Mchongo mpya kujiunga Yanga Soccer School.

NDOTO za vijana wanaopenda soka kutoka mtaani zimepata fursa mpya kufuatia ushirikiano kati ya Yanga na kampuni ya Emwani ambao utawafanya kupata nafasi ya kujiunga na mradi wa Yanga Soccer School.

Kupitia mashindano maalum yaliyoandaliwa kutokana na ushirikiano huo ambayo yatafanyika Jumamosi wiki hii Machi 28, 2026 huko Kigamboni kwenye kituo cha TFF, vijana chini ya umri wa miaka 18 wanapewa nafasi ya kuonesha vipaji vyao, wakilenga kupigania nafasi ya kujiunga na mfumo rasmi wa maendeleo ya soka wa Yanga.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema zoezi la usajili limeanza kwa vituo hivyo kuanzia leo Jumatano hadi keshokutwa Ijumaa, akieleza ushindani utakuwa mkubwa kutokana na nafasi kuwa chache.

Ameeleza kuwa utaratibu wa usajili unafanyika kwa njia mbili ya kwanza ni kufika moja kwa moja kwenye eneo la usajili ambapo ni makao makuu ya klabu na ya pili ni kutuma maombi kupitia barua pepe ya Yanga ili kumpa kila kijana nafasi ya kushiriki kupitia kituo chake.

Mbali na kuwapa vijana nafasi ya kuonekana, mashindano haya pia ni sehemu ya akademi na vituo vya soka vya mtaani kabisa kujitangaza na kuonesha ubora wa kazi wanazofanya.

“Ni nafasi ya kuuza kile ulichoandaa kama kituo, kama una vipaji bora basi huu ndio wakati wa kuvionesha ili wapate nafasi ya kufikia ndoto zao,” amesema Kamwe.

Katika kuongeza ushindani, zawadi nono zimewekwa mezani ambapo bingwa ataondoka na kombe pamoja na Sh3 milioni huku mshindi wa pili akipata Sh1 milioni na timu zitakazotolewa hatua ya nusu fainali zikijinyakulia Sh500,000 kila moja.

Kwa upande wake, Leonard Kachebonaho, ambaye pia anafahamika zaidi kwa jina la Leo Mendez kutoka Emwani, amesema wameguswa na mradi wa Yanga na kuamua kuunga mkono jitihada hizo kwa lengo la kusaidia kukuza vipaji vya vijana nchini.

Amebainisha kuwa, kupitia ushirikiano huo, vijana 10 watakaong’ara zaidi watapata ufadhili wa moja kwa moja kujiunga na Yanga Soccer School kwa mwaka mzima, hatua inayoweza kubadili kabisa mwelekeo wa maisha yao.