Tume Yakanusha Uvumi wa Usajili wa CCTV kwa Watu Binafsi

Global Publishers
March 25, 2026
0 Comments

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imebaini kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa mitandaoni zikidai kuwa kila mwenye kamera za usalama (CCTV) anatakiwa kujisajili na Tume hiyo.

Kupitia ufafanuzi wake, PDPC imeeleza wazi kuwa siyo kweli kwamba kila mtu binafsi mwenye CCTV anatakiwa kujisajili. Kwa mujibu wa sheria, wajibu huo unawahusu taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi, ikiwemo kupitia matumizi ya CCTV.

Tume hiyo imefafanua kuwa taasisi husika zinapaswa kujisajili na PDPC kabla au ifikapo tarehe 8 Aprili, 2026, kama sehemu ya kufuata matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini.

Kwa upande wa matumizi ya CCTV katika makazi binafsi, PDPC imeelekeza kuwa kamera zinapaswa kuelekezwa ndani ya mipaka ya eneo la mhusika pekee. Imeonya kuwa iwapo kamera zitakusanya taarifa nje ya mipaka hiyo na kurekodi maeneo ya umma, matumizi hayo yatakuwa kinyume cha sheria na mhusika atawajibika kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Tume imehimiza watumiaji wa CCTV kuweka alama maalum (signage/notice) zinazoonesha kuwa eneo husika lipo chini ya uangalizi wa kamera zinazokusanya taarifa binafsi. Hatua hiyo inalenga kulinda faragha za watu wanaoingia au kupita katika maeneo hayo.

PDPC imeeleza kuwa itaendelea kutoa miongozo zaidi kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia ya CCTV ili kuhakikisha sheria zinafuatwa na haki za faragha za wananchi zinalindwa.

Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu,
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).