Sh2 bilioni kuzawadiwa wateja wa CRDB

Dar es Salaam. Ikiendeleza hamasa ya kuwajumuisha Watanzania katika huduma za kidijitali, Benki ya CRDB imetenga Sh2 bilioni zitakazotolewa kama zawadi kwa wateja wake watakaoibuka kinara katika matumizi ya huduma za SimBanking.

Kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kimetangazwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo alipozindua msimu wa sita wa kampeni ya Benki ni SimBanking ambayo mwaka huu imeboreshwa na kuitwa ‘SiMBanking Benki Kimpango Wako’.

“Tutakuwa na washindi watakaopatikana kila wiki, kila mwezi na kila baada ya miezi mitatu yaani robo mwaka kabla ya kuwapata washindi wa jumla wa kampeni hii. Zawadi hizi zote zitakuwa na thamani ya Sh2 bilioni,” amesema Nshekanabo.

Tofauti na ilivyokuwa katika misimu mitano iliyopita ambayo mshindi wa jumla alikuwa anaondoka na gari, kampeni ya mwaka huu Nshekanabo amesema imekuja kitofauti kwa kuleta ubunifu wa zawadi.

Katika kampeni za miaka ya nyuma, kulikuwa na mshindi mmoja wa jumla lakini mwaka huu zawadi kubwa zaidi itatolewa kwa washindi watano ambao, Nshekanabo amesema watapelekwa barani Ulaya kufanya ziara katika nchi tatu zitakazotangazwa hapo baadaye.

“Pamoja na safari hii ya siku saba, washindi wetu wote watano watapokea zawadi ya Sh1 milioni kwa ajili ya kufanya manunuzi kipindi watakapokuwa ziarani huko Ulaya,” amesisitiza Nshekanabo.

Ofisa Mkuu wa Fedha ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wateja (hawapo pichani) kwenye uzinduzi wa SimBanking Benki Kimpango Wako.

Licha ya washindi hao watakaoenda Ulaya, Benki ya CRDB imesema washindi wengine watano watapelekwa kutalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa siku tatu mfululizo katika droo zitakazokuwa zikichezeshwa kila baada ya miezi mitatu ya kampeni hiyo. Kama ilivyo ile ya Ulaya, hii nayo italipiwa kila kitu na benki.

Washindi wengine watakaozawadia kila baada ya miezi mitatu ni wateja wanaofanya miamala kwa wakala au miamala ya bila kutumia kadi ya benki ambao watajipatia luninga ya inchi 65   zitakazotolewa kwa washindi 11 kila baada ya miezi mitatu hivyo kuwa na jumla ya washindi 33. Wateja wanaotumia huduma ya Tokenization, kutumiwa hela kupitia SimBanking kwa mtu ambaye si mteja wa Benki ya CRDB, pia wanahusika katika kipengele hiki.

Kwa wateja wanaopata huduma kwa mawakala wa Benki ya CRDB, Nshekanabo  amesema: “Tutatoa zawadi ya fedha taslimu kwa washindi watatu zenye jumla ya thamani ya Sh60 milioni. Mshindi wa kwanza atapata Sh30 milioni wakati mshindi wa pili atapata Sh20 milioni na wa tatu Sh10 milioni.”

Katika kila wiki na kila mwezi, kampeni hii itakuwa inatoa zawadi ya fedha taslimu, simu za kisasa (smart phones) pamoja na kompyuta mpakato. Zawadi hizi zitatolewa kwa wateja, mawakala na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.

Akieleza kuhusu uwezekano wa kupata moja ya zawadi hizo, Nshekanabo amesema kupitia kampeni ya SiMBanking Benki Kimpango Wako, kila Mtanzania anayo nafasi iwapo tu atatumia SimBanking.

“Hata ukifungua akaunti leo na ukaanza kutumia SimBanking, utaingia kwenye droo zetu,” amesema Nshekanabo.

Benki ya CRDB imekuwa ikiendesha kampeni hii kwa miaka kadhaa sasa ili kuwahamasisha wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutumia huduma za benki kidijitali ili kuendana na kasi iliyopo duniani kote, ambako matumizi ya fedha taslimu yanapungua kila siku.

Matunda ya kampeni hii yanazidi kuongezeka kwani zaidi ya asilimia 95 ya miamala yote inayofanywa ndani ya Benki ya CRDB inatumia majukwaa tofauti ya kidijitali yaliyopo.

“Kupitia SimBanking ambayo ni moja ya majukwaa yetu muhimu zaidi ya kidijitali, tumefanikiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma zetu. Sasa hivi mteja anaweza kufungua akaunti, kufanya miamala, kulipa bili, kupata mikopo, kufanya uwekezaji, kukata bima, na hata kusimamia fedha zake zote kupitia simu yake ya mkononi bila ya kufika tawi la benki,” amesisitiza Nshekanabo.