Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 26, 2026 kutoa hukumu katika kesi ya wizi wa mafuta na kuharibu bomba la mafuta inayomkabili aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tino Ndeketa (45) na wenzake saba.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 30189 ya mwaka 2024 yenye mashtaka manne yakiwemo ya kuharibu miundombinu, kutakatisha fedha na wizi na mafuta yenye thamani ya Sh33 milioni mali ya TPA.
Mbali na Ndeketa ambaye ni mkazi wa Tungi Kigamboni, wengine ni wafanyabiashara, Fikiri Kidevu (33), Amani Yamba (53), Mselem Abdallah (44) Kila Sangiti (30) maarufu kama mudy mzeze, Twaha Salumu (47) maarufu Mwarabu, Gaudence Shayo na Hamis Hamis (49) mkazi wa Kigamboni.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Machi 24, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea.
Hakimu Nyaki amepanga tarehe hiyo, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi wanane waliyoutoa mahakamani hapo, lakini pia washtakiwa kumaliza kujitetea.
“Baada ya washtakiwa kumaliza kujitetea, mahakama hii inapanga kutoa hukumu Alhamisi ya wiki hii, ambayo itakuwa Machi 26, 2026, hivyo washtakiwa kwa muda wote huu mtaendelea kubaki rumande hadi siku hiyo ya hukumu,” amesema Hakimu Nyaki na kisha kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, 2026.
Awali, kabla ya kupangiwa tarehe hiyo, wakili wa Serikali, Titus Aron aliieleza Mahakama kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya washtakiwa waliosalia kumaliza kujitetea na upande wa Jamhuri wapo tayari.
Katika utetezi wao, washtakiwa hao walidai kuwa wao hawahusiki na tuhuma hizo na wanaiomba Mahakama iwaachie huru.
Katika mashtaka hayo manne, mawili ni ya uharibifu wa mali wanayodaiwa kutenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi, Kigamboni, ambapo siku hiyo waliharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya petroli na dizeli mali ya TPA.
Pia wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2020 eneo la Tungi Kigamboni, waliiba lita 16,225 za mafuta ya dizeli yenye thamani ya Sh33.9 milioni mali ya TPA.
Siku na eneo hilohilo, washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh33.9 milioni, wakati wakijua zinatokana na kosa tangulizi la wizi.
Kwa mara ya kwanza, walipandishwa kizimbani Oktoba 22, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.
