Dar es Salaam. Wataalamu bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kutoka mataifa zaidi ya 20 duniani, watakutana Dar es Salaam Aprili 15 hadi 18, 2026 kujadili mbinu mpya za matibabu ikiwemo matumizi ya akili unde (AI) kwenye matibabu.
Katika mkutano huo Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, ambapo wananchi watanufaika na mkutano huo kwani wataalamu mbalimbali wataanza kambi maalumu ya matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.
Hayo yameelezwa mbele ya waandishi wa habari leo Jumatano, Machi 25, 2026 jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (Tanzania Neurosurgical Society), Dk Othman Kiloloma.
Dk Kiloloma amesema kambi za matibabu zitafanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (KCMC), Hospitali ya Bugando, Benjamin Mkapa na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).
“Tunawakaribisha wananchi ili watibiwe kupitia kambi hizi. Pia, katika kutambua magonjwa haya ya mfumo wa fahamu tumeandaa matembezi ya hisani yenye kauli mbiu, ‘vaa helmeti kichwa hakina spea’.”
Katika wagonjwa ambao tunawaona wengi wenye matatizo ya kichwa asilimia 70 wanatokana na ajali za barabarani na miongoni mwao asilimia 50 ni ajali za bodaboda,” amesema.
Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (Tanzania Neurosurgical Society), Dk Othman Kiloloma.
Amesema kama chama wameamua kutafuta suluhu ya tatizo hilo kutokana na unafuu wake, akisisitiza asilimia 30 ya wanaotibiwa hufariki au hupata ulemavu wa kudumu.
Dk Kiloloma amesema matembezi hayo yanalenga kuwahamasisha vijana hao kuvaa kofia ngumu ili kujikinga na ajali za barabarani.
Baada ya shughuli hizo ambazo zitafanyika kuanzia Aprili 12, Dk Kiloloma amesema zaidi ya wataalamu kutoka mataifa 20 wakiwemo kutoka India, Afrika Kusini, Congo, Misri, Urusi, Pakistan, Kenya, Uganda na Zambia watashiriki mkutano huo.
“Kupitia mkutano huo tutajadili shida tunazozipata, teknolojia mpya ya matibabu ikiwemo matumizi ya akili unde kwenye matibabu,” amesema.
Kuhusu mgeni rasmi, Dk Kiloloma amesema Rais Samia ndiye anayetegemewa kuzindua mkutano huo kutokana na mchango wake mkubwa wa kuimarisha huduma za tiba nchini, ikiwamo kununua mashine za kisasa za CT Scan na MRI kwa kila hospitali,
Pia amesema Rais Samia amekuwa na mchango mkubwa katika taaluma ya madaktari pamoja na kuwawezesha kuzunguka mikoani kuweka kambi za matibabu.
Wakizungumzia manufaa ya mkutano huo kufanyika nchini, mkazi wa Dar es Salaam, Asha Mgeni, amesema ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa ambazo mara nyingi hupatikana kwa gharama kubwa.
“Kwa kawaida matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu ni ghali sana, hivyo ujio wa wataalamu hawa utatusaidia sisi wananchi wa kawaida kupata huduma kwa urahisi na pengine kwa gharama nafuu au bure,” amesema.
Naye Juma Mwita, dereva wa bodaboda, amesema kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kofia ngumu ni muhimu kwa maisha yao ya kila siku.
“Ajali nyingi zinatokea kwa sisi bodaboda, na mara nyingi tunapuuzia kuvaa helmeti. Kama wataalamu wanakuja na elimu hii, itasaidia kuokoa maisha ya vijana wengi,” amesema.
