Bagamoyo. Changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu katika Kata ya Fukayosi, iliyobainishwa na uchunguzi wa Mwananchi, imeanza kupatiwa ufumbuzi kupitia hatua mbalimbali zinazochukuliwa.
Uchunguzi wa Mwananchi katika baadhi ya vijiji vya Kata ya Fukayosi, ikiwemo Mkenge, Kidomole na Mwavi, katika Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani, ulibaini kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari hutumia zaidi ya saa moja wakitembea kwenda shule.
Katika kata hiyo, ambayo ina shule ya sekondari moja, baadhi ya wanafunzi hutembea kwa takribani kilometa saba hadi 15 kwenda shule na kurudi nyumbani.
Hii ni kinyume na Mkakati wa Ujenzi na Matengenezo ya Shule (SCMS) wa mwaka 2019, ambao umeainisha kuwa mtoto anayesoma elimu ya awali hatakiwi kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 1.5, unaokadiriwa kuchukua takribani dakika 25.
Pia, kwa upande wa shule ya msingi, mwanafunzi hatakiwi kutembea zaidi ya kilometa tatu, zinazokadiriwa kuchukua dakika 40, huku mwanafunzi wa sekondari akikadiriwa kutembea umbali usiozidi kilometa tano kwenda shule na kurudi nyumbani, jambo linalokadiriwa kutumia chini ya saa moja.
Aidha, Sura ya 3.8 ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, imeweka wazi wajibu wa Serikali, kwa kushirikiana na wadau, kuhakikisha inajenga mazingira salama na rafiki katika upatikanaji wa elimu na mafunzo.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkenge katika Kijiji cha Mkenge, inayojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na halmashauri pamoja na wadau wa maendeleo.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkenge, Saidi Bwanga amesema ujenzi wa shule hiyo umeanza, jambo linaloleta matumaini kwa wananchi kumalizika kwa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu katika kijiji hicho.
“Ujenzi unaenda kwa kasi. Hadi sasa tumeshajenga msingi wa madarasa matatu, na tunatarajia hadi mwisho wa mwaka huu tayari ujenzi utakuwa umekamilika,” amesema.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutasaidia kuongeza idadi ya sekondari katika kata hiyo, pamoja na kuwawezesha wanafunzi wanaofaulu kutoka Shule ya Msingi Mkenge kusoma sekondari iliyopo jirani na makazi yao.
“Nawaomba wadau wa maendeleo na Serikali watusaidie ili ujenzi wa madarasa ukamilike kwa haraka, ikiwezekana, yajengwe pia mabweni. Hili siyo tu litanufaisha Kijiji cha Mkenge bali kata nzima ya Fukayosi kwa kuongeza shule nyingine ya sekondari,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, Shauri Selenda, amesema kwa upande wa Fukayosi, moja ya sababu inayochangia uwepo wa changamoto hiyo ya wanafunzi kutembea umbali mrefu ni asili ya jamii ambayo ni wakulima na wafugaji.
“Kama unavyojua, wakulima na wafugaji siyo watu wanaopendelea kuishi eneo moja, hivyo makazi yao yametawanyika,” amesema.
Hata hivyo, amesema licha ya changamoto hiyo, Serikali kwa kushirikiana na halmashauri hiyo wanaendelea kuhakikisha wanasogeza shule angalau kuwa karibu na wananchi walio wengi.
“Hadi sasa tumefanikiwa kujenga shule mbili shikizi za msingi katika kata hiyo. Pia, katika Kijiji cha Mkenge kuna shule ya sekondari inajengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na halmashauri,” amesema Selenda.
Amesema Serikali, kupitia halmashauri hiyo, inaendelea kujenga shule shikizi katika maeneo mengine yenye wakazi walioko mbali na shule mama na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Mbunge wa Bagamoyo (CCM), Subira Mgalu, amesema katika Kata ya Fukayosi kuna shule ya sekondari, na katika Kijiji cha Mkenge sekondari nyingine imeanza kujengwa.
“Hii nchi ni kubwa na kila wilaya ina ukubwa wake. Shule zinajengwa, lakini baadaye yanatokea mahitaji zaidi. Mfano, Mkenge ni kijiji, na nchi bado haijafikia kujenga shule katika kila kijiji.
“Lakini katika kata ambazo tumebaini uhitaji wa shule za sekondari zaidi, tumeendelea kuongeza. Mfano, katika Kata ya Mapinga kuna zaidi ya shule tatu za sekondari,” amesema Subira.
Ameongeza kuwa wameendelea kujenga shule shikizi katika maeneo mbalimbali yaliyo mbali na shule mama.
Akizungumza na Mwananchi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa, amesema Serikali imefanya jitihada kuhakikisha kila kata katika maeneo yote nchini inakuwa na shule ya sekondari.
Hata hivyo, amesema baadhi ya halmashauri zina maeneo makubwa ya kiutawala pamoja na changamoto za kijiografia, hali inayosababisha, licha ya kujengwa shule za sekondari katika kila kata, baadhi ya maeneo kulazimika kuwa na zaidi ya shule moja, hata kufikia tatu, ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Tumeendelea kuyafikia maeneo hayo kwa kuhakikisha tunajenga shule za kutosha. Kuna kata ambazo hadi sasa zina shule hadi tatu ili kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea kwenda shule,” amesema.
Mdau na mtafiti wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko, akizungumza na Mwananchi amesema ili kutokomeza changamoto hiyo ni vyema kuendelea kuongeza shule katika kata zenye maeneo makubwa ya kiutawala pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi.
Nkoronko amesema Serikali imejitahidi kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari, lakini katika baadhi ya kata, kutokana na ukubwa wa maeneo au changamoto za kijiografia, kunahitajika zaidi ya shule moja.
“Unakuta kata moja yenye vijiji zaidi ya vitano ina shule moja ya sekondari, na vingine vipo mbali zaidi ya kilometa 10 kutoka shule ilipo. Maeneo kama haya yanahitaji kuangaliwa uwezekano wa kuongezewa shule ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu,” amesema.
Nkoronko amesema njia nyingine itakayosaidia kuondoa changamoto hiyo ni ujenzi wa mabweni katika shule ambazo zimebainika wanafunzi wake wanatembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Pia, ametoa angalizo kuwa gharama za bweni zinatakiwa kuwa nafuu ili kumwezesha hata mzazi mwenye kipato cha chini kumudu.
“Ili kuondoa changamoto hiyo, hakuna budi kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa shule nyingine, mabweni, na kuboresha miundombinu ya barabara,” amesema Nkoronko.