KUNA taarifa zinazomhusu winga wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo kuwa mbioni kujiunga na Yanga baada ya mabosi wa klabu hiyo kuonekana kuvutiwa na uwezo wake.
Chobwedo ambaye huu ni msimu wake wa pili anacheza Ligi Kuu Bara, alianza kuitumikia KenGold 2024-2025 ambapo timu hiyo ilishuka daraja, ndipo akasajiliwa na TRA United msimu huu 2025-2026.
Nyota huyo ghafla amekuwa akitrendi, jina lake likitajwa kati ya vipaji vikubwa na vya kuchungwa nchini ambapo kutrendi kwake kumekuja baada ya kuonyesha kiwango kizuri wakati TRA ilipotoka suluhu dhidi ya Yanga, mechi hiyo ilipigwa Machi 19, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha huku nyota huyo akinyakua tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Baada ya mechi hiyo, ziliibuka tetesi za nguvu kwamba Chobwedo yupo katika mazungumzo na viongozi wa Yanga, huku wengine wakisema tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili.
Ilipomalizana na Yanga, TRA United ikaenda kucheza dhidi ya Simba ambapo ilipoteza kwa mabao 3-0 ugenini, huku pia Chobwedo akiendeleza moto wake licha ya kutoisaidia TRA kupata pointi.
Baada ya mechi hiyo, Mwanaspoti lilipata taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa Yanga waliondoka na Chobwedo kwa ajili ya kwenda kumalizana naye ili msimu ujao avae jezi ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.
Mwanaspoti lilimtafuta Chobwedo kuzungumzia dili hilo ambapo alionekana kutokuwa tayari huku akisema kwa sasa yeye ni mchezaji wa TRA United, hivyo hawezi kuzungumzia madili na timu nyingine.
“Kuhusu kutakiwa na Yanga mimi sijazungumza nao, mimi ni mchezaji wa TRA, hivyo siwezi kuzungumzia klabu nyingine, halafu timu zinamchukua mchezaji baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu, huwezi kusema wanakuchukua kisa nimecheza mechi mbili mfululizo, kiukweli binafsi najiona bado nina safari ndefu ya kupambana,” alisema Chobwedo anayemiliki bao moja katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Ikumbukwe kuwa, kuzungumzwa zaidi kwa Chobwedo kuliongezeka baada ya TRA kufungwa mabao 3-0 na Simba ambapo nyota huyo alipongezwa na Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally kutokana na kiwango alichoonyesha.
Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Chibwedo alisema: “Kuhusu mechi dhidi ya Simba siwezi kujisifu kama tulicheza vizuri ama nilifanya vizuri, kwani wenzetu waliibuka na ushindi na sisi hatukuvuna pointi.”
Alipoulizwa kutamani kuzichezea Simba na Yanga, alisema: “Kama zitanihitaji baada ya kumaliza mkataba wangu na TRA nipo tayari ila siyo kwa sasa, ninachokizingatia ni huduma yangu iifae timu na kuyatendea kazi yale ambayo kocha ananielekeza kila wakati.”
Kuhusu namna alivyopokelewa na mitandao ya kijanii, anasema hilo linampa chalenji ya kupambana kuhakikisha anakuwa na muendelezo wa kucheza kwa kiwango cha juu, alichokigundua ni mashabiki nchini wanapenda mchezaji anayefanya kazi nzuri.
“Ndiyo kwanza nina misimu miwili pekee katika Ligi Kuu, nina safari ndefu ya kupambana ili kuja kuzifikia ndoto zangu, ndiyo maana sipendi kulewa sifa kwa namna yoyote ile, kama mashabiki wamekiona kipaji changu nawashukuru kwa kunitia moyo, pia namshukuru Ahmed Ally baada ya mechi alinifuata na kuniambia niendelee kupambana na nimewapa chalenji katika mechi hiyo,” alisema.
Chobwedo safari yake ya mpira wa miguu ilianzia TMA ya Championship, kisha dirisha dogo 2024-2025 akasajiliwa KenGold iliyokuwa Ligi Kuu kabla haijashuka daraja msimu huo, ndipo akatimkia TRA United alipo sasa.
“Japokuwa soka bado nalidai, angalau nauona mwanga, yapo mambo nimeyafanya ya maendeleo kupitia kazi yangu, ninachokizingatia ni kupambana kwa bidii kuja kuziishi ndoto zangu,” alisema Chobwedo ambaye pesa yake ya kwanza kubwa kuimiliki ilikuwa Sh10 milioni.