Geita. Kesi mbili zinazowakabili wabunge wawili wa majimbo ya Chato na baadhi ya madiwani, zimeahirishwa baada ya watuhumiwa kushindwa kufika mahakamani kwa sababu mbalimbali.
Kesi hizo zinazowahusu Mbunge wa Chato Kusini, Paschal Lutandula na Mbunge wa Chato Kaskazini, Cornel Magembe pamoja na madiwani wanne akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Bathoromeo Manunga, zilizokuwa zitajwe kwa mara ya pili leo Jumanne, Machi 24, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Geita.
Katika kesi ya kwanza inayosimamiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Gosper Luoga washtakiwa ni Lutandula, Manunga (diwani wa Kata ya Bwongera) pamoja na Josephat Manyenye.
Kesi ya pili inawahusu Magembe pamoja na Frank Leonard Francis, chini ya usimamizi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cleofas Waane.
Akizungumza na Mwananchi leo, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita, Ruth Ndeto amesema kesi zote zimeshindwa kuendelea kutokana na kutokuwepo kwa watuhumiwa mahakamani.
Amesema katika kesi ya kwanza, Lutandula ameshindwa kufika mahakamani kutokana na changamoto ya usafiri alipokuwa akitokea Dodoma.
Kwa upande wa kesi ya pili, Ndeto amesema mshtakiwa Frank Leonard ameugua ghafla akiwa mahakamani, hali iliyosababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 24, 2026.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na tuhuma za kufanya miamala ya fedha inayodaiwa ni rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b) na (2) kikisomwa pamoja na kifungu cha 46A cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Toleo lililofanyiwa marejeo la mwaka 2023, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 11 ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka katika kesi ya kwanza, inadaiwa kuwa Novemba 29 na Desemba 1, 2025, Lutandula alitoa rushwa ya Sh5,515,000 kwa Njile Charles Mboligo ili ajiondoe katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika shitaka lingine, Lutandula anadaiwa kutoa Sh505,000 kwa Mange Samwel ili kumpigia kura Manunga katika nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo kupitia CCM. Pia, anadaiwa kutoa Sh1,530,000 kwa Faustin Mbasa kwa lengo hilohilo la kumchagua Manunga kupitia vikao vya chama.
Katika kesi ya pili, Magembe anadaiwa kushirikiana na Frank Leonard kutoa rushwa kwa madiwani ili kushawishi mchakato wa uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Inadaiwa kuwa kati ya Novemba 28 na 30, 2025, Magembe akiwa katika Hoteli ya Lakezone, Nyamuhongolo jijini Mwanza, aliwapatia chakula, vinywaji na malazi madiwani 20 kutoka Chato vyenye thamani ya Sh1,332,000 ili wampigie kura Frank Leonard apitishwe na Kamati Kuu ya CCM kuwania nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri.
Aidha, inadaiwa kuwa katika kipindi hicho, madiwani 18 walipewa Sh100,000 kila mmoja ili kumuunga mkono Frank Leonard katika mchakato wa uteuzi wa chama.
Pia, Novemba 29, 2025, Magembe anadaiwa kutoa Sh500,000 kwa madiwani 16 kwa lengo la kuhakikisha Frank Leonard anachaguliwa katika hatua za awali za kinyang’anyiro hicho.
Katika tukio jingine, Novemba 30, 2025, Magembe anadaiwa kuwa katika Hoteli ya Serengeti Palace, Katoro mkoani Geita, aliwapatia chakula na vinywaji madiwani 20 vyenye thamani ya Sh884,000 ili wamuunge mkono Njile Charles Mboligo, aliyekuwa amepitishwa na Kamati Kuu ya CCM kuwania nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.