Vilevile hawa wasaidizi wanaweza kutumia jina la mkuu kwa manufaa yao binafsi, na kuifanya picha ya mkubwa izidi kuwa ya kutisha mbele za umma.
Picha kama hili nililiona kwenye filamu moja kali sana ya enzi zetu. Ilimhusu bingwa mweusi wa ndondi (Mike) aliyesingiziwa kesi ya madawa, akafungwa kwenye gereza moja la hovyo kabisa. Gereza hilo lilikuwa mikononi mwa wafanyabiashara haramu. Wahuni hawa walilitumia gereza kwa kuchezesha kamari za michezo ya mapigano. Hivyo Mike alihitajika kuongeza chachu ya mapigano ili kamari iongezeke thamani.
Humo gerezani alikuwamo bingwa wao Mrusi aliyeitwa Boyka. Jamaa alikuwa hatari zaidi ya duma. Tangu utotoni alipoingizwa gerezani, hakuwahi kupoteza pambano. Na kipigo alichotoa kwa wapinzani wake hakikuwa kipigo cha mbwa mwizi, bali cha nyoka! Aliwaua ulingoni bila Serikali kuingilia, maana gereza kama nilivyosema, lilikuwa mikononi mwa wauza madawa na wala rushwa. Hawa walikula sahani moja na viongozi mafisadi.
Siku moja bingwa wetu Mike alipambanishwa na Boyka. Lilikuwa pambano lisilotabirika kwani Mike alikuwa tishio kubwa kule uraiani. Wakati pambano likiendelea, wapambe wa Boyka waliona wazi kuwa bosi wao akizidiwa nguvu.
Walichanganya dawa za kulevya kwenye maji ya mpinzani wake, wakamshurutisha mpambe wa Mike (aliyekuwa teja) ampatie. Mike lipoyanywa tu akapatwa na wenge na kupoteza pambano hilo.
Kumbuka Boyka hakutoa maagizo hayo na wala hakujua chochote. Lakini siri ikafichuka: Mpambe wa Mike alijinyonga na kutubu kwa ujumbe aliouacha. Boyka alipogondua alichukia kupita maelezo.
Kwa hasira alikwenda kumnyonga kikatili kabisa yule “aliyemsaidia kushinda”. Alionesha kuwa pamoja na dili chafu alizocheza maishani mwake, hakuamini katika dhuluma ya ushindi.
Filamu hii inanikumbusha kuwa kuna watu wanaoamini haki, na wapo wanaoamini longolongo maishani mwao. Ni hatari sana msaidizi anapokuwa dhulmati.
Msaidizi huuvaa upambe, na hukaa kati kama hewa ya ozone. Hakuna mawasiliano baina ya juu na chini yasiyopitia kwake. Yeye ndiye wenye uwezo wa kuzuia kelele za wananchi zisimfikie mkuu, na salamu za mkuu zisiwafikie wananchi wake huko chini kama zilivyo.
Hawa jamaa si wanasiasa. Ni wahuni tu wa mtaani ambao kwa bahati mbaya wamekuwa na ukaribu na Mheshimiwa. Pengine walisoma au kucheza naye utotoni.
Hutokea kwamba wanaijua zaidi michongo fulani fulani ya mjini. Kifupi ni wanaojiona kuwa wanaweza kila kitu. Wana uwezo wa kumsukia dili za chini ya kapeti na kumnufaisha nje ya pato lake rasmi. Wenyewe hufaidika na ukaribu wao kiasi cha kupata fedha bila kufanya kazi rasmi.
Alama zao kubwa ni umiliki wa majumba na magari ya kisasa, fedha za kumwaga na fursa kila sehemu. Wewe unaweza kuhangaikia jambo muhimu maishani mwako bila kufanikiwa.
Pengine huna vigezo vya kufanikiwa au fursa unayoitaka haipo. Lakini ukielewana naye, atapiga simu moja tu, na tatizo linaisha kwa dakika sifuri. Wanakuwa na sauti zaidi ya mawaziri na watendaji Serikalini.
Mwalimu Nyerere alipenda kuwaita watu hawa “kupe”. Jina hili linafanana na lile linalotumika leo na watoto wa mjini, “chawa”. Yote yanamdadavua mtu anayejikomba kuhakikisha na kulinda maslahi ya bosi nje ya utaratibu.
Kama vile ilivyokuwa kwa mpambe wa Boyka, chawa anaweza kufanya maamuzi magumu ili kumsafishia njia bosi wake bila kutumwa na mtu yeyote.
Hili ni jambo linaloharibu sana mahusiano ya kitaifa. Watu wanaodhurika wanaamini moja kwa moja kuwa wanadhuriwa na mkuu. Wananchi wa chini hawawezi kabisa kumwamini kiongozi wao kwa sababu ya wapambe.
Pengine ni nafuu bosi angekuwa dhalimu maana angerekebishwa na wasaidizi wake, lakini chawa huwa hasikii la muadhini wala la mnadi swala. Wasaidizi wote wanamhara. Na anapofyatuka, hali ya hewa ni lazima ichafuke.
Kwa muda mrefu tumesikia matukio ya utekaji hapa Tanzania. Matukio haya ni mageni sana katika ardhi yetu, hasa yanapohusisha raia wa kawaida. Kadhia hii inahusishwa na “machawa” wanaosingizia kulinda maslahi ya Serikali.
Mamlaka zinazoshughulika na ulinzi wa raia hazijaonesha nguvu ya ziada katika kushughulikia kadhia hiyo. Raia wengi wanahisi kuna harufu ya chawa fulani hivi…
Lakini viongozi wetu wanawakataa. Kwa sababu hiyo tunaamini kuwa kuna watu au vikundi vinavyofosi au kusingizia uchawa ili waupige kwa urahisi.
Kama ndivyo, basi mamlaka hazina budi kumhami kiongozi wao kwa nguvu zote. Lengo ni kupunguza maumivu ya wananchi na kusafisha jina la mkuu. Kadiri wanavyolegeza ndivyo idadi ya wahuni inavyoongezeka na wananchi wanavyozidi kuwa hatarini.
Hayajaanza leo na jana. Wapo viongozi waliowabadilikia ndugu na jamaa zao kwa sababu hizo.
Hata Kagame ana hadithi ya kuwashukia watu wake wa karibu baada ya kumharibia kwa wananchi. Hakika machawa hawakubaliki.
