Tanga. Jiji la Tanga, linalosifika kwa upepo mwanana wa bahari na mandhari ya minazi, limeendelea kujijengea sifa si kwa utulivu wake pekee, bali pia kwa kuibua wabunifu wanaotumia fursa zilizopo kubadili maisha yao.
Miongoni mwao ni Nafisa Mohamed, mwanamke aliyethubutu kubadili mtazamo wa watu kuhusu chai na kuigeuza kuwa fursa ya kiuchumi.
Katika jamii nyingi, chai imezoeleka kama kinywaji cha kawaida kinachotengenezwa kwa njia ile ile ya muda mrefu. Hata hivyo, kwa Nafisa, hali hiyo imekuwa fursa ya kufikiria tofauti.
Sasa, ameibuka na aina mbalimbali za chai zenye ladha za kipekee, huku chai ya nazi ikiwa kivutio kikubwa zaidi kwa wateja wake.
Nafisa Mohamedi akiwa kwenye aina kumi na mbili za chai alizobuni na kutengeneza na kuwa kimbiliao kwa wakazi wa mkoa wa Tanga na wageni kutoka nje ya mkoa huo. Picha na Mbonea Herman
Anasema safari yake ya ubunifu wa mapishi ya vyakula haikuanza kwa bahati mbaya, bali tangu akiwa mdogo, alikuwa na mapenzi ya dhati kwa kazi za jikoni.
Alipenda kupika na kujaribu ladha mpya, hali iliyomjengea msingi wa ubunifu aliouendeleza baadaye.
“Mimi ni mtu wa jikoni tangu nikiwa mdogo sana. Nilikuwa napenda kujaribu vitu vipya na kujifunza kila siku nikiwa jikoni napika,” anasema Nafisa.
Pamoja na mapenzi hayo, anasema hakuanza moja kwa moja na biashara ya chakula. Awali alijaribu ubunifu katika mavazi, lakini kadri muda ulivyokwenda, aligundua kuwa kipaji chake kikubwa kilikuwa katika mapishi, ndipo alipoamua kurejea kwenye kile alichokipenda tangu utotoni.
Hatua muhimu katika safari yake ilikuja alipoanza kutumia mitandao ya kijamii kujifunza mbinu mbalimbali za utayarishaji wa chai. Kupitia majukwaa hayo, alikutana na mawazo mapya na mbinu tofauti zilizompa msukumo wa kubuni bidhaa yake.
“Nilipoona watu wanatengeneza chai za aina tofauti, nilijiuliza kwa nini nisiwe na ya kipekee hapa Tanga,” anasema.
Akiwa na wazo hilo, alianza kufanya majaribio ya kutengeneza chai ya nazi. Tofauti na wengine, aliamua kutotumia maziwa ya ng’ombe, akilenga kupata ladha halisi ya nazi. Uamuzi huo ulimtofautisha na wengine sokoni na kumpa utambulisho wa kipekee.
Hata hivyo, mafanikio hayakuja mara moja, kwani anakiri kuwa alipitia changamoto nyingi katika hatua za mwanzo, hasa kupata ladha sahihi ya chai. Wakati mwingine nazi ilikatika na kuathiri ubora wa chai, huku wakati mwingine uwiano wa viungo ukihitaji marekebisho.
“Ilinichukua muda mrefu kupata ladha sahihi. Ilikuwa ni majaribio ya mara kwa mara,” anasema.
Katika jitihada hizo, Nafisa anasema jikoni kwake iligeuka kuwa sehemu ya ubunifu wa kila siku. Aliendelea kujaribu, kurekebisha na kuboresha hadi alipofanikiwa kupata ladha aliyokuwa akiitafuta.
Muonekano wa chai ya Nanasi ikiwa kwenye kikombe ikiwa na ladha nzuri na harufu ya kuvutia.
“Nilikuwa najipa moyo na hata kuIzungumza chai yangu, nikiamini siku moja nitafanikiwa,” anasema kwa tabasamu.
Hatimaye, juhudi zake zilizaa matunda. Chai ya nazi aliyobuni ilianza kuvutia watu na kupata wateja wa kudumu. Baada ya hapo, Nafisa alipanua ubunifu wake kwa kubuni aina nyingine za chai.
