BAADA ya kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya dunia ya Kabaddi Wanawake, timu ya taifa ya Zanzibar imesema inajipanga upya ili wakati ujao ifike mbali zaidi.
Hayo yamesemwa na Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Mchezo wa Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, alipozungumza na Mwanaspoti, huku akibainisha, kukosa uzoefu ndiyo sababu ya kushindwa kufanikiwa kwao.
Amesema timu hiyo ilizoea kucheza Afrika pekee na sio nje ya hapo, hivyo kutokana na uchanga wake iliishia hatua ya makundi, lakini sasa viongozi wanajipanga na kurekebisha makosa ili ikipata nafasi nyingine waonyeshe ubora wao.
“Mchezo wetu bado mchanga, pia hatuna uwanja na vifaa, hivyo timu ilikosa maandalizi mazuri ingawa tuliiwakilisha nchi.
“Katika mashindano hayo hatukuonesha kiwango kikubwa, lakini tulifanikiwa kushiriki vizuri na tunashkuru kupata nafasi hiyo,” amesema.
Amesema ushiriki wao huo kwa mara ya kwanza wamejifunza vitu vingi ikiwemo miundombinu ya michezo na hamasa kutoka serikalini namna inavyosaidia kwenye mchezo huo.
Zanzibar ilishiriki Kombe la Dunia la Kabaddi kwa Wanawake Novemba 2025, michuano iliyofanyika Bangladesh ambapo timu 11 zilishiriki ambazo ni wenyeji Bangladesh, India, Thailand, Kenya, Uganda, Chinese Taipei, Ujerumani, Nepal, Iran, Poland, Zanzibar na India iliyotwaa ubingwa kwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Chinese Taipei katika mchezo wa fainali.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo amesema mchezo huo una miaka minne tangu kuanzishwa kwake visiwani hapa na kwa sasa zipo klabu sita ambazo ni KMKM, JKU, Nyuki, VTA, Bububu na Fighter.
