Heche Aibua Hofu ya Usalama wa Tundu Lissu, Ataka Uwazi Zaidi kwa Mamlaka

Global Publishers
March 25, 2026
0 Comments

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Bara, John Heche, ameibua hofu kuhusu usalama wa Tundu Lissu, akisisitiza kuwa mamlaka zinazomshikilia zinapaswa kutoa maelezo ya wazi kwa umma.

Heche ametoa kauli hiyo jana 24 Machi 2026 katika viunga vya Mahakama (Judiciary Square) jijini Dodoma, wakati wa mapumziko mafupi ya shauri la maombi ya kufanywa marejeo ya mwenendo wa kesi ya mgawanyo wa mali za chama, kesi iliyofunguliwa na Saidi Issa Mohamed na wenzake wawili.

Heche amesema kuwa lolote litakalompata Lissu akiwa chini ya uangalizi wa watu hao, halitavumiliwa na Watanzania wala jamii ya kimataifa, amesema Lissu inatakiwa afanyiwe vipimo na madaktari wake nje ya nchi lakini hajafanyiwa hivyo kwa zaidi ya miezi kumi na moja sasa.

Amesema ni muhimu kwa wahusika kueleza wazi kilichotokea na sababu za hatua zilizochukuliwa dhidi ya mwanasiasa huyo.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho hali ya kisiasa nchini inaendelea kuvuta hisia za wananchi, huku baadhi ya viongozi wa upinzani wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Heche ameongeza kuwa suala la usalama wa viongozi wa kisiasa linapaswa kupewa kipaumbele, akionya kuwa kukosekana kwa uwazi kunaweza kuongeza sintofahamu na taharuki miongoni mwa wananchi.

Stori na Elvan Stambuli, Global Digital