Serikali ya Kenya Yatoa Msamaha kwa Wakenya Waliojiunga na Vita vya Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi

Raia wa Kenya waliojiunga kupigana vita kwa niaba ya Urusi dhidi ya Ukraine watapewa msamaha watakaporejea nyumbani,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi.

Tangazo hilo linafuatia ziara ya hivi karibuni ya Mudavadi mjini Moscow, ambapo alijadiliana kuhusu suala hilo na kukubaliana kuwa hakutakuwa na ajira zaidi za Wakenya kwenda Urusi kwa ajili ya kupigana vita.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, ni kinyume cha sheria kwa raia wake kujiunga na majeshi ya kigeni, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Wizara ya Mambo ya Nje inakadiria kuwa Wakenya 252 wamesajiliwa kinyume cha sheria kupigana mstari wa mbele hali iliyoanza takriban miezi sita iliyopita na pia kuwahusisha Waafrika kutoka nchi nyingine.

Baadhi ya Wakenya wamesema walidanganywa kwa ahadi za kazi za kiraia zenye mishahara mizuri, lakini walipoenda wakajikuta wanalazimishwa kupigana katika vita nchini Ukraine, mara nyingi wakisaini mikataba kwa lugha ya Kirusi bila kuielewa.

Mudavadi alisema kuwa hadi sasa: Wakenya 44 wamerudishwa salama nyumbani, 11 wanaripotiwa kupotea au kufariki vitani, 38 wamelazwa hospitalini Urusi chini ya uangalizi maalum, Wengine 160 bado wako vitani.

Aidha, alifanikiwa kufikia makubaliano kwamba Wakenya walioko mstari wa mbele ambao hawataki kuendelea na vita wanaweza kujiondoa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Urusi pia imekubali kuiweka Kenya kwenye orodha maalum ya kuzuia usajili mpya wa raia wake.
Hapo awali, Urusi imesisitiza kuwa wapiganaji wote wa kigeni walijiunga kwa hiari na kwa kufuata sheria za nchi hiyo.

Ziara ya Mudavadi ilifuatia shinikizo kutoka kwa familia za Wakenya waliokwenda Urusi wakitaka serikali ichukue hatua.

Stori na Elvan Stambuli, Global Digital