Karata ya kwanza Stars Fifa Series

TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’, leo itakabiliana na Liechtenstein katika mechi ya Fifa Series kwenye Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Kabla ya mechi hiyo itatanguliwa na Aruba ikicheza dhidi ya Macau uwanjani hapo kuanzia saa 7:30 mchana. Washindi wa mechi  mbili watasonga mbele kucheza fainali Machi 29, mwaka huu, huku zitakazoshindwa zikikutana katika kusaka nafasi ya tatu.

Kuelekea mashindano hayo,  Stars inaonekana kuwa timu yenye nguvu zaidi kulingana na viwango vya karibuni vya Fifa.

Tanzania kwa sasa iko nafasi ya 110 duniani ikiwa na pointi 1,186.14 mbele ya Aruba (ya 191), Macau (ya 193) na Liechtenstein ambao wako katika nafasi ya 205 na ndio timu iliyo katika nafasi ya chini kabisa katika kundi hilo.

Licha ya faida ya nafasi hiyo, kiwango cha hivi karibuni kinaonyesha ushindani. Liechtenstein wamepitia mfululizo mgumu, wakipoteza mechi zao zote za hivi karibuni. Vichapo vyao ni pamoja na kupoteza kwa mabao 7-0 dhidi ya Ubelgiji katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, pamoja na vipigo dhidi ya Wales (1-0), Montenegro (2-1), Kazakhstan (4-0), na Makedonia Kaskazini (5-0).

Kwa upande mwingine, Taifa Stars imeonyesha ustahimilivu katika mechi za hivi karibuni, hasa wakati wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) nchini Morocco.

Taifa Stars iliishia 16 bora ikifuzu kwa mara ya kwanza hatua hiyo ambapo hatua ya makundi ilitoka sare ya 1-1 mara mbili dhidi ya Tunisia na Uganda, ikafungwa 2-1 na Nigeria. Hatua ya 16 bora iliondoshwa na wenyeji Morocco kwa kufungwa bao 1-0.

Zaidi ya hayo, Tanzania ilifungwa 4-3 na Kuwait katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa hivi karibuni.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, alisema: “Tumefanya mazoezi vizuri Dar es Salaam na hapa Kigali. Wachezaji wako tayari, na tunalenga kupata matokeo chanya. Tunawaheshimu wapinzani wetu kwa sababu pia wanalenga lengo moja.”

Fifa Series 2026 ni toleo la pili la mashindano hayo ambayo yanaangazia mechi za kirafiki kati ya timu za taifa kutoka mashirikisho tofauti ya bara.

Toleo hili litaangazia makundi tisa yaliyogawanywa kwa timu nne unaofanyika katika nchi nane zilizopewa uwenyeji kuanzia Machi 25 hadi 31 mwaka huu.

Tanzania kituo chake ni Rwanda ikitumia Uwanja wa Kigali Pele ambapo ipo na nchi za Aruba, Liechtenstein na Macau, huku mechi zikichezwa Machi 26 na 29. Awali ilipangwa kwenda Mauritius, lakini ikahamishiwa Rwanda baada ya nchi hiyo kujiondoa katika nafasi ya kuwa mwenyeji.