KIUNGO wa Singida Black Stars, Khalid Aucho, ametoa wito kwa waumini wa Kiislamu kuendeleza mema waliyoyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhan hata baada ya kumalizika kwa mfungo huo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aucho alisema kumalizika kwa Ramadhan kusiwe sababu ya watu kurejea kwenye matendo mabaya, bali waendelee kuishi kwa misingi ya swala na toba.
“Kumaliza mfungo ni siku ya furaha lakini pia huzuni, kwa sababu wapo wanaoweza kuyaacha yale mema waliyoyafanya wakati wa Ramadhan,” alisema Aucho.
Alisisitiza kuwa mema yaliyofanywa katika mwezi huo hayapaswi kuwa ya muda mfupi, bali yawe sehemu ya maisha ya kila siku ya muumini.
“Nawaomba watu waendelee na yale mema hadi mwisho wa maisha yao, siyo kuyafanya mwezi mmoja kisha kuyaacha,” Aucho alibainisha.
Pia, alionyesha kuwa moja ya mafundisho makuu ya Ramadhan ni kujinyima na kuwajali wengine, hasa wenye uhitaji, jambo ambalo linapaswa kuendelea hata baada ya mfungo.
“Ramadhan inatufundisha kujali wengine na kuishi maisha ya unyenyekevu; tusikengeuke baada ya kumalizika kwa mfungo,” alisema kiungo huyo.
Alionya kuwa baadhi ya watu huharibu mema yao mara tu baada ya kumalizika kwa Ramadhan kwa kujiingiza katika anasa zisizofaa, hali ambayo alisema siyo nzuri.
Pai, Aucho aliwataka waumini kuendelea kushikamana na ibada na kumkumbuka Mungu kila wakati.
“Tukiendelea na yale tuliyofundishwa na Ramadhan, tutakuwa kwenye njia sahihi na kufikia malengo ya maisha yetu,” alisema.