Unguja. Licha ya wanawake kukumbana na changamoto kwa muda mrefu, imeelezwa kuwa mwanga na matumaini yameanza kuonekana kufuatia kuongezeka kwa uelewa, ujasiri na ushiriki wao katika siasa na uongozi.
Hayo yamebainika Machi 24, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyowakutanisha wadau mbalimbali Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi Wanawake (Tamwa ZNZ), Nairat Abdulla Ali, amesema wanawake kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kushiriki kisiasa kutokana na mifumo dume, lakini kwa sasa kuna hatua zimeanza kuonekana.
Ametolea mfano uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ambapo wanawake 809 walijitokeza kushiriki chaguzi za ndani ya vyama, huku 324 wakiteuliwa.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar wanawake walijitokeza kugombea nafasi ya urais, hii ni hatua kubwa ya kihistoria,” amesema.
Hata hivyo, amesema kati ya washindi 210, wanawake walikuwa 35 pekee sawa na asilimia 17, akisisitiza bado kuna kazi kubwa ya kuongeza ushiriki wao.
Amesema uwiano wa asilimia 50 kwa 50 bado haujafikiwa, huku akibainisha kuwa viti maalumu vinaendelea kusaidia kuongeza idadi ya wanawake, ambapo kwa sasa Baraza la Wawakilishi lina asilimia 32 ya wanawake.
Mwakilishi wa balozi wa Norway, Anette Petterson, amesema wanawake si washiriki tu bali ni viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko, akibainisha kuwa mafanikio yanayoonekana yametokana na uwekezaji na juhudi za wadau mbalimbali.
“Usawa wa kijinsia si suala la haki tu bali ni nguvu ya pamoja,” amesema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (Juwauza), Salma Saadat, amesema wanawake wanapaswa kupewa heshima, thamani na usawa, huku wakichukua hatua pale haki zao zinapokiukwa.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (Zafela), Salma Zain, amesema wanaendelea kupitia sheria zinazowakwamisha wanawake ili kuboresha hali yao kiuchumi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (Pegao), Hafidh Abdi Said, amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko na hawapaswi kuwa wanyonge.
“Wanawake ni wengi, wanapaswa kujitokeza na kuchangamkia fursa bila kujiwekea mipaka,” amesema.
Ofisa programu kutoka Pamoja Youth Initiative (PYI) amesema ushiriki wa wanawake una mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.