Winnie Odinga: Binti wa Raila anayegeuka turufu kwa makundi ODM

Alipojitokeza katika mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na Katibu Mkuu wa ODM anayepingwa vikali, Edwin Sifuna, katika Hoteli ya Panafric jijini Nairobi mwezi uliopita, Winnie Odinga siyo tu alihudhuria mkutano huo, alitikisa kwa nguvu muundo dhaifu wa mamlaka ndani ya chama hicho.

Mkutano huo uliofanyika kufuatia kuondolewa kwa utata kwa Sifuna, tayari ulikuwa umevutia macho na masikio ya wengi.

Lakini uwepo wa Winnie, licha ya kutosema neno lolote, uliubadilika kutoka mkusanyiko wa upande mmoja wa kisiasa hadi kuwa tukio lenye uzito mkubwa wa kisiasa.

Ndani ya uongozi wa juu wa ODM na serikali pana ya Rais William Ruto, vyanzo vya ndani vinasema kengele za tahadhari zilianza kulia karibu mara moja.

“Uwepo wake ulibadilisha kabisa mtazamo wa tukio lile,” alisema kiongozi mmoja mwandamizi wa chama anayefahamu mijadala ya ndani. “Haikuwa tena kambi ya Sifuna pekee inayozungumza kulikuwa na jina la Odinga ndani yake, hatukuweza kulipuuzia.”

Mara nyingi akielezwa na watu wa ndani kama mrithi wa kisiasa wa Raila Odinga, vyanzo vinasema Winnie ana uzito wa kisiasa unaozidi kwa mbali nafasi yake ya sasa kama mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Hatua zake za kisiasa zinafuatiliwa kwa karibu, si tu kwa maana yake ya sasa, bali pia kwa ishara zinazotoa kuhusu mustakabali wa ODM.

Kujitokeza kwake kwa muda mfupi lakini kwa mpangilio maalumu katika hoteli ya Panafric, kwa mujibu wa vyanzo, kulitikisa mhimili pinzani unaohusishwa na baba yake mkubwa, Dk Oburu Oginga, na kuchochea juhudi za kimya lakini za makusudi za kumvuta karibu zaidi au angalau kumzuia asijitenge zaidi.

Kilichofuatia, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya ndani, ni mkakati uliopangwa kwa ustadi wa kumvutia kisiasa, unaochanganya mawasiliano ya kifamilia na ishara za kitamaduni.

“Mawazo ni rahisi,” kilisema chanzo kimoja kutoka kambi ya Oburu. “Haumpingi Winnie. Unamchukua. Unamfanya ajisikie sehemu ya kitovu cha uamuzi.”

Akiwa karibu zaidi na Raila, hata akifuatana naye katika safari yake ya mwisho nje ya nchi Oktoba 2025, uhusiano wake na kambi ya “Linda Mwananchi” ulikuwa na uzito na ishara kubwa zilizowakera waliokuwa madarakani.

Ni uaminifu huo uliowapa hofu viongozi wa ODM na vigogo wa Kenya Kwanza.

Kwa washauri wa Rais William Ruto, hofu ilikuwa kwamba kundi la wafuasi wa Raila waliodhani Winnie alitendewa vibaya hadi “kuhama upande” linaweza kupiga kura dhidi ya muungano, hasa katika uchaguzi wa urais wa mwaka ujao.

Kinyume chake, kuondoka kwake kutoka kundi la “Linda Mwananchi” kungeudhoofisha upinzani, na kuwalazimu kubadili mkakati wao.

Haya yanajiri wakati ukoo mkubwa wa Kawuor ulitarajiwa kukutana Kang’o ka Jaramogi, Jumapili iliyopita, Machi 22, katika mkutano muhimu uliowaleta pamoja familia ya Odinga na jamaa wengine.

Ingawa hadharani tukio hilo linaelezwa kama sherehe ya kiutamaduni ya kumbariki na kumtawaza kiongozi mpya wa jamii, vyanzo vinasema pia, ni fursa muhimu ya kupanga upya safu za ndani ikiwemo nafasi ya Winnie.

