Wale wa kubania ushuzi, mnalijua hili…

Dar es Salaam. Umewahi kujamba mbele ya mwenza wako, rafiki au wafanyakazi wenzako? Achana na aibu na fedheha ulioipata, kitaalamu ulifanya tendo sahihi kwa masilahi ya afya yako.

Kwa taarifa yako, kubania ushuzi kunakuweka katika hatari ya kupatwa na magonjwa kadhaa yasiyoambukiza, ikiwemo saratani, kama ilivyofafanuliwa katika ripoti za tafiti mbalimbali na wataalamu wa afya.

Aibu inayowakabili wengi katika kujamba, ndiyo inayowafanya baadhi kulifanya tendo hilo sirini au kwa kujificha. Wakati mwingine watu hujibana hasa wanapokuwa mbele ya wengine na Nelson Chacha ni shuhuda wa hilo.

Chacha, anasimulia maisha yake na mkewe yaliyotimiza miezi sita sasa, bila hata mmoja kuwahi kumshuhudia au kumsikia mwenzake akijamba au kuhisi ushuzi. Wanaona fedheha kufanya hivyo mbele ya mwingine.

“Huwa naona fedheha kufanya hivyo mbele ya mke wangu, mara nyingi najibana kufanya hivyo akiwa karibu na mimi, ikitokea nimebanwa kuna mawili ama niende chooni au nje ya nyumba la sivyo nitajibana,” anasema.

Kama ilivyo kwa Chacha, Hawa Kimwaga naye, mara nyingi hubania ushuzi hasa anapokuwa kwenye mazingira yake ya kazi hadi nyumbani anapokuwa na mumewe.

“Huwa nahisi fedheha kufanya hivyo mbele ya mume wangu, sipo huru kabisa kutoa ushuzi nikiwa nyumbani au ofisini, kuna nyakati najibana hadi nahisi tumbo limejaa gesi,” anasema.

Kwa mujibu wanasayansi, ushuzi unatokea kutokana na hewa iliyozamishwa wakati wa kula, kunywa au kuzungumza, pia vyakula vinavyovunjwa na bakteria wa tumboni huku harufu ya ushuzi ingawa inachukiza, ina manufaa kwa afya ya binadamu.

Utafiti uliochapishwa katika mtandao wa Chuo kikuu cha Exter, Uingereza, uligundua gesi hiyo inayojulikana kama Hydrogen Sulfide ambayo pia hupatikana katika mayai yaliyooza, ni muhimu katika kutibu baadhi ya magonjwa kama ya moyo, akili na hata saratani.

Mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Salehe Pazi, anasema kujizuia mara chache si tatizo, lakini kufanya hivyo mara kwa mara kunasababisha madhara ikiwemo saratani ya utumbo.

Anasema ushuzi ni hewa chafu ambayo inabidi itoke, hivyo unapoibana isitoke, unabakiza uchafu katika utumbo.

“Hiyo hewa inaporundikana inaleta mabadiliko katika utumbo mkubwa ikiwamo kuharibika utumbo wenyewe na hata kusababisha saratani,” anasema.

Anasema athari ya tatizo hilo, husababisha saratani inayoanza kama kidonda, mtu kuwa na mabadiliko madogomadogo hadi kuwa tatizo kubwa.

“Ushuzi ni hewa yenye sumu, ni lazima itoke, usipoitoa inajaa, hewa hiyo ni matokeo ya vitu mbalimbali kama chakula na bakteria,” anasema.

Anasema utaratibu wa watu kuamua kubana hewa ya ushuzi, sio wa asili kwani binadamu hakuumbwa hivyo.

“Kujamba ni sawa na mtu anayetaka kujisaidia haja kubwa halafu akajibana, nini kinatokea, ndivyo ilivyo kiafya mtu hatakiwi kujibana kutoa hewa hiyo,” anasema Dk Pazi.

Amesema kujamba ni jambo la kimaumbile na kibaiolojia, kwani hiyo hewa inatengenezwa na vyakula na baktreria, kiafya inashauriwa ukihisi fedheha kujamba eneo ulilopo, basi toka nenda kajambe kisha rudi.

Mtaalamu mwingine wa afya, Dk Ali Mzige, anasema si sahihi kubana ushuzi, kwani kufanya hivyo kunaweza kutengeneza madhara mengine kiafya.

“Usipojamba maana yake una matatizo, ukibanwa tafuta sehemu ya faragha uitoe hewa chafu,” amesema.

Amesema kujibana kujamba ni kuzuia gesi isitoke mwilini, hivyo unapofanya mara kwa mara kunaweza kuwa na athari kadhaa kwa afya.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Chrispin Kahesa, amesema maambukizi ya saratani yamegawanyika katika sababu mbalimbali, asilimia tano ni kurithi.

“Asilimia 65 ni visababishi vya saratani, ambavyo vingi ni moja ya kemikali kwenye pombe kali na tumbaku, lakini pia huusisha bakteria wale wanaohusisha vidonda vya tumbo, pia huchangia kupata saratani ya utumbo,” amesema.

Amesema watu ambao hawali mboga za majani na matunda wako kwenye hatari kubwa sambamba na wale ambao mfumo wao wa maisha hauzingatii afya bora.

“Pia michubuko ya muda mrefu sugu inaweza kusababisha saratani, ndiyo sababu pombe kali inahusishwa kwa kuwa inakwangua au kusugua utumbo.”