KONA YA MALOTO: Masilahi ya kisiasa na upotoshaji historia ya nchi

Nilikuwa bado mdogo. Ni kipindi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishan’gatuka urais. Hata hivyo, alikuwa bado Mwenyekiti wa CCM. Akili zangu za kitoto, niliamini kuwa baada ya Nyerere kukabidhi urais kwa Ali Hassan Mwinyi, asingesikika tena.

Siku hiyo, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), siku hizi TBC Taifa, hotuba ya Mwalimu Nyerere, ilirushwa. Nikajisemea kwa sauti, “kumbe Nyerere bado ana nguvu,” dada yangu aliyenizidi umri wa miaka mitatu, akanikaripia, “wewe ongea tu kwa sauti, utafungwa.” Niliingiwa hofu.

Kumbukumbu hiyo haijawahi kufutika maishani mwangu. Nilikua nikiamini kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa wa kuogopwa, na siyo binadamu wa kumsema kiholela, utajikuta jela. Simulizi za miujiza ya fimbo yake na hadithi zisizosadifu ukweli, kumzunguka, vilifanya nikue nikiamini kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa binadamu aliyejaliwa nguvu za asili kuliko mtu wa kawaida, yaani supernatural human being.

Umri na maarifa vilinisaidia kubadili mtazamo kuhusu Mwalimu Nyerere. Hotuba zake zilijenga ubongo wangu. Uchimbaji wa historia ukanifanya nimpende. Kiongozi mahiri, mwanafalsafa bora ambaye Watanzania wanapaswa kujivunia siyo tu kwa sababu alikuwa Rais wa nchi, bali pia kuchangia naye utaifa ni fahari kubwa.

Nilijenga ufahamu wangu vizuri kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na maono, karama kubwa ya uongozi, utu na uzalendo kwa Tanzania na Afrika, lakini haikumwondolea ubinadamu wake. Kuna mahali alifanya makosa. Hakuwa malaika. Uzuri hata yeye alikiri.

Moja ya hotuba zake akiwa ameshaachia viti vyote, urais na uenyekiti CCM, Mwalimu Nyerere alisema katika kipindi chake cha uongozi, alifanya mambo mazuri na mabaya. Akashangaa wakati wa Mwinyi yale mazuri yake yaliachwa, lakini mabaya yakaendelezwa.

Ukichimba zaidi historia ya Mwalimu Nyerere, unagundua kuwa watu waliomzunguka, kwa mahaba makubwa waliyokuwa nayo kwa kiongozi wao, au kujipendekeza ili kunufaika kisiasa, walijaribu kumpamba kwa sifa za umungu-mtu. Ni hao ambao hawakutaka aachie madaraka, yeye akawagomea.

Ni kuchora mstari kuwa wanasiasa wakiyaona masilahi yao ndani ya mtu fulani, wanaweza kumtukuza na kumjaza upepo wa kila aina. Wanaweza kuifanya jamii isimwone kuwa ni binadamu wa kawaida. Mabaya yake yatafichwa, au kutetewa, halafu mazuri yatashereheshwa kwa ukubwa usiomithilika.

Machi 17, 2026, ilikuwa inatimia miaka mitano tangu tangu lilipotolewa tangazo la kifo cha Rais wa Tano, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli. Lilikuwa tukio kubwa. Salamu na sifa nyingi za pongezi zilitolewa kuupamba wasifu wa Magufuli. Ni jambo jema kumkumbuka. Alikuwa Rais wa Tanzania.

Kosa kubwa ambalo linafanywa, ambalo litaibebesha gharama kubwa historia ya nchi, ni kumpa Magufuli enzi ya umalaika.

Lazima kubaki kwenye mstari kuwa Magufuli alikuwa binadamu. Alifanya mazuri kwa Watanzania na yapo makosa yalitokea kipindi chake. Mema na mabaya yake, vyote vinastahili wino katika uandishi wa historia ya nchi.

Tanzania imeongozwa na marais sita hadi sasa. Ina umri wa zaidi ya miongo sita. Kutoka Dar es Salaam ya vijiji, hadi nchi ya maghorofa mikoa yote, wilayani, barabara za lami zinazounganisha wilaya zote.

Umeme unaotosheleza matumizi ya nchi hadi kuwa na ziada. Unafuu wa huduma za afya, elimu, maji, na kadhalika. Uchumi ulipo, na uwezo wa nchi kibiashara. Ni kazi ambayo imefanyika kutoka kiongozi hadi kiongozi, utawala kwa utawala.

Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, na aliye madarakani hivi sasa, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunganisha na kazi aliyofanya Magufuli, ndiyo matokeo ya Tanzania iliyopo sasa.

Kutoka kiongozi mmoja hadi mwingine, anayerithi uongozi hukuta urahisi ambao ulitengenezwa na mtangulizi wake.

Mwalimu Nyerere hakukuta taifa, yeye akalijenga. Hili pekee, bila kutaja mengine, linatosha kuonesha kazi iliyotukuka ya Mwalimu.

Mrithi wake, Mwinyi, hakuwa na jukumu la kuunganisha nchi, aliikuta tayari. Ongezea ujenzi wa viwanda, viwanja vya ndege, barabara, uwekezaji mkubwa kwenye elimu, afya, ulinzi wa nchi, uwezeshaji wa mikoa kiuchumi, ni sehemu ndogo ya kazi kubwa iliyofanyika wakati wa Mwalimu Nyerere.

Kisha, mwanamageuzi ya kiuchumi, Mwinyi. Kuihamisha nchi kutoka kwenye ujamaa na kuipeleka uchumi wa soko, ikiwa bado kwenye misingi ya ujamaa. Kuanza kubinafsisha taasisi za serikali zlizokuwa mzigo kwa serikali, ili zitengeneze fedha na kujenga nchi. Kuasisi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili iweze kusimamia mapato ya nchi. Huu ndiyo unafuu ambao Mkapa aliukuta na kuuendeleza.

Halafu, kiongozi mnyoofu na muwazi, Mkapa. Alikuwa na kusudi kubwa la uongozi wake, na aliona mzunguko wa fedha aliourithi kutoka kwa Mwinyi, haukutosha. Alianza kubana ndani, na kujitahidi kufungua nje.

Aliwaomba Watanzania wafunge mikanda. Uamuzi huo wa Mkapa uliwezesha kubadili mtazamo wa Tanzania kwenye jumuiya za kimataifa.

Utekeleza wa Sheria ya TRA, iliyosainiwa na Mwinyi mwaka 1995, kisha taasisi hiyo ikaanza kazi mwaka 1996 wakati wa Mkapa. Kuanza kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), mara Tanzania ikaanza kujenga na kuboresha miundombinu yake.

Zamani, kutoka Mwanza au Kagera mpaka Dar es Salaam, ilitakiwa uwe na pasipoti. Mkapa alijenga barabara ya kati. Daraja Mkapa (Mto Rufiji), Daraja la Umoja (Tanzania – Msumbiji).

Kikwete sasa, kilometa zaidi ya 2,000 za barabara za lami, hospitali ya Mloganzila, uboreshaji wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, kwa kuanzisha kitengo cha dharura, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kuiongezea uwezo Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi), Daraja la Julius Nyerere (Kigamboni), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (terminal III), Songwe (Mbeya), Daraja la Jakaya Kikwete (Malagarasi), barabara za mabasi ya mwendo kasi, Dar es Salaam. Alikuza mapato kutoka Sh150 bilioni hadi wastani Sh1 trilioni kwa mwezi. Ni vigumu kutaja vyote.

Rais Samia, miradi yote iliyoanzishwa na Magufuli, ameikamilisha. Tena yeye akijenga kwa asilimia 70. Mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), reli ya standard gauge (SGR), Daraja la Magufuli (Kigongo – Bisisi). Amejenga barabara za mwendo kasi kilometa nyingi Dar es Salaam, akipiku rekodi iliyoachwa na Kikwete.

Kufikisha mapato wastani wa Sh3 trilioni, kutoka Sh1.5 trilioni kwa mwezi kipindi anashika madaraka. Kuipeleka elimu bure kidato cha sita, kutoka kidato cha nne, kama ilivyoachwa Magufuli. Samia amejenga shule nyingi, hospitali na vituo vya afya.

Kila juhudi inapaswa kutambuliwa. Marais wote wametenda mema kwa nchi, na hakuna malaika, ambaye hakutenda makosa. Na hapa ndipo kwenye mjadala kwamba inakuwaje miaka mitano ya Magufuli imekuwa na kushindo kikubwa, wakati Mkapa atatimiza miaka sita kaburini ifikapo Julai 2026? Ukweli ni huu, siasa na mahaba binafsi, vinaharibu historia ya nchi.