FANYENI TAFITI, TUMIENI TAKWIMU SAHIHI – WAZIRI MKUU


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wahakikishe kila wakati wanafanya utafiti na kupata takwimu sahihi.

“Maofisa Mawasiliano wote jengeni utamaduni wa kufanya tafiti, kupata takwimu sahihi kabla kuzisambaza kwa wananchi na kuhuisha taarifa za kisekta kwenye tovuti,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Machi 25, 2026) mara baada ya kufungua mkutano wa 110 wa mwaka wa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia TBC uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa PAPU (PICC) jijini Arusha. Mkutano huo unawakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kwa umma.

Waziri Mkuu amewataka watayarishaji hao watumie vipindi walivyonavyo kutangaza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita ili wananchi wapate taarifa sahihi. “Maofisa Mawasiliano wote tumieni kila fursa kutangaza mafanikio ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta zenu ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi za sekta mnazofanyia kazi,” amesisitiza.

Amesema kuwa ili kujihakikisha kuwa wanapata wasikilizaji na watazamaji wengi wa vipindi vyao, wanapaswa kutumia maudhui yaliyo sahihi, ya kuvutia na yenye thamani ili vijana waweze kuyapokea na kufurahia kuyafuata.

Dkt. Mwigulu amewataka watayarishaji hao waandae maudhui yatakayowafikia na kuwagusa vijana kwa lugha wanayoielewa. “Bila kutumia njia na lugha rafiki kwa vijana, taarifa muhimu zinaweza zisifikie walengwa au kushindwa kuwavutia,” amesisitiza.

Amewataka waongeze ubunifu wa kuwasaidia vijana kutambua wajibu wao katika kulinda nchi yao na tunu za taifa ili mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano yaliyofikiwa yasitumiwe kufanya upotoshaji na kuangamiza Taifa.