Bagamoyo. Wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule ni moja ya changamoto zinazoripotiwa mara kwa mara nchini.
Sababu kuu ni mchanganyiko wa sababu za kijografia, hamahama ya baadhi ya jamii, uchaguzi wa shule zenye matokeo mazuri bila kuzingatia umbali, na baadhi ya shule kuwa mbali na makazi ya watoto.
Vilevile, uchumi wa familia, kutokuwepo kwa mabweni, gharama kubwa za bweni, na changamoto za usafiri pia ni vikwazo vinavyoongeza ugumu wa kupata elimu kwa wakati.
Utafiti uliofanywa katika Jiji la Mwanza mwaka 2024 na kuchapishwa Juni 14, 2025 katika jarida la International Journal of Teaching, Learning and Education (IJTLE) unaonesha moja ya sababu inayochangia umbali mrefu wa wanafunzi kwenda shule ni upungufu wa miundombinu ya usafiri wa umma, hususan katika maeneo ya vijijini.
Utafiti huo pia unaonesha umbali mrefu kati ya makazi na shule, pamoja na hali duni ya kiuchumi ya baadhi ya wazazi, husababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo mara kwa mara.
Utafiti mwingine uliofanywa na Global Road Safety Facilities kwa kushirikiana na World Bank Group katika Wilaya ya Mkuranga, na kuchapishwa Juni 30, 2023, unaonesha kuwa baadhi ya wanafunzi vijijini hutumia takribani saa moja kwa miguu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Ripoti ya Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha kuwa asilimia 92.6 ya wanafunzi wa shule za msingi nchini hufika shuleni kwa kutembea, hali inayoongeza muda wanaopoteza wakiwa njiani.
Wanafunzi wa vijijini huchukua wastani wa dakika 31.5 kufika shuleni, ikilinganishwa na dakika 29.4 mwaka 2014/2015, huku wanafunzi wa mijini wakitumia wastani wa dakika 25.5, ongezeko dogo la muda wa safari.
Utafiti huo ulihusisha kaya 3,352 nchini, ikijumuisha Zanzibar kupitia Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS).
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mkenge, aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma, amesema moja ya sababu inayochangia baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu ni pamoja na kukosekana kwa usafiri wa umma katika baadhi ya vijiji.
Ametolea mfano kijiji cha Mkenge kinachopatikana kilometa 11 kutoka barabara kuu hakina usafiri wa umma.
“Ili kufika kituoni tu kutoka kijijini, unatakiwa kulipa Sh5,000, gharama hiyo ni kubwa kwa baadhi yetu,” amesema.
Amesema kungekuwa na miundombinu mizuri ya barabara, daladala au bajaji za kuchangia zingekuwa zinapita katika barabara hizo, ingesaidia kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea pamoja na gharama kwa mzazi.
“Baada ya kutembea umbali mrefu au kupanda pikipiki, ambayo ni gharama, wanaweza kutumia daladala au bajaji za kuchangia ambazo zitasaidia kupunguza changamoto hiyo,” ameeleza.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkenge kilichopo Kata ya Fukayosi, Said Bwanga, amesema sababu nyingine inayochangia uwepo wa changamoto hiyo ni ukubwa wa maeneo ya kijografia.
Bwanga ametolea mfano kuwa katika Kata ya Fukayosi kuna shule ya sekondari, lakini kutokana na ukubwa wa kata hiyo na baadhi ya vijiji kuwa mbali na shule hiyo, jambo hilo linapelekea baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
“Hiyo ndiyo sababu katika kijiji chetu, kwa nguvu ya wananchi kwa kushirikiana na wadau, tumeanza mchakato wa ujenzi wa shule ya sekondari ili kuongeza idadi ya shule katika kata yetu na kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu,” amesema.
Pia amesema katika Shule ya Sekondari Fukayosi wamejenga mabweni ambayo pia yanasaidia kupunguza changamoto hiyo ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Kuhusu malalamiko ya wazazi ya gharama za bweni ya Sh770,000 kwa mwaka, Diwani wa Fukayosi, Mrisho Some, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda, wamesema hawajapokea malalamiko yoyote juu ya gharama hiyo kutoka kwa wakazi wa eneo hilo.
