Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuchakachua mbolea na kuwauzia wakulima mbolea bandia katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, huku mfanyabiashara mmoja akitafutwa na polisi akidaiwa kuhusika katika mtandao huo.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kubadilisha mbolea aina ya Fomi na kuipakia katika mifuko ya mbolea aina ya DAP kisha kuiuza kwa wakulima kana kwamba ni bidhaa halisi, jambo linalodaiwa kuhatarisha uzalishaji wa mazao kwa wakulima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema hayo leo Machi 25, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo.
Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni James Nziku (41) mkazi wa Bwawani, Ahmed Abdallah (21) mkazi wa Mji Mwema na Selemani Lameck Msiani (37) mkazi wa Mtaa wa Jogoo mjini Makambako.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo. Seif Jumanne
Kamanda Banga amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika chumba cha kuhifadhia mbolea kinachodaiwa kumilikiwa na mfanyabiashara Ayubu Sanga, ambaye anatafutwa na polisi baada ya kutoroka.
Amesema wakati wa kukamatwa kwa watuhumiwa hao walikuwa tayari wamehamisha mbolea aina ya Fomi na kuijaza katika mifuko 188 ya mbolea aina ya DAP kwa lengo la kuiuza kwa wakulima.
“Katika operesheni hiyo tumekamata mifuko tupu 549 ya mbolea aina ya Fomi yenye ujazo wa kilo 50 ambayo mbolea yake tayari ilikuwa imehamishiwa kwenye mifuko ya DAP,” amesema Banga.
Ameongeza kuwa polisi pia walikamata mifuko mipya 440 ya mbolea aina ya DAP yenye ujazo wa kilo 50, pamoja na mifuko tupu 341 ya kilo tano ya kampuni ya Export Trading Group (ETG), pamoja na mashine iliyokuwa ikitumika kushonea mifuko hiyo.
Kamanda Banga amesema Jeshi la Polisi linamtaka mfanyabiashara Ayubu Sanga ajisalimishe katika kituo chochote cha polisi mkoani Njombe ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuathiri sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa jeshi hilo halitomvumilia mtu yeyote atakayebainika kuvunja sheria.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Beatrice Tarimo amesema walipata taarifa kutoka kwa raia mwema aliyebaini kuwepo kwa shughuli za kupakua mbolea kutoka kwenye mifuko yake na kuijaza kwenye mifuko ya aina nyingine.
Baadhi ya mifuko mitupu ya mbolea iliyokamatwa na jeshi la polisi mkoani Njombe huko mjini Makambako ikitumika kwa ajili ya kuwekea aina nyingine ya mbolea tofauti na jina la mifuko hiyo.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo walichukua hatua za haraka kwa kushirikiana na polisi ili kulinda masilahi ya wakulima.
“Hatua ya kwanza tuliyochukua ni kusitisha shughuli zote za biashara katika eneo hilo kwa kulifunga ghala lililokuwa likitumika kufanya udanganyifu huo,” amesema Tarimo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kampuni ya Mbolea ya TFC Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Samwel Msongwe amesema kitendo cha kutumia mifuko yenye chapa ya kampuni yao kwa udanganyifu huo kimesababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima.
Amesema kampuni hiyo imejitokeza kusaidia uchunguzi ili kubaini waliokuwa wakihusika na mtandao huo wa kuchakachua mbolea.
“Ndio maana tupo hapa kusaidia kukomesha udanganyifu huu ambapo mbolea ya aina nyingine ilikuwa inahamishwa na kujazwa kwenye mifuko yenye chapa ya kampuni yetu,” amesema Msongwe.
Naye Mwenyekiti wa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo Halmashauri ya Mji wa Makambako, Oraph Mhema amesema hatua kali zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na vitendo hivyo ili kulinda sekta ya kilimo.
“Mawakala tunapaswa kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu. Wale wanaoharibu taswira ya sekta hii lazima wachukuliwe hatua,” amesema Mhema.