“Hili si suala la utamaduni tu,” alisema mwanaukoo mmoja kwa siri. “Ni nani yuko upande gani, nani anaonekana na nani, na hilo lina maana gani mbele ya safari.”

Inadaiwa kuwa kundi linalomuunga mkono Oburu lina nia ya kuhakikisha Winnie anahudhuria na kuonekana wazi kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kuonesha kwa hila umoja wa kifamilia na wa chama.

Mdogo wake Dk Oginga, Ruth Odinga, alithibitisha mkutano huo, akisema utawaleta pamoja wanafamilia na wanaukoo kumtawaza kiongozi mpya wa ODM kama kiongozi wa jamii na mrithi wa kisiasa.

“Ni mkutano wa ukoo wa Kawuor kumtawaza kama kiongozi wa jamii na kumpokea rasmi kama kiongozi mpya wa ODM baada ya kifo cha Raila,” alisema, akisisitiza uzito wa tukio hilo.

Tofauti na mikutano ya kawaida ya kisiasa, tukio hilo litabaki na misingi yake ya kitamaduni, likiwa sehemu ya mpango mpana wa kuunganisha familia, likifuatia mkutano wa wajumbe wa ODM tawi la Nairobi uliopendekeza Winnie kupandishwa hadhi.

“Litafanyika Kang’o ka Jaramogi. Ni zaidi tukio la ukoo, ingawa wageni wengine wanatarajiwa,” alisema Ruth, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisumu.

Eneo hilo lina ishara kubwa, likiwa makazi ya asili ya Jaramogi Oginga Odinga na kitovu cha kiroho na kisiasa cha familia ya Odinga hali inayolifanya tukio hilo kuwa zaidi ya mkusanyiko wa kawaida.

“Ni muhimu pia kwetu kwa sababu hii ni sherehe ya kwanza hapo tangu Raila afariki. Lina uzito mkubwa,” aliongeza Ruth, akionyesha mchanganyiko wa huzuni na azma.

Mbali na mila, tukio hilo linatarajiwa kubeba ujumbe mzito wa kisiasa wakati ODM ikijipanga upya bila kiongozi wake wa muda mrefu.

“Anatarajiwa kupata baraka za jamii katika juhudi zake,” alisema, akionesha umuhimu wa uungwaji mkono wa ukoo katika kujenga uhalali kisiasa.

Wakati wazee wakikusanyika, mila zikifuatwa na baraka kutolewa, tukio hilo linatarajiwa kuashiria si tu mwisho wa enzi, bali mwanzo wa enzi mpya kwa njia ya ishara.

Huku mvutano wa makundi ndani ya chama ukiongezeka, vyanzo vinasema kuna juhudi za kimya lakini makini za washirika wa Dk Oginga kumvuta Winnie upande wao ama kama mshirika au angalau kama nguvu isiyoegemea upande wowote.

Nafasi yake imekuwa nyeti na yenye athari kubwa katika mabadiliko ya ODM baada ya Raila.

“Winnie anawakilisha mwendelezo, lakini pia mustakabali,” alisema kiongozi mmoja mwandamizi wa chama. “Atakaposimama au kutoegemea upande wowote, hilo litaathiri namna wafuasi wanavyochukulia mabadiliko haya.”

Mjadala kuhusu nafasi yake umeongezeka hivi karibuni, hasa baada ya tawi la ODM Nairobi kupendekeza apewe nafasi katika chombo cha juu cha uamuzi cha chama hatua iliyotafsiriwa kama jaribio la kuhalalisha ushawishi wake.

“ODM ni nyumbani, ni nyumba ambayo baba yangu aliijenga. Mnatarajia kweli niondoke? Niende wapi?” alihoji Winnie katika mkutano ulioongozwa na mwenyekiti wa ODM Nairobi, George Aladwa.

Aladwa alisema wajumbe walipendekeza kupandishwa kwake hadhi kutokana na kujitolea kwake.

“Huku tukizungumza naye, tulieleza wasiwasi kuhusu kuonekana kuwa karibu na kambi ya Sifuna na tukamtaka abaki imara ndani ya mkondo mkuu wa chama. Alituhakikishia atashirikiana nasi, ndipo tukapendekeza awe naibu kiongozi wa chama,” alisema.