Kwa sasa, ana zaidi ya aina 12 za chai, ikiwamo ya nanasi, chungwa, biskuti na nyinginezo. Kila moja ina ladha yake ya kipekee na mbinu maalumu ya utayarishaji.
Anasema siri ya mafanikio yake ipo katika umakini na ubunifu, akihakikisha kila kikombe kinatoa ladha bora inayowaridhisha wateja wake.
“Watu wengi wanashangaa kusikia chai ya nanasi au chungwa, lakini wakishaonja tu, wanakuwa mashabiki zangu na wateja wazuri sana,” anasema.
Chai ya nanasi imekuwa miongoni mwa zinazopendwa zaidi kutokana na ladha yake tamu na harufu ya kipekee. Kwa Nafisa, ubunifu huo unatokana na uwezo wa kuona fursa katika vitu vinavyoonekana vya kawaida.
Kadri muda ulivyokwenda, kazi yake ilianza kukubalika na kuvutia watu wengi zaidi. Alipata fursa ya kushiriki katika maonesho mbalimbali ya biashara, ikiwamo Sabasaba na Nanenane, ambako alionesha bidhaa zake kwa hadhira pana zaidi.
Kupitia maonesho hayo, anasema amefanikiwa kujitangaza na kupata wateja wapya kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Umaarufu wake ukaanza kuvuka mipaka ya Tanga, huku wageni wakifika mahsusi kuonja aina ya chai mbalimbali anayopika.
Wengi wa wateja anasema huja kwa shaka, lakini huondoka wakiwa wameridhika na ladha wanayoipata na tabasamu pana.
“Ukinywa chai ya nazi lazima utabasamu. Watu wengi wanarudi tena baada ya kuonja,” anasema.
Kupitia biashara hiyo, Nafisa amejijengea kipato na kubadilisha maisha yake, huku akisaidia familia yake na kujijengea heshima kwa wateja kama mjasiriamali.
“Biashara hii imenibadilisha maisha kwa kiasi kikubwa. Leo nina uwezo wa kujitegemea,” anasema.
Hata hivyo, anakiri kuwa bado kuna changamoto, hususan kwa baadhi ya watu kutokuamini ubunifu huo au kuogopa kujaribu ladha mpya kutokana na mazoea waliyonayo.
“Mtu anaweza kuogopa kujaribu, lakini nikimpa aonje hubadilika na kuwa mteja,” anasema.
Kwa sasa, kikombe cha chai anakiuza kwa Sh1,000, ingawa bei hiyo hubadilika kulingana na upatikanaji wa malighafi sokoni. Anasema anaendelea kuzingatia hali halisi ya soko, ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
Mbali na biashara, Nafisa ana ndoto ya kupanua shughuli zake na kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wake. Anasema anaamini kuwa ubunifu anaoufanya unaweza kukua na kuwa biashara kubwa zaidi siku zijazo.
Muonekano wa chai ya Nazi ikiwa kwenye kikombe ikiwa na ladha nzuri na harufu ya kuvutia.
Anatoa wito kwa wanawake na vijana kuthubutu na kutumia fursa zilizopo katika mazingira yao. Kwa mujibu wake, mafanikio hayahitaji mtaji mkubwa pekee, bali uthubutu na ubunifu.
“Usikate tamaa. Anza na kile kidogo ulicho nacho. Ukifanya kwa bidii na ubunifu, unaweza kufika mbali,” anashauri.
Akizungumzia ubunifu wa Nafisa, mjasiriamali aliyejitambulisha kwa jina la Amanda Mshamu anasema imeakisi namna ambavyo wazo dogo linakua na kuwa fursa kubwa ikiwa litapewa nafasi na kuendelezwa kwa juhudi na uvumilivu.
Mshamu anasema kupitia chai, Nafisa amebadili maisha yake na sasa anawahamasisha wengine kuona thamani ya ubunifu katika maisha ya kila siku.
“Ni jambo zuri hasa kwa sisi tunaoendele kufanya kazi ya ujasiriamali, tuna cha kujifunza kutoka kwake. Ubunifu wake unaonesha namna mafanikio yanavyoanza na hatua moja ya kuthubutu,” anasema Mshamu.
