BURUDANI ya Soka Zanzibar haitegemei wachezaji pekee wakiwa uwanjani, badala yake hata baadhi ya makocha wamekuwa kivutio kwa mashabiki wa mpira visiwani hapa.
Ikitokea timu ina kocha wa aina hiyo, siku ya mechi watu hufika uwanjani si tu kuangalia utaalamu wake, bali hata kufurahia kumwona namna anavyoshangilia baada ya kupata matokeo mazuri.
Kocha wa Fufuni inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 38 baada ya mechi 20, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ ni miongoni mwa makocha wenye ushawishi kwa soka la Zanzibar kwa namna ya ushangiliaji wake wakati timu inapopata matokeo mazuri.
Akifanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti kisiwani hapa kwenye viwanja vya Mao, Mjini Unguja, Gamera anaeleza sababu ya kutumia mtindo maalum wa kushangilia kwenye mechi.
Anasema mitindo anayoitumia ni kwa ajili ya kuwahamasisha wachezaji kuongeza nguvu ya kupambana ili kupata matokeo mazuri na mara nyingi ana msemo wake anaotumia.
“Mimi ndio staa, hakuna staa mwingine zaidi yangu, mimi ndiye nitawafanya wachezaji wangu wajulikane na wapendwe, kwa hiyo nawaambia wanisikilize suala la jukwaani waniachie nitajua nifanye nini,” anasema.
Kocha Gamera anasema huwa anawaambia wachezaji wake akiwa na maana ya kazi yao ni kucheza mpira wakiwa uwanjani, lakini suala la mashabiki linamhusu yeye na sio wao.
Gamera ni kocha kijana aliyefanikiwa kujitengenezea mashabiki wake binafsi ambao wanamsapoti kulingana na timu anayoifundisha.
Kabla ya kuongoza jahazi la Fufuni iliyopanda daraja msimu huu wa 2025-2026, msimu wa 2024-2025 alikuwa Kocha wa Malindi aliyeinusuru isishuke daraja, baada ya hapo timu hiyo iliachana naye na kujiunga rasmi na Fufuni.
Siyo jambo la kawaida kwa timu iliyopanda daraja kuongoza ligi kwa msimu wa kwanza tena zikibaki mechi 10 kabla ya msimu kumalizika, lakini hilo limewezekana kwa Fufuni ya Gamera.
Katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Fufuni ilimaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Zimamoto, lakini hadi sasa zikibaki mechi 10, Fufuni ipo kileleni baada ya kuvuna alama 38.
Gamera anasema ameichukua timu hiyo ikiwa haipo kwenye hali nzuri ila aliamua kupambana nayo hadi kuifikisha hapo ilipo.
Anasema, timu hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuyumba kwa uongozi na uwezo wa kifedha, lakini anashukuru wanasaidiana wenyewe kupunguza changamoto hizo kwa kufanyakazi kwa ushirikiano.
Anaeleza, jambo la kwanza alilofanya baada ya kufika kwenye timu hiyo ni kurekebisha uongozi kwa kuweka misingi mizuri itakayoleta matokeo mazuri, kuelezea mambo anayoyahitaji na kukubaliana na hali aliyoikuta.
Ikiwa ndiyo msimu wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Zanzibar, Fufuni imekuwa miongoni mwa timu zinazofanya vizuri na kufanikiwa kuzifunga timu kongwe ndani ya ligi hiyo ambazo ni Uhamiaji, Kipanga, Polisi, Mwembe Makumbi na Zimamoto.
Haikuwa rahisi, hivi ndivyo unavyosema lakini imewezekana kwa sababu ya timu hiyo kuwa na kocha mwenye uzoefu wa ligi na uwezo wa kuiongoza timu katika nyakati ngumu na nyepesi.
Timu hiyo inapocheza inakuwa na nidhamu na muunganiko mzuri hata ikitokea imefungwa bado inapambana hadi dakika 90 za mchezo jambo ambalo limeteka hisia za mashabiki wao.
Kocha huyo anasema nidhamu ya timu inatokana na wachezaji wake kuwatii na kusikiliza wanayoambiwa na viongozi wao.
Gamera anasema, ingawa amezifunga timu kubwa na mechi kuwa ngumu lakini mchezo dhidi ya KVZ ambao walikuwa ugenini ndiyo ulikuwa mgumu zaidi kwa sababu ulikuwa na fitna ndani na nje ya uwanja japo waliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Gamera anasema msimu huu malengo yao yalikuwa ni kupambana wasishuke daraja, lakini sasa limeongezeka la kuchukua ubingwa kwa sababu nafasi waliyopo.
