Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameteuliwa kuwa Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, hatua inayolenga kuimarisha juhudi za amani, usalama na diplomasia ya kinga katika ukanda huo muhimu kimkakati.
Kwa mujibu wa taarifa ya AU iliyotolewa leo Jumatano Machi 25, 2026 mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, uteuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf.
Katika nafasi hiyo mpya, Kikwete anatarajiwa kusaidia juhudi za umoja huo kukabiliana na changamoto za kisiasa, migogoro na masuala ya usalama yanayoikabili Pembe ya Afrika.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa majukumu ya Kikwete yatakuwa pamoja na kuendeleza diplomasia ya kuzuia migogoro, kurahisisha mazungumzo ya kisiasa jumuishi na kujenga mazingira ya kuaminiana kati ya wadau mbalimbali wa kikanda.
Aidha, atafanya kazi ya kuimarisha mifumo ya ushirikiano wa kikanda kwa lengo la kukuza amani endelevu na utulivu katika ukanda huo.
Katika kutekeleza majukumu yake, Kikwete atafanya kazi kwa karibu na mashirika mbalimbali ya kikanda na kimataifa, ikiwamo Shirika la Maendeleo la kiserikali la nchi za Afrika Mashariki (IGAD), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ya Shirika la Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa (UN).
Ushirikiano huo, unalenga kuhakikisha kuna uratibu mzuri wa juhudi za pamoja katika kudumisha amani, utulivu na usalama.
Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kimkakati duniani kutokana na nafasi yake katika biashara ya kimataifa na usafirishaji wa bidhaa kupitia njia za majini.
Hali hiyo imeufanya ukanda huo kuwa kitovu cha maslahi ya kisiasa na kiuchumi kwa mataifa mbalimbali duniani.
Katika taarifa yake, Youssouf ameeleza kuwa AU ina imani kubwa na uzoefu wa uongozi wa Kikwete, akisema utaisaidia kwa kiasi kikubwa jumuiya ya kimataifa katika kutafuta suluhu za kudumu kwa changamoto zinazoikabili Pembe ya Afrika.
“Uzoefu, uongozi na hekima ya Rais Kikwete vitatoa mchango muhimu katika kusaidia nchi za ukanda huu pamoja na taasisi za kikanda na kimataifa kushughulikia changamoto zilizopo na kuendeleza amani, utulivu na ustawi wa kudumu,” amesema.
Kikwete ameongoza Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 na tangu amalize muda wake wa urais amekuwa akishiriki katika juhudi mbalimbali za kidiplomasia na usuluhishi wa migogoro barani Afrika na duniani.
Uteuzi wake mpya unaongeza orodha ya majukumu ya kimataifa anayotekeleza baada ya kuondoka madarakani.
