Kamati ya PAC wakutana na kilio cha bando, wananchi walalama

Babati. Kilio cha gharama na ufanisi wa mabando ya intaneti kimeibuka tena baada ya wananchi wa Kata ya Qash, Wilaya ya Babati mkoani Manyara kulalamika kuwa mabando yao huisha haraka bila kuelewa sababu.

Malalamiko hayo yalitolewa Machi 23, 2026 mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotembelea eneo hilo kukagua mnara wa mawasiliano uliojengwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na kampuni za simu, ikiwemo Vodacom.

Mkazi wa Kitongoji cha Maweni, Angelina Aloyce, alisema wananchi wamekuwa wakijiuliza kwa muda mrefu sababu ya mabando kuisha haraka.

“Tunataka kujua kuna shida gani, maana tunaweka bando linaisha kama limechukuliwa na upepo,” alisema.

Wananchi pia walilalamikia ukosefu wa umeme, wakisema hulazimika kuchaji simu kwa sola hali inayochangia kuharibika kwa vifaa vyao.

Aloyce alisema kabla ya kujengwa kwa mnara huo, walilazimika kupanda miti au kwenda maeneo maalumu kupata mtandao.

Akijibu, mwakilishi wa Vodacom Kanda ya Kaskazini, George Mng’ong’o, alisema mara nyingi mabando huisha haraka kutokana na matumizi ya data bila mtumiaji kutambua, hasa kwenye simu za kisasa.

Aliahidi kampuni hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya intaneti na udhibiti wa data.

Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Balozi Valentino Mlowola, alisema mnara wa Qash ni sehemu ya mradi wa kitaifa wa minara 758 uliogharimu Sh180 milioni, ndani ya uwekezaji wa Sh126 bilioni uliolenga kupanua mawasiliano vijijini.

Alisema zaidi ya wananchi milioni 8.5 wamenufaika na mradi huo, huku Mkoa wa Manyara ukipokea zaidi ya Sh800 milioni. Mradi huo ulitekelezwa kwa ushirikiano na kampuni za Airtel, TTCL, Yas, Halotel na Vodacom.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PAC, Devotha Minja, aliwahimiza wananchi kutumia mawasiliano kukuza uchumi wao, huku akiahidi kuwasilisha bungeni changamoto ya umeme ili itafutiwe ufumbuzi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo hilo, Daniel Sillo.