Arusha. Wahitimu wa Kidato cha sita waliofaulu kwa alama za juu zaidi mwaka 2025 walionufaika na programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI+ kusoma Shahada ya Kwanza kwenye masomo ya sayansi, ubunifu na akili unde wamehakikishiwa kupata elimu yenye kiwango kinachokubalika kimataifa na uhakika wa ajira kwenye kampuni zilizowekeza nchini Ireland.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Limerick anayehusika na masuala ya kimataifa, Profesa Colin Fitzpatrick amesema hayo leo Jumanne, Machi 24,2026 wakati wa ziara ya ugeni kutoka nchini Ireland uliofika katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kukamilisha maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao.
Serikali kupitia programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI ilitoa ufadhili kwa wanafunzi waliopata alama za juu kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2025 kusoma kwenye vyuo bora nje ya na kuchaguliwa katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini na Limerick nchini Ireland.
“Nimefurahi kukutana na wanafunzi wenye vipaji waliofaulu kwa alama za juu kwenye mitihani yao ,tunataka chuo chetu kuendelea kuwa kivutio cha wanafunzi mahiri kutoka ulimwenguni kote, muda wote watakaokuwa Ireland watapata uzoefu wa kimataifa kwa kufanya mafunzo kwa vitendo na kupata ajira kwenye kampuni kubwa tunazoshirikiana nazo.”amesema Profesa Fitzpatrick
Amesema ameridhishwa na maandalizi waliyopewa ya kuwaandaa kimaadili na kitaaluma yatakayowapa fursa ya kuchangamana na wanafunzi wengine wanaotoka mataifa mbalimbali wakiwemo wenyeji.
Profesa Fitspatrick amesema ndoto ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Limerick ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa jambo ambalo limeendelea kuvutia wanafunzi wengi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya, na kufunguliwa kampuni nyingi ambazo wameingia nazo makubaliano ya mafunzo kwa vitendo.
Naibu Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Anthony Mshandete amesema taasisi hiyo itanufaika kwa kupata uzoefu mkubwa walionao Chuo Kikuu cha Limerick kwenye kuzifanyia biashara tafiti mbalimbali zinazozalishwa na wanafunzi.
Mratibu wa Programu hiyo kutoka NM-AIST,Profesa Lillian Passape kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) amesema waliweka kituo cha maandalizi katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi 50, ambao kati yao 18 wameshaenda nchini Afrika Kusini na 32 wanatarajiwa kwenda Ireland hivi karibuni.
Baadhi ya wanafunzi wanaonufaika na ufadhili wa masomo hayo, Anitha Sosthenes na Emmanuel Said wameishukuru Serikali kuwapa ufadhili huo ambao wanaamini utawapa elimu inayostahili na kuwafungulia milango ya ajira kwenye viwanda na kampuni kubwa.