Dar es Salaam. Wakati mjadala wa Katiba mpya ukiendelea kushika kasi, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimezindua operesheni ya kuandika upya katiba yake, hatua inayokwenda sambamba na kuhamasisha uelewa wa umma kuhusu mabadiliko ya Katiba ya nchi.
Katika utekelezaji wa mkakati huo unaolenga chama kujijenga kisiasa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ametangaza kamati maalumu ya watu 11 kusimamia maboresho hayo ya ndani na kitaifa.
Akizungumza leo Jumanne, Machi 24, 2026 katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, Mwalimu amesema hatua hiyo inatekeleza maelekezo ya Kamati Kuu ya Agosti 4, 2025.
“Katiba ya chama cha siasa ndiyo nyenzo muhimu katika kufikia dira ya chama na katiba isiyo imara inaweza kudhoofisha matarajio ya kushika dola,” amesema.
Amesema kamati hiyo imezingatia uwakilishi mpana kutoka Bara na Zanzibar, vijana pamoja na wataalamu wa siasa na sheria, ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Benson Kigaila akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Zanzibar.
Wajumbe wengine ni Susan Kiwanga, Elia Bawa, Kangeta Ismail, Edward Kinabo, John Mrema, Esther Fulano na Ally Omari.
Amesema wanasheria wawili kutoka pande zote za Muungano wamejumuishwa kusaidia kuandaa rasimu itakayozingatia misingi ya kitaifa na kitaaluma.
Amesisitiza kuwa kamati hiyo pia itashuka kwa wananchi kukusanya maoni ili katiba hiyo iakisi uhalisia wa kisiasa na kijamii.
“Jiepusheni na masilahi binafsi. Katiba iwe kwa ajili ya wananchi tunaokwenda kuwatumikia,” amesema, akiongeza kuwa inapaswa kuweka misingi madhubuti ya kushughulikia migogoro ya ndani ya chama.
Amesema chama kinajiandaa kuanza ziara za kitaifa baada ya Pasaka, ikiwa ni sehemu ya operesheni ya kuhuisha chama, kuhamasisha mijadala ya katiba na kujenga ushawishi wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030.
“Hatutapimwa kwa maneno bali kwa matokeo,” amesema akijibu kuhusu ukimya wao baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wasomi wanatoa mitazamo tofauti kuhusu mkakati huo, wakitahadharisha juu ya taswira inayokikabili chama hicho mbele ya jamii.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema Chaumma ina mtihani mkubwa wa kujisafisha kutokana na mtazamo unaojengwa na jamii kuhusu namna vigogo wake walivyokihama chama chao cha zamani, Chadema, na kujiunga na Chaumma.
“Sioni kama kuandika katiba mpya na kufanya ziara kutakisaidia chama hicho, kwani tatizo linalokikabili si katiba bali ni namna walivyoondoka Chadema. Walipoteza imani ya wananchi wengi, hivyo kazi iliyopo ni katika kujenga imani ya wananchi,” amesema, akisisitiza kuwa changamoto ya uhalali wa kisiasa ni kubwa kuliko matatizo ya katiba pekee.
Tofauti na mtazamo huo, mwandishi na mchambuzi wa siasa Absalom Kibanda amekumbushia historia ya vyama vya siasa vilivyowahi kuibuka kuwa tishio kwa chama tawala, akitaja NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na ACT Wazalendo, ambavyo awali vilituhumiwa kuwa washirika wa CCM kabla ya kujijenga na kuwa vyama imara.
“Chaumma wanatuhumiwa kama chama kinachotumiwa na chama tawala, lakini vyama vyote vilipitia hali hiyo. CUF ilituhumiwa enzi za NCCR, baadaye ikaibuka chama kikuu cha upinzani. Nayo ikaanza kuituhumu Chadema kuwa kibaraka wa CCM hadi mwaka 2005 Mbowe alipowashangaza,” amesema.
Ameongeza namna viongozi waliokwenda kuipa nguvu Chaumma walivyotoka Chadema haitofautiani na waliounda ACT- Wazalendo, waliokumbana na tuhuma kama hizo lakini baadaye wakajijenga kisiasa na leo ni chama kikubwa.
“Hizo ni njia za kisiasa. Chaumma wakisimama imara, wakawekeza kwenye mikakati na kufuta dhana hiyo, wanaweza kuibuka kuwa chama kikubwa sana hapa nchini,” amesema.
Kwa mtazamo wake, uzoefu wa viongozi wa chama hicho, akiwemo Salum Mwalimu, ni rasilimali muhimu kwani wamepitia operesheni nyingi za kisiasa na hivyo si wa kubezwa.
