Watoto 123,000 wa kaya maskini wasaidiwa Kilimanjaro

Arusha. Zaidi ya watoto na vijana 120,000 wanaoishi katika kaya zenye mazingira magumu nchini wamepata msaada wa huduma za elimu, afya na ustawi wa familia baada ya Shirika la Compassion International Tanzania kutumia zaidi ya Sh119.7 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Fedha hizo zimeelekezwa katika miradi na programu mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuimarisha ustawi wa watoto, kuwajengea uwezo familia na kupanua upatikanaji wa huduma muhimu katika jamii.

Akizungumza leo Machi 25, 2026 jijini Arusha wakati wa mkutano wa mwaka wa maaskofu na makatibu wakuu wanaoshughulika na malezi ya watoto kutoka Kanda za Mlima Kilimanjaro na Ngorongoro, Mkurugenzi wa Compassion International Tanzania, Mary Lema amesema miradi hiyo inalenga kuimarisha malezi na maendeleo ya watoto pamoja na vijana.

Amesema kupitia utekelezaji wa programu hizo, shirika hilo limejikita katika kuboresha huduma za elimu, afya, lishe na upatikanaji wa maji safi sambamba na kuimarisha uwezo wa kiuchumi wa familia.

Kwa upande wa huduma za maji safi, Lema amesema shirika hilo limewezesha kaya 44,216 katika maeneo mbalimbali nchini kupata maji safi na salama, hatua inayosaidia kuboresha afya za watoto na familia zao.

Katika sekta ya afya, amesema watoto na vijana 96,824 wamewezeshwa kupata bima za afya kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Amesema pia wajawazito 1,390 walipata huduma za kliniki na matibabu, ambapo kati yao 1,016 walijifungua salama.

Kuhusu elimu, Lema amesema vijana 7,976 wamehitimu mafunzo ya vyuo na kati yao 4,554 wakiwemo wasichana 2,391 na wavulana 2,163 wamefanikiwa kupata ajira baada ya kushiriki katika programu za mafunzo ya ufundi stadi.

Amesema shirika hilo pia limeendelea kusaidia kaya kuongeza kipato kupitia vikundi vya akiba na mikopo vijijini.

“Tumesaidia kuanzishwa kwa vikundi 499 vyenye wanachama 61,787 ambavyo vimefanikiwa kukusanya akiba ya zaidi ya Sh3.78 bilioni,” amesema.

Aidha amesema watoto na vijana 113,201 wamepata elimu kuhusu kutambua na kuzuia ukatili dhidi yao, huku mabaraza ya watoto 639 yenye wanachama 7,255 yakianzishwa katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Daniel Mono amesema taasisi za dini zinaendelea kufaidika na ushirikiano huo katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Amesema watoto wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini mara nyingi hukumbwa na changamoto za malezi na matukio ya ukatili, hivyo programu hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa jamii.

“Programu hizi zimekuwa mkombozi kwa watoto na vijana wengi kwa kuwapatia malezi bora, elimu pamoja na mafunzo ya ufundi na ujasiriamali bila kujali dini au kabila,” amesema.

Askofu Mono pia amewataka wazazi na walezi kuongeza juhudi katika malezi ya watoto ili kujenga kizazi chenye maadili na kinachoheshimu tamaduni za Kitanzania.