Dodoma. Vyama vya ushirika kote nchini vimeagizwa kutumia mizani ya kidigitali wakati wa kupima mazao ya wakulima, ikiwa ni hatua ya kuondoa udanganyifu na kulinda maslahi ya wazalishaji hao.
Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiege, kupitia waraka aliowaandikia wenyeviti na wajumbe wa bodi wa vyama vya ushirika wa mazao Tanzania Bara.
Katika waraka huo ambao Mwananchi imeupata leo Jumanne Machi 25, 2025, Dk Ndiege ameeleza kuwa utekelezaji wa matumizi ya mizani ya kidigitali unalenga kuhakikisha uwazi katika upimaji wa mazao, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za makusanyo na mauzo.
Amesema matumizi ya mizani hiyo yatasaidia kuondoa mianya ya udanganyifu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiwakwamisha wakulima kupata malipo stahiki ya mazao yao.
Aidha, ameonya kuwa vyama vitakavyobainika kuwa na mizani ya kidigitali lakini vikashindwa kuitumia au kuitumia kinyume na malengo yaliyokusudiwa, vitachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria zinazosimamia sekta ya ushirika.
“Wakulima wanapaswa kuhakikisha mazao yao yanapimwa kwa kutumia mizani iliyounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Muvu), ili kuwawezesha kupata malipo sahihi ya mazao yao. Hatuwezi kuvumilia kuona wakulima wakinyonywa,” amesema Dk Ndiege katika waraka huo.
Pia, amevitaka vyama vya ushirika ambavyo bado havijatekeleza maelekezo ya ununuzi wa mizani hiyo kuhakikisha vinachukua hatua haraka kwa kufuata taratibu za manunuzi pamoja na mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Mrajisi.
Ameweka bayana kuwa vyama vyote vinatakiwa kuwa vimenunua na kuanza kutumia mizani ya kidigitali ifikapo Juni 31, 2026.
Wakati huo huo, Tume ya Maendeleo ya Ushirika inaendelea na juhudi za kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika nchini, ambapo moja ya vipaumbele vya sasa ni kuratibu na kuhimiza matumizi sahihi ya mizani ya kidigitali katika ununuzi wa mazao.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwazi, ufanisi na uaminifu katika sekta ya ushirika, huku ikihakikisha wakulima wanalipwa kwa haki kulingana na uzito halisi wa mazao yao.
