Chadema kibarua tena leo mahakamani Dodoma

Dar es Salaam. Mawakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Jumanne, Machi 24, 2026 watakuwa na kibarua kingine kuishawishi mahakama wakati wa usikilizwaji wa mashauri manne yanayotokana na kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili.

Mashauri hayo ya mapitio yaliyopewa usajili wa maombi ya mapitio namba 1/2026, 2/2026, 3/2026 na 4/2026 yameitishwa na Mahakama ya Rufani yenyewe, kwa utaratibu ujulikanao kwa lugha ya kisheria kama suo moto, kufuatia barua ya malalamiko ya Chadema kwa Jaji Mkuu.

Suo moto ni hatua inayochukuliwa na mahakama/jaji kwa mamlaka yake kisheria kuibua jambo/hoja au kuitisha shauri kwa utashi wake bila kuombwa na wadaawa ili kulinda haki na usawa, kurekebisha kasoro au makosa ya wazi katika mwenendo wa shauri au kushughulikia mambo muhimu ya kisheria.

Kufuatia barua hiyo ya malalamiko ya Chadema kuhusiana na mwenendo wa kesi hiyo na mashauri madogo yaliyotokana na kesi ya msingi, Jaji Mkuu, George Masaju alimwelekeza Msajili wa Mahakama ya Rufani yafunguliwe mapitio kwa ajili ya kesi ya msingi na mashauri yake madogo.

“Tufungue jalada kwa ajili ya mapitio ya shauri la madai Na. 8323 la mwaka 2025 pamoja na maombi yake ya nyongeza katika Masjala Ndogo ya Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Dar es Salaam,” inasomeka sehemu ya hati ya maelekezo ya Jaji Mkuu, ambayo Mwananchi limeiona.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo ya Jaji Mkuu, lengo la kufunguliwa kwa mapitio hayo ni mahakama hiyo kujiridhisha na uhalali na usahihi wa mwenendo wa mashauri hayo.

Hatua hiyo kwa mujibu wa maelekezo hayo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 6(3) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani (Sura ya 141, Toleo la mwaka 2023), kikisomwa pamoja na kanuni ya 65(1), (6) na (7) za Kanuni za Mahakama ya Rufani.

“Hii ndiyo kusema kwamba haya ni mapitio yaliyoanzishwa na Mahakama yenyewe (suo moto),” amebainisha Jaji Mkuu katika maelekezo hayo kwa msajili.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo, mapitio hayo yatasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Dodoma, linaloongozwa na Jaji Augustine Mwarija; Jaji Issa Maige na Jaji Abraham Mwampashi leo Machi 24, 2026, na au tarehe nyingine yoyote itakayofaa kadiri itakavyoamuliwa.

Mashauri yanayohusika katika mapitio hayo ni pamoja na:

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo wanaomba Mahakama hiyo itamke wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Wadai walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa kutokujihusisha na shughuli za kisiasa na matumizi ya mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa Juni 10, 2025 ilikubaliana na maombi na hoja za wadai na ikatoa amri hizo zilizoombwa, yaani iliamuru wadaiwa kutokujihusisha na shughuli za kisiasa na kutokutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Baadaye mahakama hiyo, kupitia Naibu Msajili, ilitoa ufafanuzi wa makundi ya watu wanaofungwa na uamuzi huo ambao kimsingi unawafunga watu wote tangu viongozi wa juu mpaka wa chini kabisa na hata wanachama na watu wengine kwa niaba ya chama hicho.

Juni 23, 2025 walalamikiwa waliandika barua ya kumkataa Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo, wakimtaka ajiondoe kusikiliza kesi hiyo na mashauri mengine madogo wakidai hawana imani naye.

Jaji Mwanga baada ya kusikiliza sababu zao za kumkataa, katika uamuzi wake alioutoa Julai 28, 2025, alitupilia mbali hoja zao akieleza hazikuwa na msingi wa kisheria kwa kuwa hazikuwa miongoni mwa sababu za kisheria za kumfanya jaji kujiondoa kwenye kesi.

Walalamikaji walifungua shauri dogo wakiomba mahakama iwaamuru walalamikiwa wawapatie nyaraka mbalimbali zinazoonesha mali za chama na za vikao kuanzia mwaka 2019 mpaka 2024, wazitumie katika kesi hiyo.

Nyaraka hizo zilikuwa ni Tamko la Mwaka la Mali zinazomilikiwa na chama hicho; taarifa za kifedha za chama hicho zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na miktasari ya vikao vya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.

Nyingine zilikuwa miktasari yote ya agenda za vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho, miktasari yote ya agenda za vikao vya Kamati Maalumu ya Zanzibar, na miktasari yote ya agenda za vikao vya Sekretarieti ya Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema Zanzibar.

Vilevile, taarifa za kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, iliyoko katika Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce Limited).

Jaji Mwanga katika uamuzi wake Septemba 29, 2025 kwanza alitupilia mbali hoja za walalamikiwa kupinga kutoa nyaraka hizo akisema kuwa hazikuwa na mashiko huku akikubaliana na hoja za walalamikaji.

Hata hivyo, Jaji Mwanga aliamuru waombaji wapewe aina tatu tu za nyaraka hizo huku akiwakatalia aina nne.

Nyaraka hizo ambazo mahakama hiyo imewaamuru walalamikiwa waziwasilishe mahakamani ni pamoja na Tamko la Mwaka la Mali zinazomilikiwa na chama hicho, taarifa za kifedha za chama hicho zilizokaguliwa na CAG na taarifa za kibenki za akaunti hiyo.

Nyaraka zinazohusu agenda na miktasari ya vikao, Jaji Mwanga aliwakatalia waombaji/walalamikaji akisema kuwa hawakuainisha tarehe za vikao walivyohitaji na kwamba haiwezekani kuwapatia nyaraka zote kwani baadhi ya vikao ni vya siri ambavyo havipaswi kutolewa hadharani.

Wakati wa usikilizwaji wa mapitio hayo, mawakili wa Chadema watakuwa na kibarua cha kukinusuru chama hicho kutoka katika mkwamo uliotokana na kesi hiyo kwa kuishawishi mahakama kuwa Mahakama Kuu ilifanya makosa katika mwenendo na amri zake.

Jopo la mawakili wa Chadema linaongozwa na Wakili Mwandamizi, Mpale Mpoki. Wengine ni Dk Rugemeleza Nshala (Mwanasheria Mkuu wa Chadema), Gaston Garubindi (Mkurugenzi wa Sheria Chadema), Dickson Matata (Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema), Hekima Mwasipu na wakili Nashon Nkungu.

Walalamikaji wanawakilishwa na mawakili Shaaban Marijan, Gido Semfukwe na Alvan Fidelis.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi…