Thamani ya uwekezaji masoko ya mitaji na dhamana yafikia Sh63 trilioni

Dar es Salaam. Hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya thamani ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji na dhamana imefikia shilingi trilioni 63.15, uwekezaji wa pamoja Sh4.4 trilioni na mauzo ya hisa na hatifungani Sh6.9 trilioni.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, katika hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa shindano kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, pamoja na kutunuku vyeti kwa wahitimu wa kozi ya watendaji katika masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Omar amesema hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa kutungwa kwa miongozo ya masoko ya mitaji na dhamana ya utoaji wa hatifungani za Sukuk kwa kampuni na taasisi za mwaka 2023, pamoja na kanuni za masoko ya mitaji na dhamana za utoaji wa hatifungani zinazowezesha utunzaji na uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii za mwaka 2025.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar

“Sababu nyingine iliyochangia ni kuwepo kwa miongozo ya masoko ya mitaji na dhamana ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji halaiki ya mwaka 2025, ambapo wadau wa masoko ya mitaji na dhamana ni sehemu ya utekelezaji wa sera, mikakati, sheria na miongozo hiyo,” amesema.

Kadhalika, Balozi Omar amesema Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetekeleza mikakati iliyowezesha utoaji wa bidhaa saba za ubunifu na kihistoria zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo.

“Mafanikio haya yanaonesha wazi kuwa soko la mitaji na dhamana ni sehemu muhimu inayoweza kutumika kama njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za miradi ya maendeleo,” amesema.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Waziri Omar amesema bado jitihada zinahitajika kuongezwa ili kuleta uelewa wa shughuli za masoko ya mitaji, na ameipongeza CMSA kwa kuendesha shindano kwa wanafunzi ili kuongeza uelewa kuhusu masoko ya mitaji, ambapo wanafunzi 28,393 wameweza kushiriki ikilinganishwa na wanafunzi 20,000 waliotarajiwa.

Kuhusu wahitimu wa mafunzo ya watendaji wa masoko ya mitaji, Waziri Omar amesema anaamini kuwa weledi na ujuzi walioupata utaleta kiwango cha ushindani wa kimataifa katika utendaji kazi katika sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini.

Katika wito wake, Waziri Omar ameitaka CMSA kutimiza vyema jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini, pamoja na kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2019/20 hadi 2029/30 na mikakati mbalimbali ya Serikali ili kufikia malengo ya Dira 2050.

Pia, CMSA na wadau wa masoko ya mitaji na dhamana wameelekezwa kuendelea kutoa elimu kwa umma, ikiwemo kuimarisha mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati.

Kwa upande wa watoa huduma za masoko ya mitaji na dhamana, amewataka kuzingatia sheria na kanuni za masoko ya fedha na kuimarisha matumizi ya huduma za fedha kwa njia za kidijitali.

Akizungumzia washindi wa shindano hilo Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Lucas Mwimo amesema katika shindano hilo washindi wa kwanza kwa kila shindano kwa upande wa wavulana na wasichana walipata Sh3 milioni, washindi wa pili Sh 2 milioni na washindi tatu Sh1.5 milioni.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa cmsa, Lucas Mwimo akizungumza katika hafla hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa shindano kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu iliyoenda sambamba na  kutunuku vyeti kwa wahitimu wa kozi ya watendaji katika masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa  iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakati kwa washindi wa nne kila upande walipata Sh1 milioni moja washindi wa tano Sh700,000 na washiriki waliosalia miongoni mwa washindi 20 wa nafasi za juu walipatiwa Sh400,000.

Huku washiriki sita kwa pande zote wenye alama za juu zaidi watagharamiwa ziara ya mafunzo, ambapo watatembelea maeneo mbalimbali ili kujifunza zaidi maswala ya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na masoko ya hisa na kampuni kubwa zinazohusika na utoaji huduma katika masoko ya mitaji hapa nchini na nje ya nchi.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesema wameendesha shindano hilo kwa wanafunzi kwa lengo la kujenga uelewa wa masoko ya mitaji na uwekezaji.

Nalitolela amesema shindano hili limetumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ikiwa ni pamoja na mitandao ya kielektroniki kama simu za mikononi na intaneti, ambapo lilikuwa limegawanyika katika sehemu kuu mbili: shindano la maswali na majibu na uandishi wa insha.