ilidaiwa kifo chake kilitokana na askari hao.
Pia, kamati nyingine iliundwa na jeshi hilo, inayowahusisha askari wafanye uchunguzi wa matukio ya mauaji mkoani Mwanza mwaka 2021.
Akiwa ziarani mkoani Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan aliupinga uamuzi huo wa polisi kuunda kamati ya kuchunguza matukio hayo, kwa kile alichosema, haiwezekani jeshi hilo lituhumiwe na lenyewe liunde chombo cha kujichunguza.
“Nimemwelekeza Waziri Mkuu, aunde kamati nyingine, iende ikafanye uchunguzi wa mauaji. Halafu watuletee taarifa. Lakini wakati huo huo Waziri Mkuu nataka jeshi lako lijitafakari, waone kama kinachotokea ndio misingi ya jeshi la polisi au vinginevyo. Kwa hiyo tutasubiri taarifa ya kamati huru ituletee taarifa, tulinganishe na ile ya polisi tuone inasemaje tuchukue hatua,” alisema.
Katika ripoti yake, kamati hiyo iliyoundwa na Waziri Mkuu, wakati huo akiwa Kassim Majaliwa, iliwatuhumu askari kuhusika na mauaji hayo na wakashtakiwa mahakamani na kuhukumiwa.
Hata hivyo, mwaka 1980 Tanzania ilitunga Sheria ya Kuchunguza Vifo, inayotoa mamlaka kwa Waziri wa Katiba na Sheria kuanzisha Mahakama ya kuchunguza kifo chochote chenye utata katika eneo husika kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.
Hata hivyo, sheria hiyo, haikuonekana kutumika tangu ilipotungwa.
Sheria hiyo inampa Jaji Kiongozi nguvu ya kuteua ofisa mchunguzi wa vifo vya utata ambaye ana mamlaka ya kuamrisha jeshi, daktari na yeyote anayeweza kusaidia katika uchunguzi kufika kuhojiwa na kutoa ushahidi.
Mchunguzi anapogundua ukiukwaji wa utaratibu hupeleka matokeo ya alichogundua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua za kimahakama.
Jana Jumapili, Machi 22, mwaka huu, Polisi mkoani Mwanza, ilitoa taarifa ya kifo cha Nyandonga (31), ikieleza kuwa, amefariki dunia baada ya kuwakimbia askari mgambo waliomuhisi ana dawa za kulevya aina ya mirungi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, ilieleza tukio hilo lilitokea Machi 20, 2026 saa 12:45 jioni katika Mtaa wa Mission, eneo la Sahara, Kata ya Pamba, askari mgambo walipomtilia shaka marehemu kuwa anauza dawa za kulevya aina ya mirungi.
Inaeleza baada ya kuanza kumfuatilia, marehemu alikimbia, akakimbizwa na kukamatwa akiwa na gramu 50 za mirungi kabla ya kuanza kuonesha dalili za kuishiwa nguvu na kupelekwa Hospitali ya Seoko Toure, alikofariki dunia akipatiwa matibabu.
Hata hivyo, shuhuda wa tukio hilo, Otieno Ernest, amesema Nyandoka alikuwa katika ofisi yake na hata mgambo walimkuta eneo hilo na walianza kumzonga wakimshinikiza awape fedha.
Amesema Nyandonga akawa anagoma kutoa fedha, mgambo hao waliendelea kumzonga hadi alipoanza kukimbia na mmoja wao akamkimbiza.
“Nilibaki na wale mgambo wengine, wakiwa na watuhumiwa wengine, wakasema bila Sh50,000 hawamuachi. Nikasema niwape Sh30,000 wakakataa nikawapa Sh40,000 wakaichukua,” amesema.
Baada ya muda, amesema Nyandonga alikamatwa naye walimchukulia Sh40,000 aliyokuwa nayo, kisha simu zake zikakabidhiwa kwake na akaanza kudai anajisikia vibaya.
“Walivyomleta marehemu akaniambia najisikia vibaya…nikamwambia umeumia wapi, hakuwa anaongea zaidi. Nikasema asije akafariki hapa, askari jamii wakatokea nikawambia si mmeshachukua Sh40,000 mchukueni mtu wenu mwende naye,” amesema.
Amesema wakamchukua akiwafuatilia, walipofika eneo la Pamba, Nyandonga alipoteza maisha,”Chanzo cha kifo alipigwa mateke tumboni na alikabwa sana,” amesema.
Kaka wa marehemu Machubu John, amesema siku ya tukio alimuona marehemu akikimbia lakini hakujua kama ni ndugu yake kwa kuwa alikuwa kavaa kofia.
