Mafuriko yaathiri kaya zaidi ya 100 Kilombero

Kilombero. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya ameeleza kuwa zaidi ya kaya 100 zimeathirika na mafuriko huku miundombinu ya barabara ya Ifakara Mlimba katika eneo la Mbingu na Lumemo ikiharibika, kufuatia mvua kubwa zinazoendelea wilayani humo

Akizungumza baada ya kutembelea kaya zilizokumbwa na mafuriko Kyobya amesema hadi sasa hakuna taarifa ya vifo vilivyotokana na mafuriko hayo, huku akitaja baadhi ya kata zilizoathirika zaidi kuwa ni Ifakara, Lumemo, Lipangalala, Michenga, Kiberege, Mbingu na Chita.

Aidha DC Kyobya amesema tayari kamati ya maafa na uongozi wa wilaya hiyo umeshachukua hatua za kunusuru maisha ya waliokumbwa na mafuriko hayo kwa kuwahamisha katika maeneo yenye hatari na kuwaweka kwenye makazi ya muda katika Shule ya Msingi Lipangalala na Michemga.

Duka la bidhaa mbalimbali lilipo kata ya Ifakara wilaya ya Kilombero likiwa limezingirwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo na kusababisha mafuriko. Picha Hamida Shariff

“Niwaombe wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye hatari ya mafuriko kuchukua tahadhari kubwa katika kipindi hiki cha mafuriko, hususani kuhakikisha usalama wao na watoto hasa wakati wa kuvuka mito,” amesema Kyobya.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo karibu na wananchi wote walioathirika na mafuriko hayo na inaendelea kufuatilia hali hiyo ili kutoa msaada pale inapohitajika.

Katika hatua nyingine, Kyobya ametoa maelekezo kwa mamlaka za maji Ifakara na Mlimba kuhakikisha wanatibu maji ya visima kwa kuweka dawa ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu na kuharisha, yanayoweza kutokea katika kipindi hiki cha mafuriko.

“Niwaombe wananchi hasa wale waliopo kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuchukua tahadhari za kiafya kwa kuhakikisha wanachemsha ama kutibu maji ya kunywa, kutumia vyoo na kufanya usafi wa mazingira kwani pamoja magonjwa ya kuhara lakini kama wazingira hayatasafishwa mazalia ya mbu yataongezeka na kusababisha ugonjwa wa Malaria,” amesema Kyobya.

Mkuu wa zimamoto na uokoaji wilaya ya Kilombero mratibu Msaidizi Haji Madulika akifanya uokozi kufuatia hali ya mafuriko yaliyotokea kwenye kata mbalimbali za Halmashauri ya mji Ifakara na Mlimba wilaya ya Kilombero kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo. Picha Hamida Shariff

Hata hivyo amesema mpaka sasa hakuna majengo ya umma ambayo yamekumbwa na mafuriko na Serikali kupitia wataalamu wake wakiwemo wahandisi kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), wanaendelea kazi kuhakikisha hali inarejea na shughuli za kila siku za wananchi zinaendelea.

Kufuatia hali hiyo Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kilombero, Khaji Madulika ametoa wito kwa wananchi wa Ifakara kuhakikisha wanachukua tahadhari maalumu kuwalinda watoto wao katika kipindi hiki cha mafuriko yanayoendelea kuikumba wilaya hiyo.

Aidha ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejipanga kwa vifaa na utayari wa kuendelea kufanya uokozi wa wananchi watakaopata madhara ya mafuriko hayo pamoja na kwenye maeneo ya barabara yaliyofunikwa na maji katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Diwani wa kata ya Ifakara wilaya ya Kilombero, Mteke Halfani akiangalia nyumba zilizokumbwa na mafuriko kwenye kata hiyo kufuatilia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo ambapo zaidi ya kaya 100 zimekumbwa na mafuriko. Picha Hamida Shariff

Akizungumza Kwa niaba ya wananchi wa kata ya Ifakara ambayo nayo ni miongoni kwa kata zilizokumbwa na mafuriko, Diwani wa kata hiyo, Mteke Halfani amesema imekuwa ikipata changamoto ya mafuriko kila mwaka kutokana mto Lumemo kupoteza njia yake ya asili na hivyo kumwaga maji kwenye makazi ya watu.

“Huu mto umepoteza njia yake ya asili kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa kando ya mto huo, hivyo umejaa mchanga, magogo na magugu na kusababisha kina cha maji katika mto huo kupungua na kupoteza mwelekeo wake,” amesema Halfani.

Hata hivyo amemuomba mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga kupeleka mtambo wa kufukua na kusafisha mto huo ili urejee kwenye mkondo wake.