Mwanza. Jiji la Mwanza linatarajiwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria, yatakayofanyika Mei 21, 2026, yakihusisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kujadili usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire, maadhimisho hayo yatakuwa ya kila mwaka yakilenga kuimarisha mshikamano wa kikanda, kukuza uchumi wa buluu na kuongeza uelewa wa uhifadhi wa mazingira ya ziwa.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire.
“Ni jukwaa muhimu la kuhamasisha wananchi, wavuvi, vijana na wanawake kushiriki katika kulinda Ziwa Victoria na bonde lake,” amesema.
Amesema kuchaguliwa kwa Mwanza kunatokana na nafasi yake ya kimkakati katika uvuvi, biashara na utalii wa maji.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Maji ya Pamoja, Mustakabali wa Pamoja,” ikisisitiza wajibu wa pamoja wa nchi za kanda kulinda na kutumia rasilimali za ziwa kwa maendeleo endelevu.
Muonekanio wa Ziwa Victoria ambalo litafanyiwa maadhimisho ya kwanza jijini Mwanza yatakayofanyika Mei 21, 2026, yakihusisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kujadili usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.
Kuanzia Mei 17 hadi 21, kutakuwa na maonyesho ya ubunifu na teknolojia, kampeni za usafi wa mazingira, mashindano ya insha na sanaa pamoja na upandaji miti.
Pia kutafanyika kongamano la wadau Mei 18–19 litakalojadili changamoto za ziwa na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa katika kikao cha mawaziri Mei 21.
Muonekanio wa Ziwa Victoria ambalo litafanyiwa maadhimisho ya kwanza jijini Mwanza yatakayofanyika Mei 21, 2026, yakihusisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kujadili usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.
Katika hatua nyingine, LVBC itazindua Mfumo wa Taarifa za Maji (LVB-WIS) na Ripoti ya Hali ya Bonde (SoBR) zitakazosaidia kupanga na kusimamia rasilimali za maji kwa ushahidi.
Baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara wa Mwanza wamesema tukio hilo litaongeza uelewa wa uhifadhi wa ziwa na kufungua fursa za kiuchumi kupitia biashara na ubunifu.

