Watu wasiopungua 66 wamefariki dunia baada ya ndege ya kijeshi kuanguka muda mfupi baada ya kupaa nchini Colombia, magharibi mwa msitu wa Amazon.
Ndege hiyo ya kijeshi iliyokuwa imebeba watu 128, wengi wao wakiwa wanajeshi, imeanguka karibu na mji wa Puerto Leguizamo na kusababisha vifo hivyo huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Mkuu wa majeshi ya Colombia, Hugo Alejandro López Barreto, amethibitisha kuwa wanajeshi 66 wamepoteza maisha katika ajali hiyo, huku watu wengine wakiendelea kupatiwa matibabu. Aidha, amesema kuwa askari wanne bado hawajulikani walipo.
Baadhi ya wanajeshi na wananchi wa jirani na ajali ilipotokea wakiwa katika eneo hilo kwa uokoaji. Picha na Mtandao
Amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ajali hiyo imesababishwa na shambulio la makundi ya waasi, akibainisha kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Miili ya marehemu imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha mji huo mdogo, huku majeruhi wakihudumiwa katika vituo viwili vya afya vilivyopo jirani kabla ya kusafirishwa kwenda hospitali kubwa katika miji mingine, ikiwemo mji mkuu Bogotá.
Eneo la Puerto Leguizamo lipo katika Jimbo la Putumayo, karibu na mipaka ya Ecuador na Peru, na linazungukwa na msitu mnene wa Amazon, hali iliyosababisha shughuli za uokoaji kuwa ngumu.
Baadhi ya wanajeshi na wananchi wa jirani na ajali ilipotokea wakiwa katika eneo hilo kwa uokoaji. Picha na Mtandao
Waziri wa Ulinzi wa Colombia, Pedro Sánchez amesema ndege hiyo ilikuwa ikisafirisha wanajeshi kuelekea mji mwingine ndani ya jimbo hilo kabla ya kupata hitilafu na kuanguka umbali wa takribani kilomita mbili kutoka uwanja wa ndege.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni zinaonesha moshi mzito ukifuka kutoka eneo la tukio, huku wanajeshi na wakazi wa eneo hilo wakikimbia kusaidia uokoaji. Baadhi ya majeruhi waliondolewa kwa kutumia pikipiki za wakazi wa eneo hilo kutokana na ugumu wa miundombinu.
Kamanda wa jeshi la anga la Colombia, Carlos Fernando Silva, amesema bado haijafahamika chanzo cha ajali hiyo, lakini alidokeza kuwa ndege hiyo ilipata hitilafu baada ya kuruka.
Ndege iliyokuwa imebeba watu 128 ikiwaka moto baada ya kupata ajali muda mfupi baada ya kupaa. Picha na Mtandao
Ndege hiyo aina ya Lockheed C-130 Hercules iliripotiwa kuwa ilitolewa na Marekani kwa Colombia mwaka 2020, na ilifanyiwa ukaguzi wa kiufundi miaka mitatu iliyopita.
Mchambuzi wa masuala ya anga, Erich Saumeth, amesema ni mapema kubaini chanzo cha ajali hiyo, lakini ameeleza kuwa uchunguzi utazingatia uwezekano wa hitilafu ya injini, hasa ikizingatiwa kuwa ndege hiyo ina injini nne.
Rais wa Colombia, Gustavo Petro ametoa wito kufanyika maboresho ya vifaa vya kijeshi, akidai kuwa juhudi za kisasa zimekuwa zikikwamishwa na urasimu. Pia amesisitiza kuwa maofisa wasio na uwezo wanapaswa kuwajibishwa.
Kikosi cha huduma ya kwanza kikitoa msaada kwa kuwapa huduma ya kwanza majeruhi walionusurika katika ajali hiyo. Picha na Mtandao
Hata hivyo, wakosoaji wa serikali wameeleza kuwa kupunguzwa kwa bajeti ya jeshi kumesababisha kupungua kwa saa za kuruka kwa ndege za kijeshi, hali inayoweza kuathiri uzoefu wa marubani.
Ajali hiyo imeacha taifa la Colombia katika majonzi, huku juhudi za uokoaji na uchunguzi zikiendelea.
