Ufahamu ugonjwa uliokatisha maisha ya Lukuvi

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameuelezea ugonjwa wa mshtuko wa moyo, unaojulikana kwa kitaalamu kama ‘Myocardial Infarction’, kuwa ni hali hatari inayotokea pale damu inashindwa kufika vizuri kwenye misuli ya moyo.

Hali hii husababisha sehemu ya moyo kuanza kufa kutokana na uhaba wa oksijeni, jambo linaloweza kusababisha kifo cha ghafla iwapo mtu hawezi kupata matibabu kwa wakati.

Ugonjwa huu ndiyo uliochukua maisha ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi (70) ambaye amefariki dunia saa 1:00 asubuhi ya leo Jumatano, Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Kifo hicho kimetangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka juu ya msiba huo wa Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isiman, Mkoa wa Iringa. Taarifa hiyo imeeleza kuwa mbunge huyo mkongwe amefariki alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa,jijini Dodoma.

Rais Samia amesema: “Tumepoteza kiongozi shupavu, mahiri, mwenye uzoefu mkubwa, mzalendo na mtumishi wa umma aliyelitumikia Taifa letu kwa uadilifu, weledi na kujitolea. Mchango wake mkubwa katika ujenzi na maendeleo ya Taifa letu utaendelea kuenziwa na kukumbukwa siku zote.”

“Ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, familia, wananchi wa Jimbo la Isimani, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania wote kwa msiba huu.”

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Peter Kisenge amesema tatizo la mshtuko wa moyo si tukio la ghafla, bali ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu unaoathiri mishipa ya damu.

“Mshtuko wa moyo hutokea pale mishipa ya damu ya moyo inapoziba kabisa kutokana na kujengeka kwa mafuta kwenye kuta zake. Hii husababisha moyo kushindwa kupata oksijeni,” amesema Kisenge.

Jinsi mshtuko wa moyo unavyotokea

Kisenge ameeleza kuna hatua tatu kuu zinazochangia mtu kupata changamoto ya mshtuko wa moyo.

Kwanza ni kujengeka kwa mafuta kwenye mishipa (plaque) lehemu hujikusanya kwenye kuta za mishipa, hatua inayojulikana kama ‘atherosclerosis’.

Pili ni kupasuka kwa plaque, wakati inapopasuka, mwili huunda damu kuganda ili kujaribu kutibu uharibifu, jambo linaloweza kuziba mshipa.

“Kuziba mshipa kwa kiasi kikubwa husababisha moyo kushindwa kupata oksijeni, na hapo ndipo mshtuko wa moyo unapotokea,” amesema Dk Kisenge.

Daktari mshauri wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kutoka JKCI, Profesa Harun Nyagori amebainisha sababu kuu za mtu kupata mshtuko wa moyo.

Ametaja shinikizo la juu la damu, kisukari, kuwa na lehemu ‘Cholesterol’ nyingi kwenye damu, uvutaji sigara, uzito kupita kiasi, kukosa mazoezi, msongo wa mawazo na historia ya familia yenye magonjwa ya moyo.

“Mshtuko wa moyo si jambo la ghafla, huwa ni matokeo ya miaka mingi ya kuharibika kwa mishipa. Ni muhimu watu wajue viashiria vya hatari na kubadilisha mtindo wa maisha,” amesema Profesa Nyagori.

Wataalamu wanasema hatari huongezeka kadri mtu anavyozeeka. “Wanaume waliopo kwenye  hatari kubwa ya kupata maradhi haya ni kuanzia miaka 65, huku wanawake kuanzia miaka 55. Lakini hata vijana wanaweza kuathiriwa iwapo wana presha, kisukari au unene kupindukia,” anasema Profesa Nyagori.

Peter Kisenge anaongeza; “Hatari pia huongezeka kwa wale wenye historia ya familia yenye magonjwa ya moyo, uvutaji sigara, na maisha ya bila mazoezi. Hizi ni sababu zinazoweza kuzuia au kupunguza ikiwa mtu atajua mapema na kuchukua tahadhari.”

Mshtuko wa moyo ni dharura ya kiafya. Profesa Nyagori amesema, “Mara mtu anapopata mshtuko wa moyo, kifo kinaweza kutokea ndani ya saa sita iwapo hatatibiwa. Matibabu ya kwanza ni kufungua mishipa iliyoziba, mara nyingine kwa kutumia stendi au njia mbadala.”

Dk Kisenge amesisitiza umuhimu wa kinga; “Jua kiwango cha presha, sukari na lehemu. Fanya mazoezi, kula lishe bora, na acha uvutaji sigara. Hii inaweza kuokoa maisha yako.”

Mabadiliko madogo katika mtindo wa maisha yanaweza kupunguza uwezekano wa mshtuko wa moyo. Wataalamu wanashauri pia kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kuzingatia ishara za hatari kama uchovu usioelezeka, maumivu ya kifua, na shinikizo la juu la damu.

“Kujua hatari na kubadilisha mtindo wa maisha ni hatua ya msingi ya kuokoa maisha,” amesisitiza Dk Kisenge.