“Baadaye ikapigwa simu kutoka kwa jirani akaanza kuongea na mama, nikasikia mama anashtuka. Nilivyoona simu zinaendelea nikamwambia mama wewe huwezi kufika ngoja niende Seoko Toure ilikuwa saa tatu kasoro usiku,” amesema.
Amesema alipofika hospitali, alikuta tayari ndugu yake amefariki kisha akakabidhi mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti na kurudi nyumbani, kesho yake asubuhi aliongozana na polisi hadi hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
“Wakaanza kumpasua pale tunashuhudia kila kona kila sehemu…wakakuta mapafu yamejifinya, wakapasua mpaka na moyo, wakatoa hadi ubongo wakaangalia hakuna jeraha lolote…
“Basi wakachukua na vipimo vya macho basi tukaambiwa ninyi nendeni tu mkafanye utaratibu wa kuzika hili muachieni mkemia mkuu, taarifa mtaipata,” amedai.
Kwa kuwa mdogo wake ameshafariki, amesema hakuona haja ya kufuatilia taarifa zaidi ya kumzika na kuendelea kuihudumia familia yake ambayo ni watoto wawili aliowaacha.
‘Mwanangu amesingiziwa’
Mama wa marehemu, Anna Gabriel, amesema mwanawe amesingiziwa kwani hajawahi kufanya biashara ya dawa za kulevya kama taarifa ilivyotolewa.
“Kwenda namkuta mtoto wangu amefariki kweli, kumuangalia amechubuka huku mkononi, amechubuka mguuni. Mtoto wangu wamemuonea, mwanangu alikuwa fundi simu lini akawa na maneno ya dawa ya kulevya?
“Hata mkiuliza watu wote mtaani kila mtu anasema nani atakuwa anatutengenezea simu,” amesema.
Mke wa marehemu, Lucia Malima ameiomba Serikali kumtendea haki mumewe ili apumzike kwa amani.
“Kweli ni kuanguka tu? Mbona watu wanaangukaga na hawajawahi kufa? Yaani yeye kuanguka tu ndo afe kweli,” amehoji.
Amesema mumewe alikutwa na mkasa huo, akiwa na rafiki yake eneo la Sahara, mgambo walikuwa wanataka awalipe Sh50,000.
“Rafiki yake akawapa Sh40,000 kwa hiyo Sh10,000 tu ndo imemuua mume wangu. Kama alikuwa ana hatia si wangempeleka polisi kwanini wamuue bila kosa,” amesema.
Ametoa msisitizo kwa Serikali kuhakikisha mumewe anapata haki zake, badala ya kumbambikizia tuhuma ambazo anadai hakuwa anahusika nazo.
“Serikali naombeni mnisaidie. Mimi ni mama, mume wangu ndiyo nilikuwa namtegemea kwa kila kitu, wamemuua halafu bado wamewakingia kifua waliomuua. Mume wangu hana sifa mbaya,” amesema.
Shangazi wa marehemu, Rehema Shabani amesema mgambo hao wamezidi na kusababisha hofu kwa wananchi.
“Mgambo wamezidi, mmoja aliua mtoto na bodaboda tunashangaa ameenda gerezani miezi mitatu na kurudi…tunaomba Serikali itusaidie hawa askari wametutesa wametusumbua huu mtaa…hatupumui watoto ni kila siku kukamatwa kusingiziwa kesi na kupelekwa na kupoteza.
“Tunaomba jamani mimi kama shangazi wa marehemu hawa watu waliomuua wawajibike ila wakirudi mtaani sijui itakuwaje… Tumepoteza sisi nguvu kazi. Kwani mapolisi hawapo mpaka wanakuja askari jamii,” amehoji.
Ameomba mgambo wapigwe marufuku, ikiwezekane askari wastaafu ndio watumike kwa ajili ya shughuli za ulinzi katika maeneo ya jamii.
Awali, ndugu na jamaa walipanga kuandamana hadi Kituo cha Polisi cha Pamba, kisha kuutelekeza mwili wa marehemu hapo, lakini kutokana na mvutano wa vijana wa mtaani hapo, marafiki na ndugu ikaamuliwa azikwe wakati wakisubiri kuona sheria inafuata mkondo wake.
Hadi majira ya saa saba mchana leo, bado hali haikuwa inaeleweka, iwapo mwili utapelekwa polisi au utazikwa, hata hivyo, baadaye walikubaliana waende kuzika.
Tayari mwili wa marehemu umezikwa katika makaburi ya Igogo baada ya familia, ndugu na marafiki kukubaliana wakampumzishe ndugu yao kisha kupigania haki yake.
