TRAMEPRO – TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MKUTANO WA WADAU WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA NCHINI TANZANIA

Sisi, Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania, tunapenda kuutaarifu umma pamoja na vyombo vya habari kuwa tumeitikia rasmi mwaliko wa Wizara ya Afya kushiriki katika mkutano muhimu wa wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, utakaofanyika jijini Dodoma, Wilaya ya Chamwino, katika Mji wa Serikali Mtumba, tarehe 25 Machi 2026.

Tunautambua mkutano huu kama fursa ya kipekee na ya kihistoria kwa wadau wote wa sekta hii kukutana, kusikilizana na kushiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini. Huu ni wakati muafaka wa kuandika historia mpya ya nafasi ya Tiba Asili Tanzania kwa kuzingatia misingi ya ubora, heshima, uwajibikaji pamoja na utambuzi wa kitaifa na kimataifa.

Aidha, tunasisitiza kuwa malengo ya Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania yanaendana kikamilifu na malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dira ya Taifa ya Maendeleo, pamoja na mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye. Tiba Asili haiwezi kutenganishwa na mazingira, kwani rasilimali zake zinatokana moja kwa moja na bioanuwai ya nchi yetu; hivyo, ulinzi wa mazingira ni msingi wa uendelevu wa tiba hizi. Mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira vinaathiri moja kwa moja upatikanaji na ubora wa dawa asilia, jambo linalohitaji mikakati jumuishi ya uhifadhi na matumizi endelevu.

Katika mazingira ya sasa ya dunia, ambapo kuna ongezeko la magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, Tiba Asili ina nafasi muhimu ya kuwa sehemu ya suluhisho endapo itaendelezwa kisayansi, kusimamiwa kwa weledi, na kuunganishwa na mifumo rasmi ya afya. Vilevile, ukuaji wa teknolojia na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) unafungua fursa mpya za utafiti, uhifadhi wa maarifa ya tiba asilia, uchambuzi wa dawa na utoaji wa huduma bora zaidi. Hivyo, ipo haja ya kuunganisha maarifa ya jadi na sayansi ya kisasa ili kujenga mfumo imara wa afya unaokidhi mahitaji ya taifa na dunia kwa ujumla.

Kupitia mkutano huu, tunasisitiza umuhimu wa kila mtabibu, taasisi na kundi la wadau kupewa nafasi ya dhati ya kuwasilisha mawazo pevu na ya kina yatakayochangia maboresho ya msingi katika usimamizi wa sekta. Tunahimiza kuimarishwa kwa ushiriki na ushirikishwaji wa kweli miongoni mwa wadau wote, wakiwemo Serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu, mashirika ya kijamii na washirika wa maendeleo. Aidha, kuna umuhimu wa kujenga mfumo imara wa kazi za kitaasisi badala ya utekelezaji wa mtu mmoja mmoja ili kuongeza uwajibikaji, ufanisi na uendelevu wa sekta.

Sambamba na hilo, tunahimiza kupanuliwa kwa mahusiano ya kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia dira ya Afya Moja (One Health), kuwezesha ujumuishaji wa Tiba Asili katika mfumo wa Bima ya Afya, kufunguliwa kwa fursa za upatikanaji wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (TMSD), pamoja na kukuza utafiti, ubunifu na maendeleo ya kitaaluma kwa kushirikiana na taasisi za elimu na utafiti. Tunasisitiza pia umuhimu wa Serikali kuijumuisha Tiba Asili katika bajeti ya Taifa kwa uwazi kama sehemu ya mkakati wa afya endelevu.

Aidha, tunabainisha kuwa ipo haja ya kuitazama Tiba Asili kama sekta muhimu ya kiuchumi, yenye uwezo wa kuchangia ajira, kipato cha watabibu na pato la taifa kwa ujumla. Hivyo basi, ni muhimu kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha sekta hii kukopesheka, kuwekeza, na kuendelezwa kibiashara kwa viwango vinavyokubalika, pamoja na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Vilevile, tunatoa wito mahsusi kwa wadau wote kutumia mkutano huu kama jukwaa la kujenga umoja, kuondoa tofauti zisizo za msingi, na kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwa watoa huduma wa Tiba Asili, jumuiya za kijamii na mashirika yasiyo ya kiserikali. Ni wakati pia wa sekta kujitathmini kwa kina na kuchukua hatua madhubuti za kuondokana na imani potofu, vitendo vya ulaghai, uramali usiozingatia misingi ya kitaaluma, pamoja na mienendo inayodhoofisha heshima na uaminifu wa Tiba Asili. Lengo ni kujenga taswira mpya ya sekta iliyo safi, yenye weledi, inayotambulika na kuaminika ndani na nje ya nchi.Huu ni wakati wa kuunganisha nguvu, hekima na uzoefu wetu kwa manufaa ya taifa letu. Muda ni sasa. Tunawahimiza wadau wote kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu muhimu.

Imetolewa na: Simba A. Simba Mwenyekiti Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania

Tarehe: 24 Machi 2026