Viuadudu vyenye thamani ya Sh23 milioni vyachepushwa Maswa

Maswa. Tukio la wizi wa viuadudu vya pamba vyenye thamani ya zaidi ya Sh23 milioni mali ya Serikali limeibuka katika Kijiji cha Ishima, Kata ya Bugarama wilayani Maswa mkoani Simiyu, huku Katibu wa Chama cha Ushirika wa Msingi (AMCOS) cha Masanwa akidaiwa kuhusika na tukio hilo.

Viuadudu hivyo vilivyokuwa na jumla ya chupa 1,300 aina ya Batamu 175EC na 44EC vililetwa na Bodi ya Pamba Tanzania kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima wa kijiji hicho ili kukabiliana na wadudu wanaoshambulia zao la pamba.

Tukio hilo limebainika baada ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vincent Naano kufika kijijini hapo na kukuta chupa 1,190 za viuadudu hivyo zikiwa zimetelekezwa katika kichaka kilichopo takribani mita 500 kutoka nyumbani kwa mtuhumiwa.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano(wa pili kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ishima kwenye eneo ambalo zilikutwa chupa za viuadudu wa zao la pamba zilizodaiwa kuibiwa. Picha na Samwel Mwanga

Akizungumza leo Machi 25, 2026, Dk Naano amesema tayari amelielekeza Jeshi la Polisi wilayani Maswa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Hili ni suala zito kwa sababu hizi ni mali ya Serikali zilizokusudiwa kuwasaidia wakulima. Nimeagiza polisi wamsake mtuhumiwa popote alipo ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Ishima, Lucas Mwakimwadoto, viuadudu hivyo vilipokewa kijijini hapo Machi 19, 2026 vikiwa vimeletwa na Bodi ya Pamba kwa ajili ya kugawiwa wakulima, lakini baadaye iligundulika kuwa baadhi vimepotea.

“Taarifa ya awali niliipata kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, na baadaye tukapokea taarifa kuwa chupa 1,190 zimepatikana kwenye kichaka karibu na makazi ya mtuhumiwa. Tangu wakati huo mtuhumiwa ametoweka na hajulikani alipo,” amesema.

Mkaguzi wa Bodi ya Pamba Wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk amesema viuadudu hivyo vilisambazwa baada ya kubainika kuwepo kwa mashambulizi makubwa ya wadudu katika mashamba ya pamba.

Amesema hatua hiyo ililenga kuokoa zao hilo ili wakulima wasipate hasara katika msimu huu wa kilimo.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Maswa, Diana Lyimo amesema tukio hilo linaweza kuathiri uzalishaji wa zao la pamba katika eneo hilo.

Amesema zaidi ya hekari 13,000 za mashamba ya pamba katika kijiji hicho ziko hatarini kutopuliziwa kwa wakati kutokana na kuchelewa kwa dawa hizo kuwafikia wakulima.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano(kulia), akiangalia moja ya chupa ya viuadudu vya zao la pamba vilivyoibiwa na kutelekezwa katika kijiji cha Ishima wilaya humo. Picha na Samwel Mwanga

“Kuchelewa kwa viuadudu hivi kunaweza kuathiri uzalishaji kwa kiasi kikubwa kwa sababu wadudu hushambulia zao la pamba kwa kasi,” amesema Lyimo.

Baadhi ya wakulima wa kijiji hicho wameeleza wasiwasi wao wakihofia kupoteza mavuno kutokana na kuchelewa kwa dawa hizo.

Mkulima wa pamba, Sengerema Mwandu amesema mashamba mengi tayari yameanza kushambuliwa na wadudu, hivyo kuchelewa kwa dawa hizo kunaweza kusababisha hasara kubwa.

“Bila dawa hizi kwa wakati tunaweza kupoteza mavuno mengi kwa sababu wadudu wameanza kushambulia pamba,” amesema.

Jilala Mahega amesema wakulima walitegemea msaada huo wa Serikali kuokoa mashamba yao.

“Pamba ndiyo tegemeo letu kubwa la kipato. Kusikia dawa zimepotea kunatupa hofu kubwa,” amesema.