Dar es Salaam. Tanzania imeingia makubaliano ya uwekezaji wa Dola za Marekani 300 milioni (takribani Sh700 bilioni) na Panda Hill Tanzania Limited, hatua inayotarajiwa kuibadilisha Mbeya kuwa kitovu kipya cha biashara na viwanda.
Aidha, kwa mkataba huo, imefungua ukurasa mpya wa uchumi unaolenga kuongeza thamani ya madini na kuimarisha nafasi ya nchi katika masoko ya kimataifa, ikiwemo Marekani.
Makubaliano hayo yanahusu uendelezaji wa mradi wa niobium wa Panda Hill, ambao ni miongoni mwa maeneo machache duniani yenye madini hayo.
Niobium hutumika kuimarisha chuma na kutengeneza aloi zenye uwezo mkubwa zinazohitajika katika sekta za miundombinu mikubwa, nishati, magari na anga.
Maofisa wa Serikali wanasema mradi huo unaashiria mabadiliko kutoka kusafirisha madini ghafi kwenda kuzalisha bidhaa zenye thamani zaidi zinazotumika katika viwanda vya kisasa, hatua inayotazamwa kuwa muhimu katika mageuzi ya muda mrefu ya uchumi wa Tanzania pamoja na kukuza mauzo ya nje.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi huo unaakisi mwelekeo wa sera ya Serikali kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi kiuchumi na rasilimali zake kupitia uchakataji wa ndani, ushiriki wa Serikali na uhusiano imara na maendeleo ya viwanda.
Amesema Serikali inalenga miradi ya madini ichangie zaidi katika ukuaji wa viwanda, ajira na mapato ya fedha za kigeni, badala ya kubaki kwenye uchimbaji pekee.
“Tunataka madini yetu yachangie moja kwa moja katika maendeleo ya taifa kupitia uongezaji thamani, umiliki na shughuli za kiuchumi za ndani,” amesema Mavunde, akihusisha mradi huo na ajenda ya maendeleo ya muda mrefu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa soko la dunia la niobium linadhibitiwa na wazalishaji wachache, jambo linaloufanya mradi wa Panda Hill kuwa wa kimkakati.
Kwa mujibu wa Serikali, Brazil huzalisha takribani asilimia 80 ya niobium duniani, mzalishaji mwingine nchini humo huchangia asilimia 11 huku Canada ikizalisha karibu asilimia 6. Kupitia mradi wa Panda Hill, Tanzania inatarajiwa kuwa mzalishaji wa nne muhimu duniani kwa kuchangia takribani asilimia 4 ya mahitaji ya soko, ikiwa na uzalishaji uliopangwa wa karibu tani 100,000 kwa mwaka.
Maofisa wamesema mradi huo una umuhimu mkubwa pia katika biashara kwa kuwa unajumuisha uchakataji na kuyeyusha madini hapo hapo mgodini, ili kuzalisha ferroniobium, bidhaa yenye thamani ya juu inayotumiwa na wazalishaji wa chuma na viwanda mbalimbali.
Mfumo huo wa uongezaji thamani unatarajiwa kuiwezesha Tanzania kuuza bidhaa zilizochakatwa katika masoko yenye thamani kubwa, ikiwemo Marekani, badala ya kusafirisha madini ghafi.
Meneja Mkuu wa Panda Hill Tanzania Limited, Dennis Cook amesema makubaliano hayo mapya yanatoa fursa ya kuendeleza mradi huo baada ya kuchelewa kwa miaka kadhaa kufuatia mabadiliko ya sheria za madini mwaka 2017.
Amesema kampuni sasa itawasilisha maombi ya leseni maalumu ya uchimbaji madini pamoja na kuhuisha mipango ya kiufundi na kifedha kabla ya kuanza kwa ujenzi.
Uwekezaji huo unahusisha ujenzi wa mgodi, kiwanda cha uchakataji pamoja na mtambo wa kuyeyusha ferroniobium. Mtambo huo unatajwa kuwa muhimu kwa sababu ni michache duniani.
Taarifa za kampuni zinaonyesha kuwa kwa sasa kuna mitambo mitatu tu ya aina hiyo duniani — miwili Brazil na mmoja Canada, hali inayomaanisha kuwa kituo cha Mbeya kitakuwa cha kwanza barani Afrika.
Maofisa wanasema athari za kiuchumi kwa jamii ni moja ya sababu kuu zinazoufanya mradi huo kuwa muhimu.
Kampuni inakadiria kuwa takribani asilimia 70 ya bidhaa na huduma wakati wa uzalishaji zitatoka ndani ya nchi, huku thamani ya manunuzi ya ndani katika maisha ya mradi ikitarajiwa kufikia dola 1.77 bilioni.
Matumizi ya ndani kwa mwaka yanatarajiwa kuzidi dola 60 milioni, yakifungua fursa kwa kampuni za Kitanzania katika sekta za usafiri, ujenzi, matengenezo, ulinzi, upishi na huduma nyingine.
Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 1,600 wakati wa ujenzi na takribani nafasi 600 za kudumu baada ya kuanza uzalishaji, pamoja na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja kupitia minyororo ya usambazaji.
Mgodi huo utajengwa katika eneo linalotumiwa kwa sasa na shamba la Gereza la Songwe. Mavunde amesema makubaliano hayo yanajumuisha mpango wa kujenga gereza jipya la kisasa kuchukua nafasi ya miundombinu iliyopo katika eneo la mradi.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema Serikali itakuwa na asilimia 16 ya hisa kwa niaba ya wananchi kupitia ofisi yake chini ya mfumo wa ushiriki wa rasilimali asilia, unaoruhusu umiliki wa Serikali bila kuchangia mtaji wa awali.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, kwa niaba ya Serikali, yakirasimisha mfumo wa uwekezaji pamoja na umiliki wa Tanzania katika mradi huo.
Kwa ujumla, maofisa wanasema mradi wa Panda Hill unalenga kuonyesha mfano mpya wa sekta ya madini nchini, ambapo miradi ya rasilimali inatarajiwa kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika minyororo ya ugavi wa kimataifa.
