Wadau wajadili utekelezaji maboresho ya mitaala na sera ya elimu

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na changamoto za upungufu wa miundombinu na walimu ili kuhakikisha utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa unafanikiwa, wadau wa sekta ya elimu nchini wamehimizwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta hiyo.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Machi 25, 2026 jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi wakati akifungua kongamano la kimataifa la uboreshaji elimu na maendeleo endelevu lililoandaliwa na Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOED).

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Dk Nchimbi amesema mafanikio ya utekelezaji wa sera ya elimu pamoja na mitaala mipya yanahitaji ushirikiano mpana wa wadau wote, ikiwemo sekta binafsi.

Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza wakati wa kongamano la kimataifa la uboreshaji elimu na maendeleo
endelevu lililofanyika leo Machi 25, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali inatambua bado kuna uhitaji wa miundombinu ya elimu pamoja na walimu, jambo linalohitaji juhudi za pamoja ili kufanikisha malengo ya maboresho ya elimu nchini.

“Serikali inaendelea kushughulikia changamoto hizi, lakini tunatambua kuna uhitaji mkubwa wa miundombinu na walimu katika kufanikisha utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa pamoja na matakwa ya sera ya elimu,” amesema.

Kutokana na hilo, Dk Nchimbi amesema ni muhimu wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo wawekezaji wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii kwa ujumla kushiriki katika maeneo tofauti ya maendeleo ya elimu.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera ya elimu ili kuhakikisha mfumo wa elimu unaendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo ya nchi na soko la ajira.

“Maboresho ya mitaala yanalenga kumwezesha mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa, lakini mafanikio yake yanategemea uwepo wa mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia,” amesema.

Aidha, Dk Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wadau kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika elimu kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa.

Amesema elimu bora itasaidia kukuza rasilimali watu yenye ujuzi na ubunifu, jambo litakalosaidia kuongeza tija katika uchumi wa nchi.

Kauli hiyo ya Makamu wa Rais imeungwa mkono na wadau mbalimbali wa elimu walioeleza ushiriki wa sekta binafsi na jamii utasaidia kuharakisha utekelezaji wa maboresho ya elimu nchini.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Dk Georgina Nyangwine amesema changamoto ya miundombinu na walimu ni suala linalohitaji nguvu ya pamoja, huku akisisitiza umuhimu wa wadau kushiriki katika uwekezaji wa elimu.

Baadhi ya wadau wa elimu walioshiriki kwenye kongamano
la kimataifa la uboreshaji wa elimu kwa maendeleo endelevu lililoandaliwa na Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema katika baadhi ya maeneo bado kuna upungufu wa madarasa, maabara na vifaa vya kujifunzia, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa mitaala mipya ikiwa haitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

“Sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kusaidia katika ujenzi wa miundombinu ya shule na utoaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia. Ushirikiano huu unaweza kusaidia kuongeza ubora wa elimu,” amesema.

Kwa upande wake Christina Mangage ambaye ni mwalimu wa sekondari amesema mageuzi ya elimu yanahitaji uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu na miundombinu.

Amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, bado kuna haja ya kuongeza idadi ya walimu na kuboresha mazingira ya kazi ili kuhakikisha wanaweza kutekeleza ipasavyo majukumu yao katika mfumo mpya wa elimu.

“Walimu ndiyo nguzo kuu ya utekelezaji wa mitaala. Hivyo, pamoja na kuboresha miundombinu, ni muhimu pia kuwekeza katika mafunzo na ustawi wa walimu,” amesema Christina.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau mbalimbali kuhusu sera ya sasa ya elimu na mafunzo na marekebisho ya mitaala na athari zake kwa maendeleo endelevu.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye

Sambamba na hilo amesema limelenga kuibua mijadala ya kitaaluma kuhusu, mitaala katika elimu ya msingi, sekondari na elimu ya juu.

“Tumekutana hapa pia kutafakari juu ya maendeleo ya taaluma na nafasi ya elimu ya ualimu kulingana na maboresho ya sera ya elimu na mafunzo na kubadilishana uzoefu wa kimataifa na kikanda, wa namna maboresho ya elimu yanavyoweza kuchangia ukuaji jumuishi na mustakabali wa maendeleo endelevu,” amesema Profesa Anangisye.

Kuhusu maboresho ya mitaala yaliyofanywa chuoni hapo amesema hadi kufikia Februari mwaka huu, jumla ya programu 270 zikiwemo 127 za shahada ya kwanza na 143 za uzamili na uzamivu, zimeshafanyiwa maboresho.

Kati ya hizo, programu 242 zimeshawasilishwa katika Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa ajili ya taratibu za urasimishaji 76 zimesharasimishwa baadhi yake zimeanza kufanya udahili na usajili wa wanafunzi.

Profesa Anangisye amesema asilimia 45 ya programu zilizorasimishwa zinaweza kutolewa kwa mtandao au kwa mfumo wa uso kwa uso na mtandao.