Hiki hapa kilichoikwamisha Dewdrop kesi ya mamilioni

Arusha. Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma imefuta kesi ya madai ya Sh500 milioni iliyofunguliwa na Kampuni ya Vinywaji ya Dew Drop Limited dhidi ya Kampuni ya Lemon Dove Limited, kwa madai ya ukiukaji wa hakimiliki na chapa ya biashara.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Augustine Rwizile, baada ya kupitia pingamizi zote za awali zilizowasilishwa na mlalamikaji na kukubaliana na pingamizi moja kati ya manne yaliyowasilishwa na mlalamikaji katika kesi hiyo ya madai.

Mlalamikaji alikuwa akidai fidia kwa ukiukwaji wa hakimiliki na chapa ya biashara akidai mlalamikiwa aliiga bidhaa yenye chapa ya ‘Heru water’ hususani katika chupa za ujazo wa mililita 1,500 na mililita 600 ambapo aliiga muundo na nembo ya chupa ambazo zilisajiliwa kisheria.

Mlalamikaji alidai fidia biyo kama adhabu kwa mlalamikiwa kukiuka kwa makusudi na wazi hakimiliki na chapa yake ya biashara ambapo aliomba gharama za kesi na nafuu zingine za mahakama.

Mlalamikiwa kupitia wakili wake, aliwasilisha pingamizi la awali lililokuwa na sababu nne ambazo ni malalamiko hayo hayana uwezo kufikishwa mahakamani kwani yamekiuka kifungu cha 13 (1),(2),(3) na (4) cha Kanuni ya utaratibu wa madai na kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza na kuamua kesi ambayo chapa ya biashara imesajiliwa na Shirika la Kikanda la Afrika la Haki Miliki (ARIPO) na kuwa mlalamikaji hana nafasi ya kushitaki pamoja na kukosekana kwa azimio la bodi la kuidhinisha kufungua kesi.

Baada ya kusikiliza hoja ya pande zote mbili, Mahakama imesema kuhusu pingamizi la kwanza, kutofuatwa Kifungu tajwa juu, ambacho kinataka wahusika kuchukua hatua ili kutatua mgogoro kabla ya kufungua kesi, ambacho pia hakisemi wazi kuhusu kutochukua au kuonyesha hatua hizo kunafanya kesi isiweze kuendelezwa.

Baada ya kupitia hoja hiyo kwa kina mahakama iliitupilia mbali na kueleza kuwa kushindwa kuonyeshwa kwa hatua zilizochukuliwa kutatua mgogoro nje ya mahakama hakuondoi haki ya mlalamikaji kuanzisha kesi.

Kuhusu pingamizi la pili, Jaji Rwizile amesema kuhusu chapa kusajiliwa ARIPO na usajili ulishaisha muda wake kabla ya kuanzishwa kwa kesi amesema Mahakama imechunguza na kubaini chapa hiyo ilisajili Februari 3, 2016 ingawa muundo wa chupa unaonekana kusajiliwa chini ya kanuni za ARIPO, ila chapa ya biashara yenyewe ilisajiliwa nchini, hivyo mahakama hiyo ina mamlaka kusikiliza.

Amesema usajili wa Dew Drop Limited ulikuwa umekwisha muda wake, na mlalamikaji hakufanyia upya kabla ya kuanzishwa kwa kesi, hivyo basi hakuwa na haki ya kisheria ya kudai fidia.

“Hakuna uthibitisho katika kesi na uwasilishaji kuwa hilo lilifanywa upya kabla ya kufungua kesi hii, ni maoni yangu leseni inapoisha muda wake huacha kutumika,” amesema

Baada ya mahakama hiyo kukubaliana na pingamizi moja kati ya manne, Jaji Rwizile alihitimisha kwa kueleza kuwa kesi hiyo imefutwa na gharama kutokana na kutokuwa na uwezo mbele ya Mahakama.

Awali wakili wa mlalamikiwa alisisitiza kwamba mlalamikaji hakuwa na uwezo wa kuanzisha kesi bila kuonyesha ushahidi wa hatua halisi za kutatua mgogoro wa kibiashara kabla ya kufungua kesi, jambo linalohitajika kwa mujibu wa kifungu cha 13(2) cha Kanuni ya Utaratibu wa Madai.

Alieleza kwamba notisi ya madai haikuambatana na ushahidi wa kuwasilishwa kwa mlalamikiwa hivyo kukosa utaratibu wa kisheria.

Aidha, wakili huyo alisisitiza kwamba Dew Drop Limited ilikuwa na haki ya kipekee ya kutumia chapa yake kutokana na usajili wa ndani wa Tanzania tu, na kwamba usajili uliotolewa chini ya ARIPO haukuthibitisha mamlaka nchini Tanzania, kwani Itifaki husika haijaidhinishwa hapa nchini.

Wakili huyo amedai kwamba usajili wa chapa ya biashara ya Dew Drop Limited uliisha muda wake Februari 3, 2023, miaka saba baada ya usajili wa awali mnamo Februari 3, 2016 na kuwa kesi iliwasilishwa Oktoba 9,2025 bila ushahidi wa kuhuisha usajili.

Amedai kutokana na sababu hizo mlalamikaji hakuwa na haki ya kisheria ya kuanzisha kesi kwa ukiukaji wa hakimiliki au chapa ya biashara, kwa sababu usajili haukuwa na nguvu yoyote ya kisheria wakati ukiukaji unaodaiwa ulipotokea.

Kwa upande wake wakili wa mlalamikaji, alipinga pingamizi zote kwa kudai kwamba mlalamikaji alifuata masharti ya kisheria, ikiwemo kutoa notisi ya madai Septemba 24, 2024, na kwamba mlalamikiwa alikuwa na ufahamu wa mgogoro.