Na Mwandishi Wetu.
Katika hatua ya kuondoa mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi, Serikali imezindua utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, utakaowezesha familia ya watu sita kupata huduma za afya 372 kwa gharama ya Sh 150,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Elimu kwa Umma wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, Said Makora, mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote bila kujali uwezo wao wa kifedha.
Amesema kupitia mpango huo, huduma zitakazotolewa zinajumuisha uchunguzi wa maabara, radiolojia, dawa na vifaa tiba pamoja na upasuaji mdogo na mkubwa, kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa za taifa.
Makora alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeweka vyanzo maalum vya mapato vitakavyokusanya takribani Sh bilioni 201.9 katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili kugharamia wananchi wasio na uwezo, huku zaidi ya Sh bilioni 48.2 zikiwa tayari zimekusanywa katika robo ya kwanza ambazo zitakazonufaisha kaya laki 276.
Aliongeza kuwa mpango huo pia unalenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na kudhibiti magonjwa yanayoongoza kuathiri wananchi kama malaria, kifua kikuu na UKIMWI.
Kuhusu walengwa wa mpango huo, alisema tayari zaidi ya kaya 931,000 zimetambuliwa kupitia kanzidata ya TASAF, huku Serikali ikilenga kufikia zaidi ya kaya milioni 3.9 zitakazonufaika na mpango huo, gharama zao zikigharamiwa kikamilifu.
“Mpango huu unakwenda kubadili maisha ya wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya kwa wakati bila hofu ya gharama,” alisema Makora.
Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza umasikini unaosababishwa na gharama za matibabu na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.