Mradi wa uwezeshaji wanawake na jamii kwa ujumla wa ‘Engage’ umetajwa kuwa chachu muhimu ya mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wanawake katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Hayo yameelezwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Engage uliofanyika katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam, ukihitimisha mzunguko wa utekelezaji wa mradi huo wa zaidi ya miaka sita.
Akizungumza kando ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali, amesema mradi huo umeongeza kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wanawake katika maamuzi na kuimarisha uongozi wao katika jamii.
Amesema kupitia mbinu bunifu na shirikishi, wanawake wamewezeshwa kujitambua, kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali, Akizungumza kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Engage uliofanyika katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam.
Aidha, Gemma Akilimali alibainisha kuwa mkutano huo umeleta pamoja viongozi, wanaharakati na wabunifu wa mabadiliko kutoka nchi mbalimbali ili kubadilishana uzoefu na kujenga mshikamano wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Coady Institute, Eileen Alma, amesema ushirikiano wa kimataifa kupitia mradi wa Engage umewezesha wanawake wengi kupata ujuzi wa uongozi na kujitegemea kiuchumi.
Ameongeza kuwa programu hiyo inalenga kukuza uongozi wa wanawake katika sekta isiyo rasmi kupitia mbinu za kifeministi zinazotambua rasilimali zilizopo katika jamii, hali inayochochea maendeleo endelevu.
Naye Mratibu wa mradi huo, Anna Sangai, amesema wanufaika wamepata fursa mbalimbali zikiwemo ujasiriamali, ushiriki katika utawala wa jamii na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa mradi huo, Anna Sangai,Akizungumza kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Engage uliofanyika katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).Baadhi ya wanufaika, akiwemo Maria Mwigune, wamesema mradi huo umebadilisha maisha yao kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kujiamini katika nafasi za uongozi.
Katika mkutano huo, zaidi ya wanawake 100 kutoka nchi za Bangladesh, Ethiopia, India, Canada, Haiti na Tanzania walishiriki, wakijadili mafanikio ya mradi pamoja na mwelekeo wa baadaye wa uwezeshaji wanawake duniani.
Kwa mujibu wa waandaaji, mradi wa Engage umejikita katika maeneo muhimu ikiwemo mustakabali wa kazi, uongozi wa wanawake, ushiriki wa kijamii, pamoja na kupunguza umaskini kupitia mbinu zinazozingatia rasilimali za jamii.
Mkutano huo unatarajiwa kuacha alama muhimu kwa kuimarisha mitandao ya kimataifa na kuendeleza juhudi za pamoja katika kukuza usawa wa kijinsia na uongozi wa wanawake katika dunia inayobadilika kwa kasi.







.jpg)












