Global Publishers
March 24, 2026
0 Comments
Ndege ya Jeshi iliyokuwa imebeba takribani watu 125, wengi wao wakiwa wanajeshi, imeanguka muda mfupi baada ya kupaa katika mji wa Puerto Leguizamo nchini Colombia, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 66 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, ajali hiyo imetokea ghafla baada ya ndege hiyo kushindwa kuendelea na safari yake muda mfupi baada ya kuondoka uwanjani. Tukio hilo limeacha taharuki kubwa katika eneo hilo la Amazon.
Naibu Meya wa eneo hilo, Carlos Claros, amesema kuwa takribani watu 81 wamejeruhiwa katika ajali hiyo, huku juhudi za uokoaji zikiendelea kwa kasi kwa ushirikiano wa vikosi vya uokoaji na wakazi wa eneo hilo.
Waokoaji wamekuwa wakijitahidi kuwahamisha manusura na kuwapeleka katika vituo vya matibabu vilivyo karibu.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Colombia, Pedro Sanchez, amethibitisha kuwa ndege hiyo ilikuwa ikiwapeleka wanajeshi katika jimbo la Amazon karibu na mipaka ya Ecuador na Peru. Ameongeza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na shambulio kutoka kwa makundi ya waasi wanaofanya shughuli katika eneo hilo.
Jeshi la anga linaendelea kufanya uchunguzi kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, huku taarifa zikieleza kuwa baadhi ya manusura wameokolewa wakiwa na majeraha mbalimbali. Wakati huo huo, video zinazosambaa mitandaoni zinaonyesha wanajeshi wakisaidiwa kuondolewa eneo la tukio na wakazi, huku wengine wakijaribu kuzima moto uliosababishwa na ajali hiyo.
Tukio hilo linatajwa kuwa moja ya ajali mbaya zaidi za ndege za kijeshi nchini Colombia katika miaka ya hivi karibuni, huku taifa hilo likiendelea na uchunguzi wa kina kubaini kilichosababisha janga hilo.