Auwawa kikatili akitoka msikitini | Mwananchi

Tanga.  Tukio la mauaji ya kikatili ya Swalehe Shekanga (60), mkazi wa kijiji cha Mawei, kata ya Soni wilayani Lushoto, limeacha majonzi na hofu kubwa miongoni mwa wakazi baada ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Shekanga aliuawa kwa kukatwa sehemu mbalimbali za mwili wake akitokea msikitini Machi 21, 2026, na mwili wake kukutwa Machi 22, ukiwa na majeraha makubwa yanayoashiria ukatili uliokithiri. Inadaiwa washambuliaji walimvizia njiani kuelekea nyumbani kwake.

Wakazi wa eneo hilo wamesema wanaishi kwa hofu na wametoa wito kwa vyombo vya dola kuwakamata haraka wahusika ili kurejesha amani. Rashed Juma, mmoja wa wakazi, ameomba hatua za haraka zichukuliwe kabla matukio kama hayo hayajaongezeka.

Msemaji wa familia ya Ostadh Swalehe Shekanga ,Hashim Shekanga mkaziwa kijiji cha Mawei kata na Soni katika wilaya ya Lushoto akizungumzia kifo cha kikatili cha baba yake mzazi mzee  Swalehe Shekanga.

Kwa upande wa familia, mtoto wa marehemu, Hashimu Shekanga, amesema tukio hilo limewaacha katika majonzi makubwa kutokana na ukatili uliofanyika. Ameitaka Serikali kuhakikisha wahusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwanafamilia mwingine, Minihaji Shekanga, amesema wanaishi kwa hofu wakihofia tukio hilo linaweza kujirudia iwapo wahusika hawatakamatwa.

Familia hiyo pia imedai kuwepo kwa mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na ndugu yake tangu mwaka jana, wakihisi huenda ukahusiana na tukio hilo. Baba mdogo wa marehemu, Muhilu Kibwana, amesema marehemu aliwahi kusema yuko tayari kufa lakini hawezi kuachia eneo lake.

Waombolezaji wakiwa msibani kwa Ostadh Swalehe Shekanga aliyeuwawa kikatili  kwa kupatwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni panga karibu na nyumbani kwake Mawei wakati alipokuwa akitoka msikitini.

Aidha, ameomba uchunguzi wa kina ufanyike, ikiwemo kuchunguza mawasiliano ya simu ya marehemu ili kubaini ukweli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema uchunguzi unaendelea na kuahidi wahusika watapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, wakazi wa Mawei wanaendelea kusubiri matokeo ya uchunguzi huo huku wakitaka haki itendeke, ili kuzuia matukio ya aina hiyo kujirudia.