Kuelekea uzinduzi wa WazoHuru Air BnB Apartments Mtaa wa Unyankae-Miembeni Manispaa na Mkoa wa Singida, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Wazohuru Media Group Limited amechangia vifaa vya michezo kwenye shule za msingi katika Manispaa ya Singida vyenye gharama ya shilingi Milioni 4.2
Vifaa hivyo vya michezo ni pamoja na jezi Jozi moja yenye jezi 16 na mpira mmoja katika shule ya Msingi Tumaini Viziwi, S/M Ukombozi, S/M Kindai, S/M Sumaye, S/M Mtipa na S/M Unyankae.
Pia amechangia Jozi moja yenye jezi 16 na mpira mmoja kwa timu ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) Manispaa ya Singida kwa ajili ya kuanza mashindano ya michezo hiyo mwaka huu 2026.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mathias Canal amesema kuwa Lengo kuu la zoezi hilo ni kuhamasisha michezo mashuleni, kukuza vipaji vya wanafunzi, pamoja na kuchangia maendeleo ya afya na ustawi wa watoto.
Ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine lakini pia kampuni yake imekabidhi vifaa hivyo vya michezo ikiwa ni sehemu ya mrejesho katika jamii baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo 7 ya WazoHuru Apartments.
Mathias amebainisha kuwa tarehe 28 Machi 2026, kuanzia saa kumi na mbili kamili jioni (12:00) mradi huo wa eneo hilo la makazi ya kisasa utazinduliwa ambapo mgeni rasmi katika tukio hilo atakuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Halima Dendego.