Pia wamesisitiza kuwa upangaji wa gharama hiyo ulikuwa shirikishi kupitia vikao vya wazazi na shule.
Athari za wanafunzi kutembea umbali mrefu
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkenge, Xavery Mtunze, amesema amepokea kesi kadhaa za watoto kuacha shule, na baadhi ya wazazi kuwataka watoto kujifelisha kwa makusudi darasa la saba kwa kuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za kuwapeleka shule.
Amesema sababu ya wazazi kuchukua hatua hiyo ni uoga wa kukamatwa kwa kushindwa kumpeleka mtoto shule, hivyo wanaingia makubaliano na watoto wao kufanya vibaya ili wasifaulu.
Mdau na mtafiti wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko, amesema tafiti mbalimbali zinaonesha mwanafunzi anayetembea umbali mrefu kwenda shule yuko katika hatari kubwa zaidi ya kuacha shule ikilinganishwa na yule anayeishi karibu.
Mbali na hilo, ameeleza kuwa umbali mrefu huathiri uwezo wa mwanafunzi kujifunza darasani kwa sababu wengi hufika wakiwa wamechoka kutokana na kutembea muda mrefu.
“Unakuta mwanafunzi anafika darasani akiwa amechoka, hivyo inakuwa vigumu kwake kuzingatia masomo. Hali hiyo huathiri ufaulu wake katika mitihani na hata uwezo wa kupata maarifa stahiki,” amesema Dk Nkoronko alipozungumza na Mwananchi.
Mtaalamu wa saikolojia, Hussein Omary, amesema kutembea kwa miguu kwenda shule kunaweza kuyumbisha akili ya mtoto na kumfanya ashindwe kuwaza masomo kwa kiasi kikubwa, na badala yake awaze aliyokutana nayo njiani.
“Akili ya binadamu inahitaji utulivu ili kufanya kitu kwa ufanisi. Kama mtoto atatembea kwa miguu tena kwa umbali mrefu, njiani anakutana na vitu vingi, pengine vitamfanya aviwaze zaidi kuliko masomo ya siku hiyo,” amesema.
Pia, amesema hofu ya kuadhibiwa pindi anapofika shule akiwa amechelewa yaweza kumuathiri kisaikolojia na kumfanya kukosa utulivu.
Mdau wa elimu, Catherine Sekwao, amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, baadhi ya wazazi huamua kuwapangia watoto vyumba jirani na shule.
Amesema hatua hiyo inaweza kuwasaidia kupunguza changamoto hiyo, lakini kama hakuna usimamizi, inaweza kuwaweka wanafunzi, hasa wa kike, kuingia katika vishawishi.
Pia, changamoto ya usafiri inaweza kuwafanya kuingia katika vishawishi vya kupewa lifti, jambo linalowaweka katika hatari ya kupata ujauzito na maambukizi ya magonjwa ya ngono.
Ameshauri kuwa katika maeneo yenye changamoto hiyo ni vyema katika shule kuwe na mabweni yatakayokuwa na gharama nafuu kwa mzazi.
Hiyo itasaidia wanafunzi wote wanaokaa mbali na shule kukaa katika mabweni yaliyojengwa shuleni.
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Kitaaluma cha Gitoya (G-CARD) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) mwaka 2021, ulioitwa:
“Mtazamo wa wadau wa elimu kuhusu athari za umbali wa shule kutoka nyumbani katika ufaulu wa wanafunzi miongoni mwa shule za sekondari za Serikali katika Wilaya ya Rorya,’ ulionesha umbali mrefu unamsababisha mwanafunzi kuchelewa kufika shule na kukosa baadhi ya masomo, hivyo kuwa katika hatari ya kutofanya vizuri kwenye masomo.
“Umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni unawafanya wanafunzi wengi kuchelewa kufika shuleni na kukuta masomo yameanza, jambo linalosababisha kukosa sehemu ya utangulizi au kipindi chote kinachoanza mapema,” inaeleza ripoti ya utafiti huo.
Inaongeza: “Baadhi ya wanafunzi hufika wakiwa wamechoka na kutokwa na jasho kutokana na safari ndefu. Uchovu kwa wanafunzi husababisha umakini duni na kupelekea kuwapo kwa ufaulu duni kwa wanafunzi hao.”