Hata hivyo, pendekezo hilo limekwama kwa sasa.

Mwenyekiti wa ODM, Gladys Wanga, alisema anafurahia kuona Winnie anatambua ODM ni nyumbani kwake.

Lakini yeye pamoja na mkurugenzi wa uchaguzi, Junet Mohamed walithibitisha kuwa suala hilo halitakuwa katika ajenda ya Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe (SNDC).

“Hakutakuwa kwenye ajenda; litasubiri mkutano wa kawaida wa NDC,” alisema Mohamed, akiahirisha uwezekano wa Winnie kuingia rasmi katika uongozi wa juu wa chama.

Hata hivyo, licha ya njia rasmi kukwama, jitihada za kisiasa zinaendelea kimya kimya.

Vyanzo vinasema mkakati wa kambi ya Oburu si kumharakisha, bali kumjenga polepole ndani ya muungano mpana unaochanganya uhalali wa kifamilia, uungwaji mkono wa ukoo na nguvu ya wanachama wa chini.

“Lengo si kumkimbiza,” alisema mdau mmoja. “Ni kumfanya awe huru na tayari, ili wakati ukifika awe tayari ndani ya mfumo unaodumisha utulivu wa chama.”

Washirika wa Sifuna wameonya wazi dhidi ya juhudi wanazosema ni za “kumtumia” Winnie kuhalalisha uamuzi wenye utata.

“Namtaka awe makini sana, kwani kuna wanaotaka kumtumia kuhalalisha uamuzi utakaofanyika Machi 27 bila ushindani wa haki,” alisema naibu kiongozi wa ODM, Godfrey Osotsi.

“Winnie hahitaji hilo, ana uwezo wa kushinda nafasi yoyote kirahisi,” aliongeza, akisisitiza uwezo wake wa kujijenga kisiasa bila kutegemea mipango ya ndani ya chama.

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino alitoa kauli zinazofanana, akimtaka Winnie kubaki thabiti katika misingi ya chama hicho.

“Asisahau itikadi za ODM. Anapaswa kusimama imara,” alisema, kauli inayodhihirisha mvutano wa kiitikadi unaoendelea ndani ya chama.

Ujumbe huo unaokinzana, mmoja wa kumvutia kwa upole na mwingine wa kumtaka awe makini na kuweka umbali unaonesha njia nyembamba anayopaswa kuipita Winnie katika kusaka mwelekeo wake ndani ya siasa zinazobadilika.

Hali yake inazidi kuwa tata kutokana na mvutano wa hivi karibuni ndani ya familia pana.

Januari, ukoo wa Kawuor uliwakosoa hadharani Winnie na ndugu yake, Raila Junior, kwa kile kilichoonekana kama kutomheshimu baba yao mkubwa, Oburu Oginga, tukio nadra lililofichua tofauti za kizazi na kimkakati ndani ya familia ya Odinga.

Mzozo huo uliibua wito wa uvumilivu na umoja, huku wazee wakikitaka kizazi kipya kuzingatia zaidi misingi na taratibu zilizopo. Wachambuzi wa siasa wanasema tukio hilo linaweza kuwa limeimarisha azma ya kambi ya Oburu kumhusisha moja kwa moja Winnie si tu kurekebisha mpasuko wa ndani, bali pia kuhakikisha familia inaonekana kuwa na msimamo mmoja katika kipindi hiki muhimu cha mpito.

Kwa upande wa kambi ya Oburu, kupata hata uungwaji mkono wa kimya kutoka kwa Winnie au angalau kumzuia asiungane na makundi pinzani ni ushindi.

Kwa upande wa kundi linaloongozwa na Sifuna na washirika wake, kuhakikisha Winnie anabaki huru au angalau hamegwi na kambi ya Oburu ni jambo lenye uzito sawa.

Akiwa katikati ya mvutano huu wa maslahi, Winnie hadi sasa ameendelea kuwa kimya kwa tahadhari katika siku za hivi karibuni, akiepuka kutoa kauli za wazi ambazo zinaweza kubadili mwelekeo wa mizani ya kisiasa upande wowote.