Nyuma ya pazia dili la Mpanzu Simba

“NINA mipango naye.” Ni kauli aliyoitoa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker juu ya kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Elie Mpanzu ambaye jana klabu hiyo ilitangaza kumuongezea mkataba wa miaka miwili na kuzima kabisa tetesi zilizokuwa zimezagaa kuhusu mwisho wa msimu huenda angeondoka baada ya mkataba wake kumaliuzika.

Simba imetekeleza maagizo ya Barker ambaye anaonekana kujilipua katika kumbakisha nyota huyo raia wa DR Congo anayeamini bado ana uwezo wa kuibeba Simba licha ya hapo kati kiwango chake kilizua mashaka baada ya ujio wa mastaa wapya kipindi cha dirisha dogo akiwamo Anicet Oura, Libase Gueye na Ino Loemba.

Hatua hiyo inamfanya nyota huyo kuendelea kuitumikia Simba hadi Desemba 2028, ikiwa ni nyongeza ya mkataba wake wa awali uliokuwa ukielekea ukingoni.

Kwa muda mrefu, Mpanzu alikuwa akihusishwa kuondoka Msimbazi kutokana na mkataba wake kuwa ukiongoni, hali iliyozua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo.

Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo chini ya mwekezaji Mohamed Dewji, umeingilia kati na kuhakikisha unaimarisha kikosi hicho kwa kumbakiza mchezaji huyo.

Pamoja na kusaini mkataba huo mpya, bado kumekuwa na mjadala kuhusu nafasi yake kikosini kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kufuatia kusajiliwa kwa Libasse Guaye na Anicet Alain Oura katika dirisha dogo la Januari 2026.

Katika mechi za karibuni, Mpanzu amekuwa akianzia benchi kufuatia ujio wa wachezaji hao waliobadilisha muundo wa kikosi cha kwanza.

Licha ya hali hiyo, Mpanzu ameendelea kuonyesha thamani yake, hasa baada ya kufunga bao muhimu lililoipa Simba ushindi dhidi ya Singida Black Stars na kutoa asisti katika mechi mbili mfululizo zilizofuata dhidi ya Pamba Jiji kwenye sare ya 1-1 na TRA United, Mnyama akishinda 3-0.

Katika mahojiano na Mwanaspoti ambayo yalifanyika mjini Singida, Barker aliweka wazi kuwa hali ya Mpanzu kutokuwa na nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza sio ishara ya kushuka kwa kiwango chake.

Kwa mujibu wa Barker, ushindani uliopo ndani ya kikosi hicho ni mkubwa na maamuzi ya nani aanze hutegemea mahitaji ya kiufundi ya kila mchezo.

“Mpanzu ni sehemu ya kikosi chetu na kila mchezaji aliyepo Simba ni muhimu. Nina mipango naye,” amesema Barker, akionyesha imani yake kwa mshambuliaji huyo.

Kauli hiyo ilionyesha wazi kuwa kocha huyo bado ana mipango na Mpanzu na ndio maana mabosi wa timu hiyo wakiongozwa na Mo Dewji walifanya uamuzi wa haraka kabla ya kumpoteza Mkongomani huyo ambaye kwa sasa anaonekana kurejea kwenye makali yake kama ilivyokuwa chini ya Fadlu Davids.

Mpanzu aliyetua Simba Oktoba 2024 akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, huu ni msimu wake wa pili kikosini hapo.

Mkongomani huyo amekuwa mchezaji wa tatu hivi karibuni kuongezwa mkataba wa kuendelea kuitumikia Simba baada ya Yusuph Kagoma na Rushine De Reuck.