MABOSI wa Yanga wameshafanya uamuzi unaomuweka katika wakati mgumu kocha mkuu wa kikosi hicho, Pedro Goncalves, ikielezwa hivi sasa anahesabu siku ndani ya klabu hiyo.
Kuanzia leo Machi 24, 2026 hadi Aprili 2, 2026, kuna takribani siku tisa zimebaki katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Bara imesimama kupisha Kalenda ya Fifa na ndiyo muda ambao Yanga inapambana kuhakikisha inampata mbadala wa Pedro, kisha kuachana na Mreno huyo.
Uamuzi huo wa mabosi wa Yanga umefanyika baada ya kukaa kikao cha dharula kujadili mwenendo wa timu hiyo lakini hapohapo wakataka kupata ripoti kutoka kwa Pedro.
Baada ya kupata ripoti, jana mchana, viongozi wa Yanga wakiongozwa na rais wa klabu hiyo, Hersi Said walikutana na benchi la ufundi na kufanya kikao cha tathmini ya kikosi hicho baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Katika kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam, Pedro Goncalves aliongozana na kocha msaidizi, Matthew Silva na kocha wa makipa, Fernando Pereira.
Kwa upande wa viongozi, mbali na Hersi pia alikuwepo Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Rodgers Gumbo na Munir Said.
Hatua hiyo imekuja baada ya mabosi hao kuona kila siku zinavyozidi kwenda kikosi chao kinazidi kushuka kiwango huku kilichowashtua zaidi ni sare tatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam (0-0), TRA United (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1) licha ya kwamba bado Yanga inaongoza msimamo wa ligi huku ikiwa haijapoteza mechi yoyote kati ya 16 ilizocheza ikishinda 11 na sare tano, ikikusanya pointi 38.
“Katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama, kuna mchakato unafanyika wa mabadiliko ya benchi la ufundi, tunataka kuleta kocha mpya kisha kuachana na Pedro baada ya viongozi kukubaliana hilo lifanyike ili kuiweka timu katika mwendo tunaoutaka wa kufanya vizuri na kutetea ubingwa wetu,” kilisema chanzo na kuongeza.
“Ukiangalia kwa siku za karibuni timu haifanyi vizuri, licha ya kwamba kuna changamoto za mejeruhi, lakini hata mbinu za kocha hazifurahishi, kwa hiyo viongozi wamekubaliana tupate kocha kwanza, ndiyo tuachane na huyu.”
Aidha, inaelezwa kwamba, sio Pedro peke yake ambaye yupo kwenye hesabu hizo, kwani hata kocha wa mazoezi ya viungo, Chyna Mokaila, anaonekana kazi yake haijakubalika ndani ya kikosi hicho.
Taarifa zingine zinabainisha kwamba, wasaidizi wa Pedro wametajwa kuwa chanzo cha timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwani hawana ushirikiano mzuri na bosi huyo wa benchi la ufundi, hivyo pia kuna uwezekano yakafanyika maboresho makubwa kwa kulifumua benchi zima.
Siku chache kabla ya kukutana kwa mabosi wa Yanga na kufanya kikao cha kumjadili Pedro, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, alilithibitishia Mwanaspoti kwamba uongozi wa timu hiyo umemtaka Pedro kuwapa ripoti ya haraka kwenye mechi ambazo ameiongoza tangu akabidhiwe kikosi Oktoba 25, 2025.
Ndani ya mechi 16 ambazo Yanga imecheza msimu huu kwenye ligi, Pedro amehusika kwenye mechi 13 ambapo ameshinda tisa na sare nne zikiwemo tatu mfululizo za hivi karibuni. Hajapoteza.
Yanga bado inaongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na jumla ya pointi 38, baada ya kucheza mechi 16 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 31 katika mechi 14. Ya tatu ni Azam iliyokusanya pointi 29 ikicheza mechi 15.
