Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba imemwachia huru Deus Boniphace, baada ya kujiridhisha kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukutosha kuthibitisha bila shaka yoyote kuwa ndiye aliyemuua mama yake mzazi, Cricencia Boniphace (83).
Deus alikuwa akikabiliwa na shtaka la mauaji yaliyodaiwa kutokea Mei 22, 2024 katika Kijiji cha Kihinda, wilayani Kyerwa, ambapo alidaiwa kumshambulia mama yake kwa panga na kusababisha kifo chake.
Hukumu hiyo ilitolewa Machi 18, 2026 na Jaji Lilian Itemba, aliyesema kuwa licha ya kuthibitishwa kuwa marehemu alikufa kifo kisicho cha kawaida, ushahidi uliotolewa haukumuunganisha moja kwa moja mshtakiwa na tukio hilo.
Mahakama ilibainisha mapungufu kadhaa, ikiwemo ushahidi dhaifu wa kukiri kosa, kutowasilishwa kwa taarifa ya onyo, pamoja na kasoro katika mnyororo wa uhifadhi wa vielelezo (chain of custody). Baadhi ya vielelezo muhimu kama nguo zenye damu havikuwasilishwa mahakamani ipasavyo.
Aidha, kulikuwepo na mkanganyiko wa maelezo ya mashahidi na ushahidi wa awali wa polisi, jambo lililoacha mashaka makubwa.
Katika utetezi wake, Deus alikana kuhusika na mauaji hayo, akidai alimkuta mama yake tayari amefariki na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji, ingawa baadaye alikiri kosa hali iliyoongeza utata katika ushahidi.
Mahakama ilisisitiza kuwa katika kesi za jinai, ushahidi wa mazingira lazima uonyeshe hatia bila uwezekano wa maelezo mengine. Kutokana na mashaka yaliyokuwepo, Mahakama iliamua kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo ipasavyo.
Hivyo, mahakama iliamuru mshtakiwa aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa kosa jingine halali.
