Watoto 162,099 Maswa kupatiwa chanjo ya matone ya polio.

Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Vincent Anney, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi 10 wanapatiwa chanjo ya matone ya polio ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo, unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.

Rai hiyo imetolewa leo Machi 24, 2026 wakati akizindua rasmi kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio wilayani humo, ambapo jumla ya watoto 162,099 wanatarajiwa kufikiwa.

Amesema utoaji wa chanjo hiyo ni hatua ya tahadhari baada ya kubainika kuwepo kwa kirusi kinachosababisha ugonjwa wa polio katika moja ya mikoa ya kanda ya Ziwa.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Polio. Picha na Samwel Mwanga

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imeamua kutoa chanjo katika mikoa sita ambayo ni Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Singida ili kuzuia uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo.

“Naomba niwatoe hofu wananchi, hakuna mtu aliyepatikana na ugonjwa wa polio. Baada ya kufanya vipimo kwenye maji, ilionekana kuna vimelea vinavyoweza kusababisha ugonjwa huo, ndipo Serikali ikaamua kuchukua tahadhari kwa kutoa chanjo,” amesema.

“Chanjo hii haina madhara yoyote kwa mtoto, na hata mtoto akipewa matone haya hatapata maumivu wala kulia,” amesema.

Anastela Celestine ambaye ni muuguzi wa hospitali ya Wilaya ya Maswa akitoa chanjo ya matone ya Polio kwa wanafunzi wa shule ya msingi Binza. Picha na Samwel Mwanga

Kwa mujibu wa Mratibu wa chanjo Wilaya ya Maswa, Abel Machibya amesema kuwa shughuli hiyo  itafanyika katika vituo 401 vilivyoandaliwa wilayani humo, huku vituo 39 vikiwa katika hospitali ya wilaya hiyo ambavyo vitahudumia maeneo jirani na mji wa Maswa.

Amesema lengo ni kuhakikisha watoto wote wenye umri husika wanapatiwa chanjo hiyo ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Mkazi wa Maswa, Maria Aron, amesema hatua hiyo ni muhimu na kuwahimiza wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo.

Kwa upande wake, Pili James amesema ugonjwa wa polio ni hatari, hivyo ni vyema wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo mapema.

Baadhi ya wakinamama waliojitokeza katika hospitali ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya ugonjwa wa Polio. Picha na Samwel Mwanga

“Ni ugonjwa hatari sana. Hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake anapooza, hivyo chanjo hii ni muhimu kwao,” amesema.

Naye Mratibu wa Chanjo kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Boniface Mabonesho, amesema taasisi yao inashirikiana na Serikali kuhakikisha hatua ya uchanjaji  inafanikiwa na kila mtoto anayestahili anapatiwa chanjo.

Amesema timu za wahudumu wa afya na wadau wengine zimeandaliwa kuwafikia watoto katika vituo vilivyopangwa pamoja na maeneo ya jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Kampeni hiyo ya chanjo ya matone ya polio itafanyika kwa siku nne, kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026, katika maeneo mbalimbali wilayani Maswa.