Anasema ushindani wa ligi msimu huu umekuwa mkubwa ikilinganishwa na msimu uliopita kwani timu nyingi zimesajili vizuri.
Mbali na hilo, anasema matokeo ya aina hiyo yatapatikana kwa mechi 10 zilizobaki kwa sababu ya kuwa na mikakati ya kushinda kila mechi na wamejipanga na hilo.
“Sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunavuna alama tatu kila mchezo bila ya kujali tunacheza na timu gani, la muhimu alama tatu kwa tumejiandaa vizuri kwa michezo yote,” anasema.
Kocha huyo, anasema hakutarajia kuona mafanikio hayo katika kipindi kifupi lakini baada ya kuongoza ligi kwa hatua ya kwanza ndipo walipoamua kuwa hakuna haja ya kuogopa tena zaidi ya kuendeleza mapambano.
Anasema, siri kubwa ya mafanikio hayo ni kuwaweka wachezaji pamoja na kuwafanya kuwa rafiki japo kuna baadhi wanaona kama anawadekeza lakini siyo kweli zaidi ya kujenga umoja na kuwafanya wachezaji wote kuwa sawa.
Anasema kila kocha ana utaratibu wake katika ufundishaji na kukaa na wachezaji kwa upande wake hiyo anaona ndio njia sahihi ya kujenga urafiki baina yao.
“Tukio ambalo msimu huu siwezi kulisahau ni kupoteza mchezo dhidi ya Malindi SC kwa mabao 2-0 kwani ni mchezo ambao tuliutawala na kutengeneza nafasi nyingi, lakini matokeo hayakuja vile ambavyo tulitarajia,” anafichua.
TIMU ALIZOWAHI KUFUNDISHA
Katika maisha yake ya kuwa kocha, Gamera amewahi kufundisha timu ya Small Boy, Bad Boy, Ijitimai, Stritaz ya Mwembeni, Kwerekwe City, Taifa Jang’ombe, Miembeni City, Ngome FC, Malindi SC na sasa Fufuni.
Timu zote ambazo alifundisha zipo Zanzibar hivyo Kocha huyo anatamani kufundisha soka nje ya Zanzibar kwa sababu hiyo ni fursa bado anaisubiria.
Kocha huyo amewataka mashabiki wasivunjike moyo, waendelee kuisapoti Fufuni kwani bado inahitaji kushikwa kwa kila hatua.
MIPANGO YA MECHI ZILIZOBAKI
Katika kuhakikisha mechi kumi za Ligi Kuu Zanzibar zilizobaki Fufuni inaendelea kufanya vizuri, kikosi hicho kinaratajiwa kuanza mazoezi hivi karibuni baada ya kupisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na ndipo kipindi ligi hiyo ilisimama.
Wakati ligi hiyo itakaporejea Machi 28, 2026, Fufuni itashuka dimbani Aprili 2 kucheza dhidi ya Polisi, huku ikiwa na hesabu za kuzicheza vizuri mechi 10 zilizobaki ili kuendelea kusalia kileleni na kuweka rekodi ya kubeba ubingwa katika msimu wa kwanza kushiriki Ligi Kuu.
Hadi sasa, Fufuni ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar baada ya kucheza mechi 20, imevuna pointi 38, kutokana na kushinda 11, sare tano na kupoteza nne, huku ikifunga mabao 26 na kufungwa 14.
Timu hiyo mbali na kuongoza katika msimamo, pia imetoa mchezaji kinara wa mabao ambaye ni Mboni Stephen Kibamba akitupia 10 na asisti 6 katika mechi 15. Kwa sasa nyota huyo amejiunga na Singida Black Stars inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Kipanga 1-3 Fufuni, Mafunzo 1-1 Fufuni, Malindi 2-0 Fufuni, Zimamoto 0-3 Fufuni, Fufuni 1-0 Polisi, Fufuni 0-2 Mlandege, Junguni 1-1 Fufuni, Fufuni 1-0 Chipukizi United, New King 1-1 Fufuni, KVZ 0-1 Fufuni, Fufuni 0-1 JKU, Fufuni 1-0 KMKM, Fufuni 1-0 Muembe Makumbi, Fufuni 1-0 Uhamiaji, Fufuni 4-0 New Stone Town, New Stone Town 2-4 Fufuni, Fufuni 0-0 Kipanga, Fufuni 1-3 Mafunzo, Fufuni 0-0 Malindi, Fufuni 2-0 Zimamoto.
